Mashindano hayo ya 34 na Makubwa zaidi katika ardhi ya Afrika michezo kadhaa imepigwa na tayari wana Fainali wawili wameshapatikana kati ya wenyeji Ivory Coast pamoja na Nigeria. Safari haikuwa rahisi kwa timu hizi kufika fainali hiyo ya AFCON ambayo yanafanyika nchini Ivory Coast.
Michuano hii ilianza rasmi kuanzia tarehe 13 Januari kwa kuwakutanisha wenyeji Ivory Coast na Guinea-Bissau ambapo Ivory Coast walifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 huku mabao hayo yakifungwa na mchezaji Seko Mohamed Fofana na Jean-Philippe Krasso.
TANZANIA AFCON
Katika timu shiriki ambazo zilikuwemo kwenye hiyo michuano nayo timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ na ilikuwa miongoni mwao. Taifa Stars ilianza kutupa karata yake Januari 17, 2024 dhidi ya Morocco huku ikichezea kichapo cha mabao 3-0, katika mchezo ule tulishudia mchezaji Novatus Dismas akizawadiwa kadi nyekundu kipindi cha pili na kuipa mzigo mzito Stars ambayo ilionyesha kuelemewa kwa kiasi kikubwa. Kundi ‘F’ lilikuwa na timu kama Morocco, DR Congo, Zambia na Tanzania, ambao mpaka michezo ya makundi inakamilika iliambulia alama mbili pekee na kushindwa kushinda hata mchezo mmoja.
SAFARI YA NIGERIA
Timu ya Taifa ya Nigeria ambao ni wana fainali waliianza safari yao kwa mchezo wao kwanza dhidi ya timu ya Taifa ya Guinea kwa ushindi wa mabao 2-0, kisha mchezo uliofuata ambao walikwenda sare ya bao 1-1 na Equatorial Guinea, Nigeria iliendelea kujitengenezea mazingira mazuri kwani katika kufanya vizuri Katika michezo yake ya makundi ilipata ushindi dhidi ya wenyeji wa michuano hiyo ya AFCON, Ivory Coast kwa bao 1-0 na kuanza kuzungumzwa kila Kona na wadau wa michezo kwamba wanaweza kuondoka na Ubingwa huo. Kwa kumalizia ule mchezo wake wa mwisho na Guinea-Bissau wakashinda tena kwa bao 1-0 na kwenda hatua ya 16 bora.
SAFARI YA IVORY COAST
Timu ya Taifa ya Ivory Coast imefanikiwa kuingia fainali ya AFCON na kuibua sherehe kubwa ambayo unaweza kusema ni kama mgonjwa aliyetoka ICU yaani ilikuwa taabani, hali ilikuaje? Katika hali isiyo ya kawaida kila mmoja aliamini timu ya Ivory Coast ndiyo kama hakuna kitu tena pale ilipopoteza mchezo wake wa mwisho kwenye makundi dhidi ya Equatorial Guinea, kichapo kizito cha mabao 4-0 ambacho unaweza ukakiita kipigo cha aibu kutoka kwa wababe hao. Hata hivyo unaweza kusema mchezo wa mpira umejawa na bahati kubwa kwani baada ya kutoka zile nafasi za Best loser (yaani nafasi ya upendeleo) ikiwapa nafasi zaidi wenyeji Ivory Coast na kuwanyima nafasi kama hivyo timu ya Taifa Tanzania, Taifa Stars, Zambia na Msumbiji ambazo zilikuwa zikiitafuta kuwa na alama nne ambazo Ivory Coast pekee ndiye aliyekuwa na sifa hiyo. Mechi ya 16 bora dhidi ya Senegal, Ivory Coast ikifanikiwa kuondoa Senegal kwa penati 5-4 baada ya zile dakika 90′ kumalizika kwa sare ya 1-1. Mchezo wa robo fainali wakaitandika Mali mabao 2-1 Kisha kutinga Nusu Fainali ambao waliiondosha DR Congo kwa bao 1-0, na sasa Fainali ni dhidi ya Nigeria ambayo inasubiriwa kwa hamu kubwa na wana michezo wengi ambayo inahitimishwa Februari 11, 2024 huko Abidjan.
NBC NDANI YA AFCON
Tunaweza kusema hivyo Ligi Kuu NBC PL, ni kama imejitangaza zaidi Katika michuano hiyo ya AFCON kule nchini Ivory Coast kwa kushuhudia baadhi ya nyota wanaocheza kwenye Ligi hiyo kuzitumikia timu zao za Taifa. Mchezaji kama Henock Inonga Baka anayekipiga Katika Klabu ya Simba SC, naye ni miongoni mwa wachezaji walioitumikia vyema timu ya Taifa ya DR Congo kwa kuzuia vyema huku kuwavitia watu wengi kama ilivyokuwa kwenye mchezo wa Nusu Fainali kati ya Ivory Coast na DR Congo, mkongwe Didier Drogba alishindwa kuizuia pindi kija huyo alivyokuwa akitimiza majukumu yake vyema. Nyota mwingine ni Stephanie Aziz Ki mchezaji wa timu ya Taifa ya Burkina Faso ‘Burkina Be’ anayekipiga kuna klabu ya Yanga SC, Clatous Chama, timu ya Taifa ya Zambia na Klabu ya Simba SC, Kennedy Musonda, timu ya Taifa ya Zambia klabu ya Yanga SC, Golikipa Djigui Diarra timu ya Taifa Mali huku akiidakia Klabu ya Yanga SC. Kazi kubwa imefanywa kwa vilabu vya Tanzania kwa kufanya usajili mzuri ambao umeleta tija kwenye soka la Tanzania.
HAIKUWA BAHATI
Timu ya Taifa ya Afrika Kusini imeondolea kwenye michuano hiyo hatua za mwisho ya nusu fainali dhidi ya Nigeria kwa changamoto ya mikwaju ya penati ambayo iliwauma watu wengi. Hapa stori ilikuwa tofauti kidogo, kila kila mmoja alikuwa amewapa nafasi kubwa Afrika Kusini kulingana na ubora wa mlinda mlango wake, Ronwen Williams ambaye kwa kiasi kikubwa alionyesha umahiri wake kwa kucheza mikwaju ya penati katika mchezo wa robo fainali siku ya Jumamosi dhidi ya Cape Verde. Williams aliondoa mikwaju ya wanasoka wa Cape verde wakiwemo Bebe, Willy Semedo, Laros Duarte na Patrick Andrade.Williams, mwenye umri wa miaka 32, anayeichezea Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, alikataa kujizolea sifa zote licha ya ushujaa wake na badala yake, kutoa shukrani kwa wakufunzi na watalaam wa kiufundi wa timu ya Afrika Kusini.