Pengine unaweza kuja na jibu kuwa wapinzani wao ni dhaifu mno msimu huu. Lakini mimi naamini kuwa hili ni jibu sahihi pale Bundesliga kwenye kesi ya Bayern Munich au hata PSG pale Ufaransa lakini sio pale Uingereza. Ubora wa Man city msimu huu hautokani na udhaifu wa wapinzani wao wakubwa bali matumizi sahihi ya pesa na mbinu za kiufundi. Pale Ujerumani pesa yote anayo Bayern ananunua mchezaji anaemtaka. PSG wana ubora mkubwa kitimu kuliko wapinzani wao lakini kwa Uingereza timu kubwa zina pesa na watu lakini zilishindwa kuwa na mikakati makini nazo.
Ubora wa City haupo tu ndani ya uwanja bali nje pia na hapa ndipo wapinzani wote waliposhindwa lakini sio kwamba wao wamekuwa dhaifu sana, Hapana! Walikosa mipango na mikakati ya kuwa tofauti kama ilivyo kwa City. Ubora wa City ni matokeo chanya ya mikakati makini na ubora mkubwa wa rasilimali watu wake. Ubora wa Man city msimu huu unatokana na….
UWEKEZAJI
Ni wazi kuwa fedha haichezi lakini inapowekezwa vizuri na kwa wingi basi huwa na athari kubwa sana ndani ya uwanja. Manchester City hawakuona tabu kuwekeza zaidi ya pauni milioni 200 peke yake kwa ajili ya safu yake ya ulinzi. Ni wazi ubora wa City umetokana na uwekezaji mzuri uliofanyika wa pesa za Sheikh Mansour.
MFUMO WA UCHEZAJI
Baada ya kufanya biashara nzuri alichofanya Pep Guardiola ni kuingiza mfumo wake. Mfumo wa Pep ni Tikitaka. Mpira wa pasi nyingi na wa umiliki mkubwa. Timu zote za Pep zinacheza kuanzia nyuma na zinakaa zaidi na mpira. Jambo hili limewapa wakati mgumu wapinzani hasa kwenye kuutafuta na kujaribu kumiliki mpira na kuanza mipango yao. City hawakupi muda huo. Ingizo la golikipa Ederson limesaidia sana kuimarisha mfumo wa Pep hasa kutokana na uwezo wake mkubwa wa kukaa na mpira mguuni lakini pia kuugawa kwa usahihi mkubwa kwenda mbele.
MABADILIKO BINAFSI YA WACHEZAJI
Guardiola amewafanya baadhi ya wachezaji wa wastani kucheza katika kiwango cha dunia msimu huu. Raheem Sterling akiwa mfano. Guardiola amepandisha baadhi ya viwango vya wachezaji wake. Tazama Sterling alivyo na mchango mkubwa pale City msimu huu. Guardiola amemtengeneza kijana huyu vile anavyotaka yeye. Mara kadhaa Sterling amekuwa akikopi na kupesti maelekezo ya mwalimu wake mazoezini akiwa ndani ya uwanja kwneye mechi za ushindani. Amewabadilisha John Stones na Nicholas Otamendi pia wawe na uwezo mkubwa wa kukaa na mpira mguuni na haishangazi kuwa Muargentina huyo ndio mpiga pasi nyingi zaidi kwenye ligi kuu.
UBORA WA MCHEZAJI MMOJA MMOJA
Kevin De Bruyne anaweza kuwa ameanza kupika mabao kwa miaka kadhaa sasa lakini msimu huu ndio anahusishwa kabisa na kuwania tuzo ya mchezaji bora. Ubora wake binafsi umekuwa ni msaada mkubwa kwenye kikosi cha Manchester City msimu huu. Mikakati karibu yote hasa ya kushambulia kwa upande wa City huwa lazima ipitie kwake. Miguu ya Sane imekuwa na udambwi dambwi mwingi sana. Kumzuia winga huyu wa Kijerumani kunahitaji kazi ya ziada sana. Ukiachana na uwekezaji na mfumo wa Pep lakini ubora wao wa ziada wa nyota hawa umekuwa ni bonasi kubwa sana ndani ya uwanja.
Kama ni fedha na wachezaji wazuri basi wapinzani wote wa City wanavyo. Utasemaje ni dhaifu? Ubora wa City msimu huu umetokana na matumizi na mikakati yao makini lakini sio kwamba wapinzani walikuwa wabovu sana. Hapana! Liverpool hawakuwekeza mahala walipotakiwa hasa kufanya hivyo mwanzoni mwa msimu, Mbinu za Conte zimesomwa na wapinzani wengi msimu huu na zimetumika kumdhibiti yeye mwenyewe. United wamekuwa waoga kwenye mechi kubwa, Spurs wamekosa uzoefu zaidi kwenye timu lakini Arsenal ndio hata hamasa na ari hawana. Timu zijipange na zije kumla changamoto city lakini sio kwamba zimekuwa dhaifu. Ubora kimipango na kimpira haukuifikia City.