Menu
in

KOMBE LA DUNIA 2022

Neymar

Brazil wamefuta utegemezi wao kwa Neymar? 

Ukitaja fainali za Kombe la Dunia unaitaja Brazil. Wao ndio wanaongoza kutwaa  kombe hilo mara tano. Brazil ni nchi ambayo kila taifa linatamani kuchza dhidi  yao na kuwafunga. Kila kocha anatamani kuwafunga Brazil ili asifiwe na kukuza  wasifu wake. Kwahiyo Brazil ni kama nembo ya fainali za Kombe la Dunia.  

Tangu Kombe la Dunia lianzishwe Brazil imeshiriki fainali zote. Hili ni taifa  linalowavutia wengi na makocha wanaamini ndilo linalotakiwa kuchungwa kila  unapopangwa nao. 

Imepita miaka 18 bila kutwaa taji la Kombe la Dunia. Mara mwisho Brazil kutwaa  kombe hilo ilikuwa kwenye fainali za mwaka 2002 zilizofanyika nchini Korea  kusini na Japan. 

Brazil inajipanga upya kupitia vipaji vipya katika ulimwengu wa kandanda. Kizazi  kipya ambacho kimekabidhiwa jukumu la kutamba kwenye soka miaka kadhaa  ijayo. Wachezaji chipukizi wanataka namba katika timu ya taifa maarufu kama  Selecao.  

Thiago Silva bado ni nahodha wao, japo ana miaka 36 kwa sasa, na ifikapo fainali  za Kombe la Dunia mwaka 2022 atakuwa na miaka 38 zitakazofanyika nchini  Qatar. 

Ingawaje miaka ya karibuni Brazil haijawa taifa tishio kwenye mashindano  linapofika suala la wachezaji ndani ya uwanja, lakini nje ya uwanja jina lao ni  kubwa na tishio tosha. Miaka ya karibuni vipaji vya Kibrazil havikuwa tishio, na  madhara yake yalionekana kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014  lililoandaliwa nchini kwao ambapo walizabwa mabao 7-1 na Ujerumani kwenye  mchezo wa nusu fainali.  

Tangu wakati huo Brazil imeanza mikakati ya kuibuka upya kwenye mchezo huo  kupitia vipaji mbalimbali. mojawpao ni kuhakikisha wanaachana na utegemezi  wao kwa supastaa Nermay Junior. Kwanini wana mwelekeo huo?

Iko hivi. Mastaa kadhaa wanacheza Ligi kuu England, lakini linapofika suala la  mashindano ya kimataifa mafanikio yao ni hafifu. Kwa sasa wana kizazi kipya,  lakini swali la kujiuliza je kizazi hiki kitaweza kuleta mafanikio ikiwemo kutwaa  kombe la dunia tena?  

WAKONGWE NI DHAHABU 

Linapofika suala wachezaji nyota Brazil ni lazima mwelekeo wa ushindi unaanzia  kwao. Baadhi ya wachezaji hao wana majina makubwa, wamefanya mambo  makubwa, hivyo wanahitaji kuongezewa damu change ili kuibuka na ushindi. Kwa  kipindi hiki Thiago Silva ndiye mkongwe zaidi kuliko wote. 

Beki huyo wa kati ni kipenzi cha wachezaji wengi chipukizi. Tangu alipoibuka  katika soka na kuchaguliwa timu ya taifa, Silva hajawahi kuwaangusha Brazil na  wala hajawekwa kando. Ni kama amejimilikisha nafasi hiyo. Kwa sasa ana miaka  36 hii ina maana bado ni mchezaji muhimu katika nafasi yake na wanahitaji  mchango wake katika ulinzi ili kuimarisha uwezo wa chipukizi. 

Mara nyingi amecheza sambamba na Marquinhois, ambaye wamecheza wote PSG,  kisha amewahi kupangwa pamoja na wengine kama Ederr Militao wa Real Madrid.  Nyota wote wawili hawajaweza kumwondoa kikosini Thiago Silva. Sasa kama  wanamtegemea Silva, je Brazil wataweza kusonga mbele? 

Kocha wao Tite ana mikakati ya muda mrefu kuhakikisha Brazil inafanya mambo  makubwa kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka 2022. Pengine wataingiza  timu yenye ushindani mkali kuliko miaka ya 10 iliyopita. Tite anakabiliwa na  kibarua kigumu cha kufanya uamuzi wa uteuzi wa wachezaji. 

KUACHA KUMTEGEMEA NEYMAR 

Kwa kipindi cha miaka 10 sasa huwezi kuzungumzia Brazil bila kutaja jina la  Neymar. Mshambuliaji huyo wa PSG anaipenda nchi yake na amechora tattoo  mwilini. Wakati fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014 alikabiliwa na presha  kubwa mno.  

Mabega yake yalibeba mzigo mzito wa mamilioni ya wananchi wa Brazil  waliokuwa na matumaini yote kwake. Naye hakuwaangusha, alijitahidi kadiri ya 

uwezo wake kabla ya kufanyiwa madhambi kwenye mfupa wa mgongoni  yaliyosaabisha ashindwe kuendelea kucheza michezo mingine.  

Kwenye mchezo wa nusu fainali dhidi ya Ujerumani Neymar hakuweza kucheza.  Wabrazil waliamini bila Neymar maisha yao kisoka yalishakwama mbele ya  Ujerumani. Baada ya fainali hizo maisha ya Naymer yalionekana kama yamepotea  kama nahodha aliyepoteza jaketi la kujiokoa.  

Brazil ilijengwa kupitia Neymar tangu akiwa timu za taifa za vijana. kila kitu  kilifanywa ili Neymar afanye vizuri. Wachezaji walielewa iliBrazil ipate mafanikio  ni lazima Naymer apachike mabao ya ushindi, na pasi ziende kwake. 

Licha ya kupata matokeo, benchi la ufundi liliamua kuondo utegemezi huo katika  timu. Mawazo ya kumtegemea Neymar kikosini yaliondolea haraka na mwanzo  mpya wa mbinu uliwekwa kunusuru taifa hilo.  

Tite na wasaidizi wake pamoja Shirikisho la Soka CBF waliona majeraha  anyaopata Neymar mara kwa mara yanakwaza maendeleo yao. Baada ya  kuondolewa Neymar kwenye mipango ya timu ya taifa mambo mapya yakaanza  kuibuka. Kisha Brazil ikatwaa kombe. 

Mwaka 2019 Brazil walikuwa wenyeji wa fainali za Copa America. Neymar  hakushiriki mashindano hayo baada ya kupata majeraha kwenye mchezo w  akirafiki dhidi ya Qatar, hivyo ilikuwa wazi kuwa nyota huyo hatakuwepo kwa  muda. Tite alikiongoza kikosi chake kwenye fainali hizo akipanga wachezaji  wapya ambao walibeba majukumu yote na kuibuka washindi.  

Tangu fainali hizo ilionekana wazi Brazil wameacha kumtegemea Neymar.  Kwenye mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Bolivia  wlaipata ushindi wa mambo 5-0 mwezi Oktoba mwaka huu. Kwahiyo majukumu  ya kufunga mabao na kutengeneza yanahusisha wachezaji wote sio mmoja kama  ilivyokuwa kwa Neymar. Je, ni dalili ya mwanzo mpya? Muda utaongea. 

VIPAJI VIPYA, DAMU CHANGA 

Kama nchi, Brazil inasifikakwa vipaji. Haijawahi kuishiwa vipaji hata kama  haifanyi vizuri kimataifa. Baada ya kuondokana na utegemezi kwa Neymar, sasa 

vipaji vipya vimeingia. Kwenye fainali za Copa Amaerica nyota ya mshambuliaji  Everton Soares iling’ara, naye Richarlison akaweka alama nzuri kikosini.  

Yupo Rodrygo Goes ambaye anakuja kuipa uhai Brazil kwenye fainali za mwaka  2022. Akiwa na miaka 19 Rodrygo Goes ameibuka kwenye mechi muhimu na  kufanya mambo makubwa. Baadhi ya wachambuzi wanasema Rodrygo atachukua  nafasi ya Neymar na kuwa mshambuliaji wao mahiri miaka ijayo.  

Rwal Madrid walilazimika kulipa kiasi cha pauni milioni 50 kumsajili Rodrygo  alipokuwa na miaka 17 akichezea klabu ya Santos. Aliitwa kwenye maandalizi ya  mchezo dhidi ya Argentina, ambako Brazil walizabwa bao 1-0 katika mchezo wa  kirafiki. Mastaa wengine walioibuka Brazil ni Lucas Pacqueta (Olumpique Lyon)  na Renan Lodi (Atletico Madrid) watachukua nafasi ya Marcelo. Wengine ni  Wesley Moraes, Garbiel Menino, Bruno Guimaraes, Pedro, Vinicius Junior na  Richarlison. 

UZOEFU WA MAKOMBE 

Tanzania Sports
Timu ya Taifa ya Brazil

Kwa miaka ya karibuni Brazil haiajcheza vizuri na matokeo yake yamekuwa ya  kusuasua. Kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka 2018 nchini Urusi waliishia  robo fainali baada ya kufungwa na Ubelgiji. 

Brazil walishinda mechi nane na kutoka sare moja. Kwa kiasi fulani takwimu hizo  zinawapa nafasi ya kuamini watafanya vizuri fainali zijazo. Tayari mwaka 2019  wamechukua Copa America, wanaongoza kuwania kufuzu kombe la dunia 2022.  

Wapo wachezaji wenye uzoefu wa kutwaa makombe kikosini. Gabriel Jesus na  Phlippe Coutinho wakipangwa na chipukizi kadhaa kwenye mechi za kufuzu  wameonesha kiwango cha kuvutia.  

Argentina wanashika nafasi ya pili nyuma ya Brazil. Licha ya kupitia nyakati  ngumu, lakini sasa Brazil wameonesha wazi wanakuja kuleta mambo makubwa.  Wakifuzu fainali za 2022 bila shaka Tite atashusha kikosi cha maagamizi.  Tusubiri.

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

Leave a Reply

Exit mobile version