Jana Jurgen Klopp alifanikiwa kumaliza utawala wa Manchester City wa kwenda
mechi mechi 22 bila kufungwa.
Anazidi kujiwekea rekodi nzuri dhidi ya Pep Guardiola, mpaka sasa
katika michezo 12 waliyokutana Jurgen Klopp kafanikiwa kushinda
michezo 6 na kutoka sare mchezo mmoja huku Pep Guardiola akishinda
mechi 5.
Jana Manchester City walicheza mfumo wa 4-3-3, wakati Liverpool pia
walitumia mfumo wa 4-3-3 baada ya kupata goli walibadirika na kuanza
kutumia mfumo wa 4-5-1.
Kumwanzisha Andrew Robertson upande wa beki wa kushoto dhidi ya timu
ambayo wachezaji wake wa pembeni wamehusika kwenye magoli kwa kiasi
kikubwa ilikuwa kama kamari.
Mchezaji ambaye alikuwa na michezo nane (8) kabla ya mchezo wa jana
akapambane na Raheem Sterling ilikuwa ni kuinamisha kichwa na kujidai
kutokuona kinachotokea.
Lakini Andrew Robertson alifanikiwa kumzuia Raheem Sterling na hii ni
kutokana na sababu kuu moja.
Mabeki wote wa pembeni wa Liverpool ( Gomez na Robertson ) walikuwa
wanapanda kwa tahadhari mbele kwenda kusaidia mashambulizi.
Asilimia kubwa ya muda wao waliutumia nyuma kuwakaba Sane na Sterling
hali ambayo iliwanyima uhuru kwa kiasi kikubwa.
Ilikuwa ni mara chache kwa Lovren na Matip kuonekana wakienda kusaidia
upande wa kushoto au kulia kwa sababu muda mwingi Robertson na Gomez
walikuwepo kule.
Hali ambayo iliwafanya pia kina Matip na Lovren kusimama eneo moja ,
eneo ambalo walisimama na Sergio Aguero kwa muda wote.
Kwa kiwango cha jana cha Sergio Aguero kimeonesha kwanini Alexie
Sanchez anahitajika katika kikosi cha Manchester City.
Kwa sababu, jana Sergio Aguero muda mwingi alitumia kukaa eneo moja.
Kitu ambacho kilikuwa rahisi kwa mabeki wa kati wa Liverpool kuendana
nacho.
Hakuwa na mijongeo au kasi ambayo ingewalazimu mabeki wa kati wa
Liverpool kufanya makosa binafsi.
Pia hakuna uwazi uliotengenezwa sehemu ya nyuma ya Liverpool ili
kuweza kuwasaidia kina Kelvin De Bryune, Gundogan kuutumia wakitokea
katikati, kwa sababu ya Aguero kutumia muda mwingi akiwa eneo moja
bila kuhama.
Kuna wakati Pep Guardiola alimtaka Van Djik na John Evans. Jana
kumedhihirisha kwanini Pep Guardiola anahitaji beki wa kati.
Manchester City kabla ya mechi ya jana ndiyo ilikuwa timu ambayo
imefungwa goli chache, hii kwa tafasri ya haraka haraka ni kwamba
Manchester City walikuwa na safu imara ya ulinzi. Kitu ambacho
kiuhalisia siyo kweli kwa sababu Manchester City hujilinda kwa
kumiliki mpira kwa muda wote.
Jana mabeki wake wa kati walikuwa siyo wepesi kufanya maamuzi, mfano
goli la Roberto Firmino, John Stones alichelewa kufanya maamuzi
kuuondoa ule mpira.
Pia makosa mengi binafsi yalionekana kati yao wawili ( Otamendi na John Stones).
Ukiachana na mabeki wa kati, Manchester City hawana mtu sahihi wa
kukaa eneo la Mendy. Danilo alisajiliwa kwa ajili ya kubadilishana na
Mendy, lakini jana alipoingia kuchukua nafasi ya Fabian Delph hakuwa
na uwezo mzuri kipindi timu ilipokuwa inakaba na kipindi timu
ilipokuwa inashambulia.
Oxlaide Chamberlaine kumwanzisha eneo la katikati la uwanja kushoto
lilikuwa na msaada mkubwa kwa Liverpool kwa sababu Liverpool ilikuwa
inaanza kushambulia kwa kasi kuanzia eneo la katikati uwanja.
Hali hii ilikuwa inawapa nafasi Liverpool kuwa na watu wanne wenye
kasi kule mbele (Mohamed Salah, Roberto Firmino, Saido Mane na
Oxlaide Chamberlain aliyekuwa anatokea katikati kuja mbele).
Wote walikuwa wanakabia juu, hali iliyowafanya Manchester City kufanya
makosa binafsi.
Kila walipokuwa wanakabia juu kwa kasi walikuwa wanafanikiwa kupata
mipira na kuanzisha mashambulizi kwa kasi.
Liverpool walijua Manchester City huanza kutengeneza mashambulizi yao
nyuma, ambapo mabeki hushuka mpaka katikati ya uwanja ili kuisukuma
timu iwe mbele na mpinzani awe nyuma.
Hivyo Liverpool walichokifanya ni wao kuanzia kukabia juu ili kuwafanya
mabeki wa Manchester City wafanye makosa binafsi.
Ukiangalia magoli ya Firmino, Sane na Salah. Yalianza wakati ambao
Manchester City wakiwa wanaanza kutengeneza mashambulizi nyuma, hivo
Liverpool kufanikiwa kukawakabia juu na kuanzisha mashambulizi kwa
kasi kabla safu ya ulinzi ya Liverpool haijajipanga vizuri na
kufanikiwa kufunga magoli.