WAKATI ligi kuu Tanzania Bara ikiendelea kutimua vumbi, Timu ya soka ya Azam ilionja adha ya kuzomewa na watazamaji ambapo baadhi ya watu wamedai Wakazi wa Wilaya ya Temeke hawaitaki timu hiyo.
Azam yenye umri usiozidi miaka 10 imekuwa timu ya kwanza kujenga Uwanja wake wa Kisasa eneo la Chamazi wilayani Temeke.
Lakini pia kujengwa kwa uwanja huo kumeiongezea sifa Wilaya ya Temeke ya kuwa na viwanja vitatu maarufu kwa mchezo wa soka.
Kiwanja cha kwanza kujengwa wilayani humo ni Uwanja wa Uhuru ambao unatumika zaidi kwa sherehe za Kitaifa kwani ndipo mahali palipopokewa Bendera ya Tanganyika ilipopata Uhuru mwaka 1961.
Hali kadhalika wilaya hiyo ina uwanja wa Taifa ambao ulijengwa wakati wa Serikali ya awamu ya tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa iliyomalizika mwaka 2005 kwa msaada wa watu wa China.
Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya maisha ya Dar es Salaam tayari wanasisitiza kwamba Temeke ni maarufu kwa viwanja vya soka, sawa na ilivyo Wilaya ya Kinondoni ambayo ni maarufu kwa kuwa na baa nyingi wakati Wilaya ya Ilala ikiwa maarufu kwa kuwa na kumbi nyingi za Starehe na ofisi za umma.
Pamoja na Temeke kuwa na viwanja vingi, Wilaya hiyo haikubahatika kuwa na timu yoyote yenye makao yake humo licha ya hivi karibuni kuwapo kwa timu ya Lyon inayoshiriki ligi kuu Tanzania ambayo inaelezwa kuwa ya asili Temeke, lakini makao yake halisi hayajulikani.
Kwa hali hiyo Timu ya Azam ambayo watu wengi wanaamini kwamba imedhamiria kuishi Temeke. Simba na Yanga zote zipo Ilala wakati Kinondoni inajikongoja na timu y Villa.
Lakini wakati Azam ndio kwanza imeanza kuutumia uwanja wake msimu huu, tayari ilianza kwa kuzomewa sana na wapenzi wa soka.
“Kiongozi wa klabu hiyo aliwahi kukiri kwamba timu yake inazomewa kutokana na ugeni katika eneo hilo, lakini hivi karibuni pia alifafanua kwamba wapenzi wa soka wameanza kuipenda timu hiyo inapocheza nyumbani.
Watafiti wa masuala ya upenzi wa michezo wanasema , wapenzi wengi wa soka wako Wilaya za Kinondoni na Ilala ambazo hazina uwanja hata mmoja.
Lakini pia wanasema karibu watu wengi wa wilaya hizo mbili ni mashabiki wa asili wa timu za Simba na Yanga kiasi kwamba hata wakienda Uwanja wa Chamazi unaomilikiwa na Azam wanaendeleza kuiponda wakihofia kwamba timu hiyo inaweza kuziua timu zao kimaendeleo. Wengine wanaohifa kuona timu changa ikiwa na uwanja mzuri.
Wapo wadadisi wengine wanaosisitiza kwamba wanaoiponda Azam kwenye uwanja wake siyo wakazi wa Temeke, kwani kwa ujumla wakazi wengi wa wilaya hiyo wanatoka mikoa ya Lindi na Mtwara ambako kipato chao ni shida hata kuingia kwenye mchezo ni shida tofauti na wilaya zingine mbili ambazo zinapokea watu wa kutoka mikoa karibu yote iliyobaki na hivyo kuzifanya kuwa na watu mchanganyiko zaidi.
Hoja ni je Azam itakosa wapenzi wa soka ikionyesha kandanda safi? Swali hili na mengine mengi yanatarajiwa kujibiwa ndani ya miaka michache ijayo.
mwisho.
info@tanzaniasports.com