Menu
in , , , ,

KOMBE LA DUNIA LA VIJANA

*Mali, Senegal robo fainali

*Nigeria watolewa na Ujerumani

Michuano ya Kombe la Dunia kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 20 imefika patamu, ambapo Mali na Senegal wameingia robo fainali.

Mali waliwashangaza Ghana waliokuwa wakipewa nafasi kubwa ya kusonga mbele kwa kuwachabanga 3-0 mabingwa hao wa 2009.

Kwenye kundi lao la B Ghana waliwafunga Argentina na kuwa juu hivyo kupewa nafasi kubwa ya kuingia robo fainali.

The Eaglets waliuanza mchezo kwa nguvu na wakafanikiwa kuwaibua washabiki wao vitini katika dakika ya 20 tu pale Diadie Samassekou alipokwamisha kombora nyavuni baada ya kugongeana haraka haraka na Adama Traore.

Baada ya mapumziko walipata bao la pili kupitia kwa Diedonne Gbakle, aliyekatiza kutoka upande wa kulia, akawalamba chenga wachezaji wawili wa Ghana na kuachia fataki na kuzama chini tu ya mtambaa wa panya.

Ghana walishaona Jua limewachwea na wakati wakijaribu bila mafanikio kurudia hali yao ya zamani, walipachikwa bao jingine dakika tisa kabla ya mpira kumalizika, kwa bao la Aboubabacar Doumbia aliyewatoka walinzi wa Ghana na kuweka kitu kwenye kona ya goli.

Senegal nao walifanikiwa kuingia hatua ya robo fainali baada ya kuwafunga Ukraine kwa mikwaju ya penati, kwani katika muda wa kawaida walikwenda sare ta 1-1, shujaa wa mechi akiwa kipa Ibrahima Sy.

Licha ya kuingia katika muda wa ziada, walibakia nguvu sawa, mabao yakiwa yamefungwa na Artem Biesiedin’ dakika ya 77 na kusawazishwa na Sidy Sarr dakika ya 83.

Katika changamoto ya penati, Senegal walishinda kwa 3-1. Kipa Syanayechezea klabu ya L’Orient wa Ufaransa aliokoa mikwaju ya Yevhen Chumak, Yevhenii Nemtinov na Valerii Luchevych, huku wapigaji wote wa Senegal wakitikisa nyavu za adui.

Kwingineko Nigeria wametolewa kwenye michuano hiyo na Ujerumani, baada ya kuwafunga bao moja kwenye mechi ya hatua ya 16 bora.

Flying Eagles walijitahidi kila hali lakini bahati haikuwa yao, kwani hawakuweza kutengeneza nafasi za kufunga kwenye mechi hiyo iliyofanyika Christchurch.

Ujerumani walipata bao lao katika dakika ya 19 tu pale Levin Oztunali alipotikisa nyavu kwa mpira wa mguu wa kushoto kutoka ukingoni mwa eneo la penati. Nigeria waliokuwa washindi wa pili mwaka 1989 na 2005 walijaribu kupambana lakini mambo yalikuwa magumu.

Ujerumani sasa watapepetana na Mali kwenye robo fainali Jumapili hii Christchurch wakati ambapo Senegal watakipigfa na Uzbekistan huko Wellington.

Katika mechi nyingine Dostonbek Khamdamov alifunga mabao mawili ndani ya dakika 10 na kuwahakikishia Uzbekistan ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Austria. Kwa matokeo hayo, Uzbekistan watakwaana na Senegal Jumapili hii, ikiwa ni mara ya pili mfululizo wanafika hatua hii.

Mechi zinazochezwa Alhamisi hii kupata timu nyingine za kuvuka ni Ubelgiji dhidi ya New Zealand wakati Brazil wanachuana na Uruguay.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version