*Arsenal yajipa hadhi ya nyota tano
Wakati Chelsea wamepoteza nafasi ya kuingia fainali ya Capital One Cup, Arsenal wamewakandika West Ham United mabao 5-1 kwenye Ligi Kuu ya England (EPL).
Chelsea waliingia uwanjani ugenini kwa Swansea wakijiamini, hasa baada ya kocha wao wa muda, Rafa Benitez kuwatoa wasiwasi washabiki kwamba kombe hilo lipo.
Lakini waliingia uwanjani wakiwa na deni la mabao mawili, kwani katika mechi ya awali Stamford Bridge, walilala kwa mabao 2-0.
Mchezo wa Jumatano hii ulimalizika kwa timu kuondoka Liberty Stadium zikiwa suluhu, hivyo Swansea kusonga mbele kwa wastani wa mabao mawili hayo.
Hii ni mara ya kwanza kwa timu hiyo ya Wales kuingia fainali ya kombe kubwa katika historia yake.
Mchezo ulikuwa na tukio la kiungo wa Kibelgiji wa Chelsea, Eden Hazard kupewa kadi nyekundu kwa kumpiga kijana mwokota mipira, kwa madai ya kukatalia mpira uliotoka kando ya lango la Swansea.
Kwa ushindi huo, Swansea watawavaa Bradford City wanaocheza ligi ndogo ya daraja la pili, ambapo fainali ya Kombe la Ligi itafanyika katika uwanja wa Wembley Februari 24.
Chelsea walianza mchezo kwa nguvu, Demba Ba akianza badala ya Fernando Torres, aliyeingia kipindi cha pili hata hivyo, lakini hawakupata bao hata la kuotea.
Vijana wa Benitez walishindwa kushikilia rekodi yao ya kufanya vizuri kwenye mechi za ugenini, na ni kombe la pili limewaponyoka, baada ya kombe la klabu la dunia.
Mara ya mwisho kwa Swansea kucheza kwenye nusu fainali ya kombe kubwa kama hili ilikuwa mwaka 1964, kwenye FA Cup, walipofungwa na Preston North End mabao 2-1.
Katika mechi ya kiporo ya EPL, Arsenal waliwafurahisha washabiki wa nyumbani Emirates, walipowafunga West Ham wa Sam Allardyce mabao 5-1.
Huu ni ushindi mkubwa wa aina yake kwenye ligi kwa mwaka huu, licha ya kuanza vibaya mechi kwa kufungwa dakika ya 18 kupitia kwa Jack Collison.
Hata hivyo, mshambuliaji wa Kijerumani, Lukas Podolski alisawazisha dakika chache tu baadaye.
Kipindi cha pili Arsenal walidhibiti karibu maeneo yote, ambapo mvua ya mabao ilianza dakika ya 47 kwa Olivier Giroud kuweka kimiani bao, kabla ya kumtengea Santi Cazorla dakika ya 53 naye kumsalimu golikipa.
Mchezaji aliyesumbua kuhuisha mkataba wake kwa muda mrefu na hatimaye akakubali, Theo Walcott naye alizifumania nyavu katika dakika ya 54 wakati Giroud alirejea tena golini na kufunga kitabu cha mabao katika dakika ya 57.
Mwaka 2007, West Ham walikuwa timu ya kwanza kuwafunga Arsenal katika uwanja mpya wa Emirates, ambapo Bobby Zamora alifunga bao pekee la mchezo, na Jumatano hii ilionekana kana kwamba historia ingejirudia, baada ya West Ham kutangulia kufunga.
Kwa matokeo hayo, Arsenal wanabaki nafasi ya sita, lakini wakiwa na pointi 37, moja nyuma ya Everton na nne nyuma ya mahasimu wao wa London, Tottenham Hotspurs.
Wamewaacha Liverpool na West Bromwich Albion waliokuwa wamefungana kwa pointi nyuma yao kwa alama tatu.
Kocha Arsene Wenger alieleza kabla kutokuwa na wasiwasi wa kuingia nafasi nne za juu, isipokuwa anasikitishwa na wachezaji wake kupoteza mechi kubwa.
Arsenal walifungwa na Manchester United, Manchester City na Chelsea. Wenger amekuwa akishikilia kwamba kikosi chake ni imara, wachezaji wanajituma na kwamba anatarajia watabadilika.