TAFUTA picha mnano au video ya Giorginio Chiellini akifanya uhuni wa kumvuta jezi kiungo wa pembeni wa England, Bukayo Saka na kumlazimu mwamuzi wa mchezo kuashiria madhambi na kumlima kadi ya njano.
Ulikuwa mchezo wa fainali ya Kombe la Mataifa ya Ulaya, EURO 2020 iliyomalizika jijini London kwenye dimba la Wembley. Safu ya ulinzi ya Italia imedumu kwa takirbani miaka 15 ikiwahusisha walinzi wawili Leonardo Bonucci na Giorginio Chiellini.
Kwa mtazamo wangu hawa ni mabeki wa soka la kihuni au la mitaani ambako mbinu zote za kihuni wamekuwa wakizitumia katika kushinda mechi. Kama kuna mchezaji ambaye ningetamani wacheze naye pamoja basi ni Sergio Ramos ambaye ni mhuni mwenzao, na mbele yao kiungo angekuwa Carlos Casemiro. Nafahamu mashabiki wa Liverpool watakereka hapa kwa kukumbushia tukio la ‘kabali’ ya Ramos kwa Mohammed Salah.
Hao ni wachezaji ambao wanamudu kutumia uhuni wao katika mchezo na kuhakikisha washambuliaji na viungo hawafurukuti. Wengi wanakumbuka tukio la kuvutwa jezi Bukayo Saka, lakini ni machache mno katika ulimwengu wa soka wa leo watajadili kompyuta na mwelekeo wa soka la dunia yetu.
Chiellini ni mchezaji mkongwe ambaye ameshiriki EURO akiwa na miaka 36 na kushangaza zaidi amecheza kwa kiwango bora pasipo kutetereka. Italia ilionekana kama vile iko chini ya mabeki vijana, lakini wastani wa umri wao unawafanya watajwe kama mabeki wazee.
Siri ya ufanisi wao si vipaji na ubora pekee bali pia matumizi ya mbinu za kucheza kwa timu yao, ambazo ni matunda ya mabadiliko ya soka yanayaowapa nafasi hata mabeki hao wazee kutamba, wakicheza kwa uhuru na kutuikia mbinu kuliko zile kashaksh za soka la zamani.
Kwa upande wa mbinu kupitia Kompyuta Cheillini na Bonucci ni wachezaji wazuri hadi sasa waliokulia zama za uhuni na soka la kashkash nyingi hadi la sasa matumizi makubwa ya akili kupitia kompyuta.
Kwamba Kompyiuta imewafanya wachezaji wengi waliokuwa wakidhaniwa umri wa umewatupa mkono waendelee kutamba kwenye ulimwengu wa soka.
Miaka ya nyuma ilifahamika kuwa wachezaji wakifikisha umri wa miaka 30 wengi walikuwa wanaanza kushuka viwango na timu nyingi ziliwasajili kwa ajili ya kutoa uzoefu wao kwenye vikosi vyao. Pia kasi zao uviwanjani hazikukidhi matakwa ya mabenchi ya ufundi.
Fikiria nyota kama George Weah alihama AC Milan akaenda kucheza Chelsea, Nikolas Anelka naye akaelekea Chelsea na Man City wakiwa wachezaji ambao walishavuka miaka 30.
Luis Figo aliondoka Real Madrid kwenda Inter Milan, kisha Raul aliondoka Real Madrid kwenda Schalke 04. Wachezaji hao kwa namba za umri wao walionekana kupitwa na wakati licha ya huko walikokwenda kuonesha uwezo kiasi fulani.
Cristiano Ronaldo ana umri wa miaka 36 kwa sasa na ametoka kushiriki michuano ya EURO. Ronaldo wa sasa si yule wa Sporting Lisboa (Lisbon), Manchester United na Real Madrid. Uwezo wake wa kukaa na mpira na kukokota umepungua mno, lakini ni mchezaji hatari anayepangwa na ‘kompyuta’ ili akae kwenye eneo la kupachika mabao.
Jamie Vardy amewahi kuzungumzia suala hilo la umri na mbinu za kisasa za makocha. Alimkariri kocha wao Brendan Rodgers alivyomfundisha namna ya kutotumia nguvu nyingi na kukimbia maili nyingi uwanjani kulimngana na umri wake.
Kwa Rodgers alitaka Vardy awe anakaa eneo la 18 na hapaswi kuvuka katikati ya dimba kuingia eneo lao bali kuzunguka eneo la mshambuliaji ili kazi yake iwe kupachika mabao tu. Hivi ndivyo makocha wanavyogeuza umri mkubwa kuwa fursa.
Leo hii mambo yamehamia kwenye mabeki, na ndio maana tunawaona Thiago Silva akiwa bando uwnajani pale Chelsea na Brazil. Timu nyingi zilizoshiriki Euro zilitumia mfumo wa mabeki watatu nyuma.
Ni mfumo huo ndio uliwapa wakati mzuri Bonucci na Chiellini. Hawakuwa mabeki wa kukimbizana na washambuliaji wala mawinga wenye kasi. Timu pekee ambayo iliwatumia mawinga wake vizuri ni Ubelgiji, ingawa walitolewa. Ubelgiji wakiwa na Roberto Martinez na Thiery Henry walikuwa na kizazi kizuri ambacho wameshindwa kukitumia vizuri.
Bonucci na Cheillini ni kielelezio cha wahuni wa soka kuendelea kutamba kwa sababu mbinu za makocha wa sasa zinawanyima nafasi wachezaji wenye vipaji vikubwa kuwa wa kipekee hivyo kuchangamana na wale wenye vipaji vya wastani kisha wote wakatuikia mbinu za aina moja.
Kasi na uwezo wa Federico Chiesa na Raheem Sterling vinafichwa zaidi katika mbinu za timu. Ubora na kipaji cha Barella ulifichwa sababu ya mbinu za mwalimu Mancini ingawa kila mara alikuwa kikosi cha kwanza.
Mbinu za Mancini za viungo watatu katikati ya dimba vilimnyima uhuru Barella, laiti kama angecheza kiungo cha ushambuliaji kwa uhuru wa kipaji chake bila shaka angekuwa na mashuti ya kutosha kama Damsgaard kuliko ilivyokuwa.
Hali kadhalika John Stones ambaye awali pale Everton alionekana kuwa beki mhuni, sasa amebadilika na kuwa ‘beki mtanashati’ kama Harry Maguire na kuwaachia jukwaa akina Chiellin,Bonucci na Ramos wakiwa wachezaji wa aina yake. Stones ananikumbusha uchezaji wa Tony Adams, kwamba ni wachezaji wababe lakini wanacheza ‘kitanashati’ zaidi, na ambao soka la leo la mbinu kubwa linawabeba na kuondoa ule uhuni uhuni wa mpirani.
Kwamba wachezaji wahuni hao ni aina ya wale ambao hucheza soka la ‘undava undava’ au ‘hapendwi mtu’ kama ilivyozoeleka mitaani. Staili hiyo alikuwa nayo pia Nemanja Vidic alipokuwa Manchester United au Marco Materrazzi akiwa na Inter Milan ya Italia.
Na kila ninavyoona uchezaji wa timu za kisasa kuna mabadiliko makubwa. Uchezaji hautegemei tena vipaji maridhawa kama Samba ya Brazil enzi hizo au kuwaona wachezaji kama Pablo Aimar na,Ariel Ortega wakidensi mpirani na Argentina au El Hadji Diouf pale Senegal na wengineo wengi ambao soka la kileo lingewapiga kumbo. Ni mabadiliko makubwa kwenye kandanda hadi wazee kama Bonucci,Chiellini,Ramos na Thiago Silva wanaonekana eti vijana mpirani, kisa kompyuta.