LIGI Daraja la Kwanza Tanzania Bara ilianza kutimua vumbi wiki iliyopita katika viwanja mbalimbali nchini ikishirikisha timu 16.
Ligi hiyo ambayo Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, iliifuta na kuanzisha Ligi ya Ttaifa ambayo ilikuwa ikianzia katika ngazi ya wilaya hadi taifa kwa timu tatu zilizofanya vizuri zaidi zilipanda Ligi Kuu.
Lakini baada ya kupotea kwa takriban miaka mitatu, TFF imeirejesha Ligi Daraja la Kwanza lakini Ligi ya Taifa ikiendelea kuchezwa kama kawaida ambayo pia itapandisha timu zitakazocheza Ligi Daraja la Kwanza.
Mbali na Ligi Daraja la Kwanza, lakini pia Ligi ya Wanawake imepangwa kuanza baadaye Novemba ikishirikisha timu kutoka maeneo tofauti ya nchi yetu.
Awali Ligi ya Wanawake ilikuwa ikichezwa katika wilaya ya Kinondoni pekee ikisimamiwa kikamilifu na Chama cha soka Wilayani humo, KIFA, na matunda yake yameonekana kwa kutengeneza timu ya taifa ya wanawake, Twiga Stars iliyoshiriki mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa wanawake.
Pamoja na Tanzania kuwa nyuma katika soka ya wanawake, lakini dada hao waliweza kuwafungisha virago wenzao wa Eritrea na kuvuka hatua ya pili kabla ya kutolewa na Cameroon.
Kimsingi, tukiangalia Ligi Daraja la Kwanza na ile ya wanawake kutokana na kuonekana kusahaulika na wadau mbalimbali wa mchezo wa mpira wa miguu na hasa wadhamini, kuna kila sababu kwa Shirikisho la Soka Tanzania, TFF lina kila sababu ya kusaka wadhamini kwa ajili ya kusadi kupunguza makali ya hili.
Timu nyingi za Daraja la Kwanza pamoja na kuanza mechi zao, lakini hazina mdhamini, ambaye kwa namna moja ama nyingine husadia kuongeza changamoto na ushindani miongoni mwa timu kutokana na zawadi ambazo zingetolewa kwa wachezaji, ama timu itakayofanya vizuri pamoja na kupunguza makali ya gharama za usafiri na uendeshaji.
Ligi inapokuwa na udhamini wa kueleweka huongeza ushindani kutokana na kwamba kila timu kutaka kupata moja kati ya zawadi zitakazotolewa, ama kwa wachezaji kushindania zawadi ya mfungaji bora, kipa bora, au mchezaji mwenye nidhamu.
Inapotokea ligi kukosa udhamini ina maana hata ushindani pia unakuwa ni mdogo kwa sababu wachezaji wanafahamu kuwa hata akijituma namna gani hakuna anachokipata.
Kwa tathmini ndogo, ukiangalia timu zinazoshiriki Ligi Daraja la Kwanza, utagundua kuwa nyingi ni za wananchi wa kawaida ambao hawana kipato kikubwa kwa hiyo inakuwa vigumu kumudu uendeshaji wa timu.
Kama tunavyofahamu, timu inapokuwa ikishiriki mashindano inakuwa na mahitaji mengi ikiwemo vifaa vya mazoezi na mechi, posho, fedha za nauli kutoka sehemu moja kwenda nyingine.
Kabla ya ligi kuanza wadhamini hutoa vifaa pamoja na fedha za nauli kwa timu ili ziweze kushiriki vema katika mashindano na ndio maana wiki chache zilizopita tulisikia viongozi timu zinazoshiriki Ligi Kuu wakilalamikia ugumu wanaopata kusafirisha timu kutokana na kuchelewa kupata fedha za nauli kutoka kwa wadhamini, kampuni ya simu za mikononi ya Vodacom.
Zipo timu zinazomilikiwa na majeshi ya ulinzi na Usalama na baadhi zina wadhamini ambazo angalau ndio zina uwezo wa kujumudu hata kama ligi haina udhamini kutokana na kupata kila kitu.
Ipo timu kama Polisi Tabora ya Jeshi la Polisi, Ruvu Shooting ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) lakini pia ipo timu ya Mwanza United yenye udhamini wa kampuni ya bia ya Serengeti (SBL) na timu ya Balimi ambayo inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania, TBL.
Ukiondoa timu hizo, nyingine zilizobaki kama Ashanti, Pan Africa za jijini Dar es Salaam, Kijiweni ya Mbeya, Majimaji ya Songea, Mbagala Market na nyinginezo hazina uwezo wa kumudu gharama kubwa za uendeshaji wa timu tofauti na hizo za majeshi ama zenye uhakika wa udhamini.
Kwa upande mwingine, katika ligi ya wanawake hadithi ni ile ile hakuna mipango thabiti ya kuleta changamoto kwa kuwaleta wadhamini kwa ajili ya kupunguza makali ya maisha ya soka, sasa TFF ambayo ndiyo baba wa soka, inatakiwa kusimama hapo.
TFF kufanya kazi ya kuzikopesha timu fedha halafu kuja kuzidai ni mzigo, kinachotakiwa ni kuwatafutia wadhamini wa uhakika.
Tukiwaangalia wachezaji hawa tunaowaona wakichezea timu ya taifa kwa mafanikio wametokea katika ligi za chini ambazo hazina budi kuboreshwa.
Lakini kinachoonekana hapa ni kwamba Watanzania wengi tunapenda vitu vilivyo tayari, bila kuangalia msingi. Nyumba imara inatokana na msingi imara.
Ligi imeanza hivyo ni wakati mwafaka kwa TFF, si kuangalia Ligi Kuu pekee, bali watafute wadhamini wengine katika madaraja ya chini ambayo kama kukiwa na mdhamini wa uhakika, hata msisimko utakuwepo pamoja na timu za wanawake.
Ukweli ni kwamba, zinahitajika nguvu zitakazosaidia timu kufanya vizuri pamoja na kuibua ushindani wa nguvu kwa madaraja ya chini kwa wanawake na wanaume.