Mabao mawili ya Meshack Elia na lingine la Jonathan Bolingi yaliyoipa ushindi wa 3-0 timu ya Taifa ya Jamhuri ya Kidemokraisa ya Kongo dhidi ya Mali yameifanya Kongo kutwaa ubingwa wa CHAN hapo jana.
Mabingwa hao wanaonolewa na mwalimu Florent Ibenge wamekuwa nchi ya kwanza kutwaa ubingwa wa michuano hiyo mara mbili wakiwa wametwaa ile ya mwaka 2009 kule nchini Ivory Coast.
Mchezo huo wa fainali ya CHAN – Michuano inayoshirikisha wachezaji wanaocheza ligi za nyumbani pekee, ulifanyika katika dimba la Amohoro huko Kigali nchini Rwanda.
Licha ya DR Congo kupokea sapoti kubwa ya mashabiki kwenye dimba hilo, ni Mali waliokuwa na ari zaidi kwenye dakika za mwanzo za mchezo wakifanya mashambulizi kadhaa ya hatari kupitia kwa mchezaji wao Mamadou Coulibaly aliyefika langoni mara kadhaa kwa mashuti makali.
Hata hivyo ni DR Congo walioweza kufungua kitabu cha mabao mnamo dakika ya 29 kupitia kwa mshambuliaji wao Meshack Elia aliyepiga shuti la mbali lililomuacha golikipa Djigui Diarra akijituma kulizuia bila mafanikio.
Bao hilo la Elia lilidumu hadi kipindi cha mapumziko na DR Congo walirejea wakiwa na makali zaidi kwenye kipindi cha pili kiasi cha kuwanyima Mali nafasi ya kutengeneza nafasi yoyote ya wazi ya kuweza kusawazisha bao hilo.
Mnamo dakika ya 61 mlinda mlango Djigui Diarra aliadhibiwa tena na Elia, safari hii akimtoka kwa ustadi na kupasia mpira kwa urahisi ndani ya wavu.
Lassan Samaka alikosa nafasi ya kuwapatia bao la kuwatia nguvu Mali dakika 10 baadae kabla ya Jonathan Bolingi kuifungia DR Congo bao la tatu lililohitimisha mchezo huo mnamo dakika ya 73.
Ubingwa huo unaashiria uwepo wa vipaji nchini DR Congo hasa inapozingatiwa kuwa klabu ya TP Mazembe, iliyochangia nyota kadhaa kwenye kikosi cha mabingwa hao, ilitwaa ubingwa wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika miezi miwili iliyopita.
Kwa upande mwengine sifa zaidi zinamstahili mwalimu Florent Ibenge ambaye pia aliiongoza DR Congo kushinda nafasi ya tatu kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika mapema mwaka jana.
Kwenye mchezo mwengine Ivory Coast waliwafunga Guinea 2-1 na kutwaa nafasi ya tatu huku golikipa wao Abdoul Cisse akifanya kazi kubwa kwa kuokoa mikwaju miwili ya penati.
Golikipa huyo aliokoa mkwaju wa penati uliopigwa na Ibrahima Sankhon kwenye dakika ya 27 na baadae ule wa Alseny Camara kwenye kipindi cha pili cha mchezo.
Magoli ya Ivory Coast yaliwekwa wavuni na Mohamed Youla na Badie Gbagnon huku lile la kufutia machozi la Guinea likifungwa na Aboubacar Leo Camara dakika tano kabla ya mchezo kumalizika.