Menu
in , , ,

Kutoka Manchester hadi Mwanitesa United

Tanzania Sports

KIPIGO cha mabao 4-3 walichokipata Manchester United kutoka kwa mabingwa wa zamani wa Ulaya Bayern Munich kimeendeleza gumzo huku golikipa namba moja Andre Onana akikiri kuwa makosa yake ndiyo kiini cha kufungwa mchezo huo wa hatua ya makundi katika Ligi ya Mabingwa Ulaya. Mabingwa hao wa zamani wa EPL na Ulaya hawajawahi kuwa na mafanikio tangu kuondoka kwa Sir Alex Ferguson. Katika mazingira ya sasa Manchester United imekuwa klabu ambayo haiogopwi, huku matukio ya nje ya uwanja nayo yakishimiri.

TANZANIASPORTS katika uchunguzi wake wa kikosi hicho imebaini matatizo mengi yanayoikumba klabu hiyo. Kuanzia benchi la ufundi,wachezaji ndani ya uwanja,utamaduni wa klabu klabu yenyewe na mfumo mzima wa uongozi. Uchambuzi wetu uliofanywa kutokana na mchezo uliochezwa Allianz Arena unagundua matatizo yanayoochangiwa na kocha mwenyewe na mengine yanatokana na wachezaji wa timu hiyo. Makala haya yanaorodhesha na kuchambuzi kwa makini.

Jukumu la Marcus Rashford ni lipi?

Alichezeshwa upande wa kushoto ili kuongeza nguvu ya mashambulizi. Mchezo kwake ulianza vizuri, lakini ndani ya dakika 20 Rashford hakuonekana kuwa na amdhara yoyote. Eneo la kulia la Bayern Munich halikuona madhara yoyote. Kadiri mchezo uliovyokuwa unaendelea, uchunguzi unaonesha Rashford hakuwa tishio, hakupiga mashuti langoni mwa Bayern, hakuwa na majaribio ya kufunga mabao, hakuwa mbunifu, hakusaidia ulinzi kama anavyotakiwa kulinda upande wa kushoto wa Manchester United alikopangwa Sergio Reguilon. Mhispania Reguilon alikuwa moto wa kuotea mbali, lakini hakuweza kuonana (gonga safi) vizuri na Rashford. Kati ya mambo ambayo mashabiki wa Man United wanadanganywa ni kuaminishwa kuwa Marcus Rashford ni mshambuliaji thabiti na mwenye kuibeba klabu yao. Licha ya kuwa mchezaji aliyehitimu kwenye akademi yao, bado si mchezaji wa kuamua matokeo. 

Kwenye ulinzi alishindwa hata na Harry Kane ambaye ambaye baadhi ya matukio alionekana eneo la ulinzi wa kati kusaidia ulinzi pale timu yake inapozuia mipia ya adhabu ndogo. Ukiangalia namna Rashford alivyokwenda eneo la kiungo badala ya kusaidia na kuziba mianya ya kupenyezwa pasi, akawa anatembea kama ‘mkurugenzi anaingia ofisini’ huku akishuhudia Jamal Musiala akiwasambaratisha mabeki wake wa kati. Matukio mengi ya mchezaji huyu yanasikitisha. 

Wakati mwingine unajiuliza, Ten Hag alitaka nini kwa mchezaji kama Marcus Rashford ambaye hakuweza kumpa kile kilichotarajiwa. Hata kipindi cha pili alipomhamishia winga wa kulia ili kumpa nafasi Garnacho kucheza winga wa kushoto bado hali haikuwa nzuri. Kuna wakati alikuwa anatembea tembea tu, huku akiwa amechoka mno. Kwa jinsi Manchester Uniterd ilivyoundwa na tamaduni zake hatua ya mchezaji kutembea tembea kama mzururaji ni pigo.

BEKI WA KULIA

Dalot ni mchezaji wa kutegemea kwenye mechi kubwa kuliko Wan Bissaka? Uamuzi wa kocha Eric Ten Hag ulipotea hapa, Dalot hakuwa mchezaji aliyestahili kupangwa kwenye mchezo huo kwa sababu hakuwa mahiri kiulinzi wala kushambulia. Badala yake aligeuzwa asusa na Jamal Musiala au Leroy Sane. Wakati timu inaanza mchezo Dalot alionekana wazi kuwa mchezaji ambaye asingeweza kudhibiti mshambulizi ya Bayern Munich. Je uamuzi wa kupanga nafasi hiyo ulikuwa sahihi au kamari ya mwalimu ilitokota?

VIUNGO WAKABAJI

Ikiwa Eric Ten Hag alitaka timu yake ikae kuanzia eneo la 18 la adui na alipomwingiza McTominay ilidhihirika wazi angeweza kuipanga timu yake mapema kuliko kumwingiza Christian Erickssen. Vilevile mwalimu alikuwa na uwezo wa kuchangua viungo wakabaji wawili ambao wangemsaidia Erickssen kushambulia zaidi. Matokeo yake wakati Manchester United ilipokuwa inaanda mashambulizi, ilimlazimu Erickssen kurudi nyuma zaidi hadi eneo la beki wa kati kupokea mipira na kuanza kuiandaa timu ishambulie namna gani. 

Ili kuifanya kazi ya Erickssen iwe nyepesi ilitakiwa viungo wakabaji wawe wawili. Carlos Casemiro umahiri wake unachangiwa pia na ushirikiano na wachezaji wengine. Namna alivyokuwa akicheza Real Madrid ilikuwa ‘double pivot’ akiwa na Toni Kroos na Luka Modric. Lakini kwenye mechi nyingi Casemiro amekuwa akipangwa peke yake eneo la kiungo na kuifanya kazi yake iwe ngumu zaidi.

VIPANDE VYA MABEKI WA KATI

Kama kuna jambo limeshangaza ni namna safu ya ulinzi inavyokatika. Jamal Musiala aliwafanya walinzi wa Man United waonekane kama hawana uwezo wowote, kwa sababu makosa yalishafanyika kwenye upangaji wa eneo la kiungo. Walinzi wa kati Lendof na Martinez walionekana kuhitaji mtu wa kuwachunga na kuhakikisha wanafanya kazi kwa ufanisi. 

Mtu wa kuwachunga mabeki wa kati inakumbusha namna Carles Puyol alivyokuwa akicheza na Grerrad Pique. Kwenye moja ya simulizi zake Pique anasema, “kuna wakati Puyol alikuwa ananiita jina langu kama anataka kuniambia kitu, lakini kila nikiitika anasema ‘nilitaka kujua kama uko makini,”. Kazi ya Puyol ilihitajika Man United, yaani mchezaji ambaye anaweza kuwalinda mabeki wa kati. Yaani beki mwenye uwezo wa kuongoza jahazi mbali ya mfumo unaotaka kufanyika. Eric Ten Hag ana kazi nzito wa kuisuka safu ya ulinzi ili iwe na kombinenga thabiti.

GOLIKIPA MZEMBE

Pengine makosa ya Andre Onana katika bao la kwanza la Bayern Munich linaturudisha kwa kipa wao wa zamani Mark Bosnich. Huyu mwamba alikuwa na makosa mengi mno kiasi kwamba Man United ikawa inahaha kusaka makipa sokoni enzi za Sir Alex Fegurson. Lakini Andre Onana golikipa wa kisasa alifanya kazi la kuzembea kuzuia shuti jepesi lililotinga wavuni. Ingawa goli hilo linatajwa kuchangia kuharibu nguvu ya timu lakini Manchester United ina matatizo mengi mno kama timu. Hawana umakini, uharaka katika mashambulizi, ari, ushirikiano wa kitimu.

BEKI WA KUSHOTO

Sergio Reguilon anacheza kwa mkopo Man United lakini aliwaonesha mashabiki nini alichofundishwa alipokuwa Real Madrid kabla ya kununuliwa na Tottenham Hotspurs. Reguilon ni beki ambaye anakupa vitu viwili, analinda vizuri na anashambulia kwa kasi. Alichokikosa ni mshirika wa kushambulia katika upande wake wa kushoto ambako alipangwa Marcus Rashford. Eric Ten Hag atakuwa amesoma vema uchezaji wa kijana huyu ili awapunguzie mateso mashabiki wao ambao sasa wanaiona Manchester Unitd kama Mwanitesa United.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version