KILA kona ya nchi yetu kuna mjadala unaendelea kuhusiana na wachezaji wa klabu ya Singida Black Stars ambao wamepewa uraia wa Tanzania kutoka kwenye Mataifa yao ya Ivory Coast, Ghana na Guinea. Kwa mujibu wa taarifa ya Idara ya Uhamiaji pamoja na mambo mengine ilieleza kuwa wachezaji watatu wa timu ya Singida Black Stars wamepewa uraia wa Tanzania kwa Tajnisi.
Je mamlaka ya Uhamiaji ilisema nini?
“Idara ya Uhamiaji inapenda kutoa taarifa ya ufafanuzi zilizochapishwa na kujadiliwa kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kuhusu kupatiwa uraia wachezaji watatu; Emmanuel Kwame Keyekeh kutoka Ghana, Josephat Arthur Bada kutoka Ivory Coast, na Muhamed Damaro Camara kutoka Guinea. Wachezaji hao waliomba na kupewa uraia kwa mujibu wa vifungu vya 9 na 23 vya sheria ya Uraia ya Tanzania, Sura ya 357,”.
Taarifa hiyo iliibua mjadala zaidi na baadhi ya wadau wa michezo kuhoji utaratibu uliotumika. Pia baadhi ya wachambuzi mbalimbali waliibua madai kuwa wachezaji hao walibadilisha uraia wakiwa na malengo ya kuchezea Timu ya Taifa ya Tanzania maarufu kama Taita Stars kwenye mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) ambayo yatafanyika mwaka huu katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda. Pia wanatajwa kulenga mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) ambayo yatafanyika katika Mataifa ya Uganda, Kenya na Tanzania. Hata hivyo tetesi hizi hazithibitishwa na upande wa wachezaji wenyewe wala klabu wanayotumikia.
Je uraia wa Tajnisi ni nini?
Kwa mujibu wa sheria za Tanzania, huo ni uraia wa kuandikishwa kwa wale wageni wanaoomba kuwa raia na kisha kukidhi vigezo vyote vya kisheria; wanapatiwa cheti cha uthibitisho kwamba wao ni raia wa Tanzania. Mtu mwenye uraia Tajnisi; watoto wake watakaozaliwa baada ya yeye kusajiliwa moja kwa moja wanakuwa raia wa Tanzania, ila kama wachezaji hao wanao watoto watatakiwa kuomba kuwa raia. Kwa msingi huo wanakuwa raia kama wengine licha ya kuwa wachezaji wa kandanda.
Je uraia huo ni sifa ya kuitwa Taifa Stars?
Sifa ya kutumikia Taifa Stars ni lazima uwe raia wa Tanzania. Kwahiyo wachezaji hawa wamekidhi vigezo vya kuwa raia huku wakikabiliwa na jukumu lingine ya kuonesha uwezo uwanjani. Ili mchezaji aitwe Taifa Stars ni lazima awe na uwezo mkubwa. Wachezaji waliopo Tanzania ni wengi na ambao wamejaliw avipaji vizuri. Lakini si wachezaji wote wanaweza kuwa kuwa muhimu katika kikosi hicho. Kocha wa timu yoyote anaangalia mahitaji yake kwa ajili ya kupata matokeo mazuri. Kocha anataka kuwa na wachezaji ambao wanaendana na mfumo anaotaka kutumia ili kuipa mafanikio klabu.
Wapo wachezaji ambao wanatamba katika klabu mbalimbali lakini hawana nafasi kwenye timu za taifa. Sababu za kukosa nafasi hiyo ni mifumo ya mwalimu au uwezo wao haukidhi vigezo vya kuitwa timu ya taifa. Kimsingi wachezaji hao kupewa uraia ni jambo moja, lakini kuitwa timu ya Taifa ni kitu kingine. Kibu Dennis alipewa uraia wa Tanzania kwa vile ameishi katika kambi za wakimbizi nchini pamoja na kipaji chake murua katika mchezo wa soka.
Katika ngazi ya klabu Kibu Dennis amekuwa mchezaji muhimu na ameotoa mchango mkubwa katika mashindano mbalimbali. Lakini kwenye timu ya taifa pia amekuwa akikaa benchi au kuanza kikosi cha kwanza kulingana na matakwa ya mwalimu. Ukiangalia wachezaji waliopewa uraia, wana uwezo mzuri wa kucheza kandanda hivyo kama watakidhi vigezo vya benchi la ufundi la Taifa Stars wanaweza kuitwa. Sifa kubwa ya kuitw atimu ya taifa lazima ukidhi kigezo hiki cha uwezo mkubwa wa kucheza, ushindani, na maarifa ya mchezaji katika kuleta ufanisi kwenye timu.
Je uraia wao ni jambo la ajabu?
Kimsingi katika dunia ya leo ipo vita kubwa kwenye sekta ya michezo. Wachezaji wenye vipaji wanawindwa katika mataifa mbalimbali. Mfano timu ya Taifa ya Ujerumani imekuwa na vipaji vingi vya watoto wa wahamiaji ambao walipewa uraia. Inatukumbusha pia vita ya kummiliki Joseph Desire Job kati ya Cameroona Ufaransa, kisha Diego Costa kati ya Hispania na Brazil. Pia timu za mataifa mbalimbali zimekuwa na wachezaji wanaochukua uraia na kupewa nafasi ya kuwakilisha na kuonesha vipaji vyao. Manufaa ya vipaji hivyo yanakwenda kwa nchi wanayowakilisha. Wabrazil wapo katika nchi mbalimbali na baadhi wametumikia timu za taifa za kigeni kwa sababu walipewa uraia huko. Utaona hili si jambo la ajabu lakini linakwenda sambamba na kigezo cha mchezaji kuwa na uwezo mkubwa katika kandanda. Mchezaji ambaye anaitwa timu ya Taifa ni yule ambaye anaweza kuitumikia vizuri na kuleta mchango. Kwahiyo kuitwa inaweza kuwa hatua moja, lakini kuonesha cheche zake ni hatua nyingine.