Sasa Declan Rice amekuwa lulu barani Ulaya. Anacheza timu ambayo imetoka kutwaa taji la Europa Conference League, hivyo tayari anayo medali mkononi mwake…
USAJILI wa Declan Rice umekuwa kitendawili kizito. Timu mbalimbali za EPL zimatamani kuwa na kiungo mkabaji huyu ambaye ndiye injini ya timu ya West Ham United. Kocha wake David Moyes haambiliki.
Makocha wapinzani nao hawaambiliki kuhusu kiungo huyu. Hata timu kama Manchester United wene Carlos Casemiro wamehusishwa na usajili wake. Manchester City wenye viungo wawili wakabaji Kalvin Philips na Rodrigo nao wanatajwa kuwinda saini ya Declan Rice. Picha za Matukio mbalimbali yaliyokutanisha West Ham United dhidi ya Arsenal katika mfululizo wa mechi za EPL msimu ulioisha zinaonesha kocha Mikel Arteta akikumbatiana na Declan Rice, kukiwa na ishara kana kwamba alikuwa anamweleza jambo fulani. Bila shaka lilikuwa kumkaribisha Arsenal katika msimu ujao. Kila kocha anatamani kumchukua Rice awe sehemu ya kikosi chake.
Umahiri wake ndiyo Sababu hasa inayowapa wazimu makocha kumtaka Nyota huyo, huenda kwa utani ndiyo maana anaitwa ‘mpunga’ au Waswahili wanaweza kusema “ubwabwa” wake uwanjani ni mtamu.
Sasa Declan Rice amekuwa lulu barani Ulaya. Anacheza timu ambayo imetoka kutwaa taji la Europa Conference League, hivyo tayari anayo medali mkononi mwake.
TANZANIASPORTS katika tathmini yake imekuja na swali moja muhimu kwako msomaji wake; ni kwanini Declan Rice anatakiwa na timu nyingi? Au labda kwanini anahitajika sana kwenye vikosi vya vilabu vya Ulaya? Swali hili linaweza kuangaliwa majibu kuanzia katika utangulizi wa makala haya.
Hebu fikiria, kwa mfano kocha wa Man City, Pep Guardiola alimsajili Kalvin Philips kumwongezea nguvu Rodrigo, lakini msimu umeisha huku beki wa Kati John Stones ndiye aliyekuwa akiongeza nguvu eneo la kiungo akiwa mkabaji. Hii Ina maana Kalvin Philips bado hajasimika miguu katika kikosi Cha Pep Guardiola, lakini kwanini amtake tena Declan Rice?
Ifahamike kuwa Declan Rice ni mojawapo ya viungo bora kabisa waliopo sasa barani Ulaya. Ana nguvu, muono wa mbali na zaidi anazijua kazi chafu zote za mchezaji wa kiungo. Nyota huyu anasifika kwa uwezo wake mkubwa wa kuvuruga mipango ya mashambulizi ya timu pinzani. Kwenye kazi ya kuwavuruga wapinzani pale wanapoenda kushambulia lango lake huyu ndiye kikwazo chao na Waswahili wangesema ni kivuruge haswa. Mipango ya mashambulizi hufanywa kwa mbinu au kiufundi ndiye fundi wa kuvuruga.
Declan Rice anao uwezo mkubwa wa kupora mipira kutoka kwa wachezaji wa timu pinzani, lakini anaweza kukokota na kuandaa mpango wa kushambulia lango la adui. Kwamba wakati anapora mipira kutoka kwa wachezaji pinzani huwa anabadilika Sasa anakuwa kama kiungo mshambuliaji. Hizi ni kazi mbili anazoweza kuzifanya kwa wakati mmoja.
Siri nyingine ya kipaji cha Declan Rice ipo kichwani mwake. Anao uwezo mkubwa wa kusoma mbinu za mchezo wa timu pinzani. Anaweza kugundua ufundi uliofichwa na timu pinzani katika mifumo yao ya kujilinda na kushambulia lango la adui. Eneo hili anafanya vizuri sana kazi yake inayowapa uchizi makocha mbalimbali.
Vilevile kwenye suala la kufanya maamuzi wakati mchezo ukiendelea, anaweza kuwaonesha mfano wachezaji wenzake kwa kuhakikisha anakimbizana na wapinzani kila eneo na kuwafanya warudi nyuma zaidi. Anaweza kugundua namna bora ya kufanya uamuzi wa kuwakabili timu pinzani na kuharibu kabisa mipangilio yao ya kiufundi.
Akiwa kiungo mkabaji wa West Ham United anachezeshwa katika mfumo wa 4-2-3-1, na Declan Rice anakuwa kiungo wa pili katika eneo la ukabaji sambamba na Tomas Soucek.
Kwahiyo Declan. Rice anaunda nguzo ya kiungo wa ulinzi kwa pembetatu na kuleta uwiano wa kulinda na kushambulia. Uzuri zaidi yeye anaweza kuhusika katika mashambulizi na wakati wote anakaa kwenye nafasi ya kupokea pasi za kuanzisha mipango ya kushambulia lango la adui.
Lakini, kuvuruga mipango ya adui ndipo mahali alipo na nguvu na ubora zaidi. Kazi yake ni kuzurura katika eneo la kiungo na kudhibiti mipango yote ya adui ya mashambulizi ya kushtukiza, na kubomoa njia wanazotegemea kutumia.
Unapokuwa na kiungo wa namna hii unawezesha timu yako kujihakikishia ushindi na kupunguza ukubwa wa presha ya kujilinda. Kwa namna yoyote ile Mikel Arteta anahitaji kiungo wa pili wa katika ulinzi kusaidiana na Jorginho au Thomas Partey au Mohammed Elneny. Katika mechi yao msimu ulioisha dhidi ya Manchester City, Mikel Arteta alivurugwa eneo la kiungo. Sababu ni moja tu; hakukuwa na kiungo mwenye uwezo wa Declan Rice.
Lakini mabadiliko ya kumwingiza Jorginho yalileta ufanisi kidogo. Hali kadhalika Man City wanataka Declan Rice awe sehemu ya kiungo kwani John Stones analaribia umri wa miaka 30 na hivyo mbadala wake ni muhimu. Kalvin Philips ndiye mchezaji anayecheza na Declan Rice timu ya Taifa na wameunda kiungo Cha hatari na chenye nguvu na kuipa uhai England.
Nao Man United wanajua kuwa Casemiro anahitaji kiungo wa pili wa kusaidiana naye kazi za eneo hilo. Bila shaka nao wanamtazama Declan Rice kama suluhisho la eneo hilo. Ni Sababu hizo Declan Rice amekuwa lulu barani Ulaya.