*Wameishia nafasi ya 17 kwenye Ligi Kuu Uingereza
*Kulikoni wasijiimarishe, ni biashara au huduma zaidi
Rais Jakaya Kikwete alipozuru Uingereza hivi karibuni, wadau wa michezo, hasa wa Tanzania, walikuwa na mengi ya kuongea na kubadilishana mawazo.
Pamoja na mambo mengine, Rais Kikwete alitembelea klabu ya Sunderland ya Uingereza, ambayo katika Ligi Kuu ya England (EPL) msimu uliopita ilinusurika kushuka daraja.
Hali ilikuwa mbaya hivyo kwamba mmiliki ambaye ni Mmarekani, Ellis Short alilazimika kumfukuza kazi kocha Martin O’Neal na kumwajiri mwanasoka nguli lakini mtata wa Italia, Paolo Di Canio kwenye mechi za mwisho mwisho kuokoa jahazi.
Ilikuwa wazame kabisa, na ilikuwa bahati mbaya kwa timu nyingine kuachia ngazi na yenyewe kupona, hasa baada ya Arsenal kuwatandika Wigan katika mechi muhimu kwao na kuwashusha. Wigan walikuwa na uwezo wa kuwapiku Sunderland.
Kwa hiyo ligi ile ilikomalizikia, kama wangesema ishuke timu moja zaidi, Sunderland ndio wangeshuka. Kwa maneno mengine, katika matokeo ya mwisho, walishika nafasi ya 17 miongoni mwa timu 20.
Sasa leo tuna swali; kipi kimewavutia mpaka wakaamua kuwekeza kwenye mpira nchini Tanzania wakati wenyewe wapo hoi bin taabani na wanatakiwa kujinusuru na hali hiyo mbaya?
Hii kwao ni biashara zaidi au ni huduma? Je, ni mapenzi kwa Tanzania na kutaka kuinua soka ya Tanzania na watu wake au ni vipi hasa? Ofisa Mtendaji Mkuu wa Sunderland, Margaret Byrne anasema ushirikiano na Tanzania ni hatua kubwa mbele.
Sunderland ambao hujulikana kwa jina la utani la The Black Cats au ‘Paka Weusi’ wamejenga ushirika na kampuni kubwa ya kimataifa ya kufua umeme ya Symbion Power kwa ajili ya kujenga kituo kikubwa kabisa cha mafunzo ya soka – Academy jijini Dar es Salaam.
JK alipofika hapa, aliongoza ujumbe wa watu waliokwenda Wearside, ambako ilikuwa maalumu kuzindua rasmi mradi huo mpya.
“Kwa kweli ni siku ya aina yake kwa klabu yetu na jiji kwa ujumla. Sisi kuweza kuwa na Mheshimiwa (Rais JK) hapa kututembelea wakati akiwa hapa kuzungumza na wakuu wa nchi tajiri zaidi duniani (G8) kumeonesha jinsi yeye mwenyewe na mawaziri wake wanavyojituma. Kwetu ni furaha kubwa,” akasema Byrne katika tukio lililovuta vyombo vya habari vya kimataifa.
Mipango ya awali ya Academy hiyo ilielezwa katika hafla maalumu iliyohudhuriwa pia na Short, ambaye ni mwenyekiti wa Sunderland, ambapo mradi unaelezwa kwamba utawafikishia miundombinu na vifaa vya soka maelfu ya watoto na vijana wa Dar es Salaam.
Ipo mipango pia ya kuendeleza mfumo wa soka ya vijana, katika kung’amua vipaji na kuvikuza, ili hatimaye Tanzania inyanyuke na kutamba kwenye soka la kimataifa.
Sunderland itajihusisha kwa kiasi kikubwa huko, katika kutoa wataalamu wa ujenzi na kusaidia kwenye mafunzo. Watashirikiana na Symbion Power kujenga kituo hicho cha michezo cha muundo wa kijamii, kitakachoruhusu watoto wengi kuingia, kujiunga, kucheza na kufurahia soka.
Baada ya watoto na vijana kufika na kucheza kwa wingi, hatua ya pili itakuwa kuanza ujenzi wa vituo kwa ajili ya ukuzai vipaji, kwa kutoa mafunzo ya kisasa, tayari kwa wao kujiunga katika timu za taifa.
Sunderland ambao wanajiandaa kwa msimu mpya na mgumu wa ligi unaoanza Agosti, wanasema watatumia mifano ya kituo chao – Academy of Light na pia uzoefu waliopata kutoka kwenye miradi mingine kuinyanyua Tanzania na watu wake kisoka.
Hatua ya sasa ya uwekezaji nchini Tanzania ni ya pili kwa Sunderland kuonesha kwa Afrika, kwani kwa sasa wanaendelea na udhamini wa ‘Invest In Africa’, wakivaa fulana zilizoandikwa hivyo, wakielekea kulipigia chapuo bara la Afrika katika uwekezaji.
Ushirikiano mkubwa Sunderland ambao wamekuwa nao ni wa Bidvest, kampuni kubwa la Afrika Kusini, Bidvest Wits Football Club na pia Asante Kotoko wa Ghana.
Je, Sunderland kumaliza ligi mkiani na kujielekeza zaidi katika ukuzaji soka na uwekezaji Afrika ni mambo yaliyotokea kwa bahati tu au ni mkakati wa Mmarekani Short na Bodi ya Wakurugenzi?
Je, wataweza kwenda sambamba kimaendeleo, wakihakikisha wanafanya vizuri kwenye ligi, na wakati huo huo wakijenga kituo cha kweli cha kisasa cha michezo, kuingiza watoto, kung’amua vipaji na kuvikuza kwenye academy ya kisasa? Ni mpango mzuri kinadharia, lakini mgumu kutekelezwa na klabu ya aina hiyo, japokuwa tunautakia heri.