KOMBE la Mataifa ya Afrika (CAN), ndiyo michuano mikubwa ya soka katika bara la Afrika inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Kwa mara ya kwanza, michuano hii ilifanyika mwaka 1957 na kuanzia mwaka 1968 ndipo utaratibu wa kuchezwa kila baada ya miaka miwili ulipoanza.
Katika mashindano ya kwanza mwaka 1957 timu shiriki zilikuwa kutoka mataifa matatu tu yaani, Misri, Sudan na Ethiopia.
Nchi nyingine ambayo ilitajwa kushiriki katika mashindano haya ni Afrika Kusini ambayo hata hivyo ilinyimwa nafasi hiyo kutokana na sera zake za ubaguzi wa rangi kwa wakati huo.
Baada ya hapo mashindano yameendelea kukua na kuzihusisha nchi nyingi zaidi na hivyo kuwezesha kuwapo kwa utaratibu wa mashindano ya awali ya kusaka tiketi ya kushiriki fainali zenyewe na hatimaye timu shiriki kufikia 16.
Historia ya Kombe la Mataifa ya Afrika inaanzia Juni mwaka 1956 katika mkutano wa tatu wa FIFA mjini Lisbon, Ureno, baada ya kiubuka wazo la kuanzishwa kwa CAF.
Hapo jambo kubwa lililofikiriwa ni kuanzishwa kwa mashindano ya Bara la Afrika ambayo yalifanyika kwa mara ya kwanza, Februari 1957 katika jiji la Khartoum, Sudan.
Katika mashindano haya hakukuwa na mechi za kufuzu ambako nchi nne waanzilishi wa CAF, Misri, Sudan, Ethiopia na Afrika Kusini zilipanga mahali pa kufanyika michuano hiyo.
Afrika Kusini ilifutwa katika michuano hiyo baada ya kukataa kutuma kikosi chenye mchanganyiko wa wachezaji weusi na wazungu weupe hali ambayo ilitosha kuifanya Ethiopia iende moja kwa moja hadi hatua ya fainali.
Hali hiyo ilisababisha pia kuchezwa mechi mbili tu hadi bingwa kupatikana, Misri iliumana na Sudan katika hatua ya Nusu Fainali na kushinda na baadaye kuifunga Ethiopia katika hatua ya fainali na kutawazwa bingwa wa kwanza wa CAN.
Ethiopia ilikuwa icheze Nusu fainali na Afrika Kusini ambayo iliondolewa na hivyo kubahatika kwenda fainali moja kwa moja.
Miaka miwili baadaye, Misri ilikuwa mwenyeji wa mashindano hayo yaliyofanyika katika jiji la Cairo, ambayo pia yalizishirikisha timu zile zile tatu na Misri ikatwaa ubingwa kwa mara ya pili kwa kuibwaga Sudan.
Mashindano yalizidi kupata umaarufu, mwaka 1962 yalifanyika mjini Addis Ababa, Ethiopia na kwa mara ya kwanza kulikuwa na michuano ya awali ya kufuzu kushiriki fainali hizo ili kupata timu nne zitakazoshiriki hatua ya fainali.
Wenyeji Ethiopia na mabingwa watetezi Misri walifuzu moja kwa moja na timu nyingine mbili zilizoshiriki ni pamoja na Nigeria na Tunisia.
Kwa mara ya tatu, Misri ilifikia hatua ya fainali lakini safari hii iliangushwa na Ethiopia ambayo ilitwaa taji hilo baada ya kuibwaga, Tunisia katika hatua ya Nusu Fainali na baadaye kuiangusha Misri katika dakika za nyongeza.
Ghana ambao ni wenyeji wa fainali za CAN hapo mwakani, ilishiriki kwa mara ya kwanza mwaka 1963 ikiwa mwenyeji na kulibeba taji baada ya kuibwaga Sudan, katika hatua ya fainali.
Miaka miwili baadaye, Ghana tena ililibeba taji hilo nchini Tunisia ikiwa na kikosi ambacho kilijaa wachezaji wapya huku waliotwaa taji hilo mwaka 1963 wakiwa wawili tu. Hadi hapo Ghana ilijiwekea rekodi ya kutwaa taji hilo mara mbili sawa na Misri.
Utaratibu wa fainali za mwaka 1968 ulibadilika kwa kujumuisha timu nane kati ya 22 zilizoshiriki katika hatua ya awali ya kuwania kufuzu, timu ambazo baadaye zilifuzu nane na kupangwa katika makundi mawili ya A na B.
Katika utaratibu huo mpya, timu mbili zilizofanya vizuri katika kila kundi zilisonga mbele katika hatua ya Nusu Fainali, mfumo ambao uliendelea kutumika hadi mwaka 1992.
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) ilitwaa taji hilo kwa mara ya kwanza mwaka 1968 kwa kuifunga Ghana katika mechi ya fainali.
Katika fainali za mwaka 1968, mshambuliaji nyota wa Ivory Coast, Laurent Pokou aliibuka mfungaji bora akiwa amefunga mabao sita na kufanya hivyo tena katika fainali za mwaka 1970 kwa kufunga mabao manane.
Rekodi yake ya mabao 14 katika fainali mbili imeendelea kuwa rekodi ya kipekee katika michuano hiyo.
Fainali za mwaka 1970 zilifanyika nchini Sudan na kwa mara ya kwanza katika historia, fainali hizo zilianza kuonyeshwa kwenye Televisheni huku wenyeji wakibeba kombe hilo baada ya kuwabwaga Ghana ambao walikuwa wakifikia hatua hiyo kwa mara ya nne mfululizo.
Kuanzia mwaka 1970 hadi 1980 nchi sita zilitamba katika michuano hiyo kwa kuibuka vinara, nchi hizo ni Sudan, Congo Brazaville waliolibeba mwaka 1972, Zaire (DRC) Morocco, Ghana na Nigeria.
Zaire ilibeba kombe hilo kwa mara ya pili mwaka 1974 (awali ililitwaa ikiwa inatumia jina la DRC kabla ya kubadili na kuwa Zaire na sasa kurudia jina la DRC) baada ya kuilaza, Zambia katika mechi ya fainali.
Mechi hiyo ya fainali ililazimika kuchezwa mara mbili baada ya timu hizo kutoka sare ya mabao 2-2 katika dakika za nyongeza na kurudiwa siku mbili zilizofuata ambako Zaire ilishinda kwa mabao 2-0.
Katika mechi hizo, mabao yote manne ya Zaire katika mechi hizo mbili yalifungwa na mshambuliaji wao, Mulamba.
Morocco kwa mara ya kwanza ilibeba taji hilo mwaka 1976 nchini Ethiopia wakati Ghana ililibeba taji kwa mara ya tatu mwaka 1978 na kuwa nchi ya kwanza kujiwekea rekodi ya kubeba taji hilo mara tatu.
Mwaka 1980, Nigeria ilikuwa mwenyeji wa fainali hizo ambazo pia Tanzania ilishiriki na wenyeji Nigeria walifanikiwa kulibakisha kombe nyumbani baada ya kuilaza, Algeria katika fainali.
Ghana iliendeleza ubabe mwaka 1982 kwa kulitwaa kombe nchini Libya, ilianza kwa kuinyuka, Algeria katika hatua ya Nusu Fainali na kuumana na wenyeji Libya katika mechi ya fainali kwa mikwaju ya penalti.
Miaka miwili baadaye, Cameroon walibeba taji hilo kwa kuilaza Nigeria na mwaka 1986 walifikia hatua ya fainali na kuumana na Misri lakini ni Misri ndio walioibuka vinara kwa mikwaju ya penalti.
Mwaka 1988, nyota ya Cameroon iling’ara baada ya kufikia hatua ya fainali na kulibeba kombe kwa ushindi dhidi ya Nigeria wakati mwaka 1990, Nigeria ilianguka tena na kujikuta ikishindwa kulibeba kombe ambalo lilichukuliwa na Algeria.
Katika fainali za mwaka 1992, idadi ya timu iliongezeka na kufikia 12 ambazo ziligawanywa katika makundi manne, kila kundi lilitoa timu mbili zilizosonga mbele katika hatua ya Robo Fainali.
Mchezaji mahiri wa Ghana, Abedi Pele Ayew ambaye alifunga mabao matatu katika fainali hizo ndiye aliyetangazwa kuwa mwanasoka bora wa fainali hizo kutokana na mchango wake ulioiwezesha timu hiyo kufikia hatua ya fainali.
Hata hivyo, katika mechi ya fainali dhidi ya Ivory Coast alitolewa nje na timu yake ilishindwa kufurukuta.
Utaratibu wa timu 12 uliendelea mwaka 1994 nchini Tunisia ambako wenyeji walijikuta wakilala katika hatua ya kwanza na Nigeria ambao ndio waliofikia fainali na kuibwaga Zambia hadi kutwaa taji.
Nigeria ambayo wakati huo ilifuzu kwa mara ya kwanza fainali za Kombe la Dunia iliwafunga Zambia ambao mwaka mmoja kabla ya fainali hizo ilipatwa na msiba mkubwa wa kufiwa na nyota wake waliokufa katika ajali ya ndege. Rashid Yekini, mshambuliaji wa Nigeria aliibuka kinara wa upachikaji mabao akiwa na mabao matano, Yekini katika fainali za mwaka 1992 aling’ara kwa mabao manne.
Mwaka 1996, Afrika Kusini ilikuwa mwenyeji ikishiriki kwa mara ya kwanza baada ya kusimamishwa kutokana na sera za ubaguzi wa rangi zilizokuwa zikitawala nchini humo.
Timu ziliongezwa na kufikia 16 ambazo ziligawanywa katika makundi manne ingawa baadaye timu hizo zilibakia 15 baada ya Nigeria kujitoa katika hatua za mwisho kwa sababu zilizotajwa kuwa ni za kiusalama.
Afrika Kusini ikiwa na kikosi maarufu cha Bafana Bafana ililibakisha taji hilo nyumbani na nahodha wa timu hiyo, Neil Tovey akawa mzungu wa kwanza kulibeba juu kombe hilo.
Miaka miwili baadaye fainali hizo zilipigwa nchini Burkina Faso ambako Afrika Kusini ilifurukuta na kukawa na matumaini makubwa ya kulibeba taji hilo lakini timu hiyo ilishindwa kutamba mbele ya Misri walioibuka vinara.
Mwaka 2000 fainali ziliandaliwa kwa ushirikiano wa nchi za Ghana na Nigeria ambao walichukua nafasi ya Zimbabwe iliyoandaliwa kuwa mwenyeji.
Cameroon ilifanikiwa kulibeba taji hilo baada ya kuibwaga Nigeria kwa mikwaju ya penalti. Mambo yaliinyookea tena Cameroon au Indomitable Lions mwaka 2002 kwa kuwafunga Senegal ambao walifikia hatua ya fainali kwa mara ya kwanza na mwaka 2004 wenyeji Tunisia walifanikiwa kulibakisha kombe nyumbani baada ya kuilaza, Morocco kwa mabao 2-1.
Mwaka 2006, kombe pia lilichukuliwa na wenyeji, Misri, ambao pia walijiwekea rekodi ya kubeba taji hilo kwa mara ya tano, Misri wakiwa nyumbani mjini Cairo waliibwaga Ivory Coast katika fainali.
Bila shaka kwa sasa anasubiriwa kwa hamu kinara wa taji hilo kwa mwaka 2008.
Rekodi za washindi wa CAN tangu kuanzishwa kwake…
Mwaka Nchi iliyoshinda
1957 Misri
1959 Misri
1962 Ethiopia
1963 Ghana
1965 Ghana
1968 DRC
1970 Sudan
1972 Congo Brazzaville
1974 DRC
1976 Morocco
1978 Ghana
1980 Nigeria
1982 Ghana
1984 Cameroon
1986 Misri
1988 Cameroon
1990 Algeria
1992 Ivory Coast
1994 Nigeria
1996 Afrika Kusini
1998 Misri
2000 Cameroon
2002 Cameroon
2004 Tunisia
2006 Misri
2008 …….?????