Menu
in , , , ,

Kombe la Dunia 2014: Presha yapanda Brazil

 

 
ZIKIWA zimebaki pungufu ya siku 100 kuanza kwa Fainali za Kombe la Dunia Brazil, presha imeanza kupanda kwa wenyeji hao ambao hawajakamilisha maandalizi.

Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) lilikuwa limewataka waandaaji kukamilisha miundombinu ya viwanja vyote mwishoni mwa Desemba mwaka jana, lakini hadi sasa kuna viwanja ambavyo bado.

“Tupo katika mazingira tete kwa sababu mambo hayajakamilika na siku zinakatika,” anasema Katibu Mkuu wa Fifa, Jerome Valcke akizungumzia hali ya viwanja 12 ambavyo nyasi zake zitasiginwa kwenye michuano mikubwa zaidi duniani.

Fifa ilitaka viwanja kukamilika kwa ajili ya kufanyiwa majaribio na marekebisho pale ambapo ingebidi lakini ajabu ni kwamba Sao Paulo, kwa mfano, penye uwanja utakaochezewa pambano la ufunguzi hautakabidhiwa hadi Mei.

Licha ya kuchelewa kukamilisha ujenzi na ukarabati, hali ya kisiasa ilipata kuchafuka, wananchi wakiandamana kupinga gharama kubwa na baadhi ya miji wenyeji kukataa kulipia miundombinu itakayotumika kwa ajili ya wanahabari au shughuli za usalama.

Valcke, hata hivyo, amesema kwamba hakuna mjadala katika hilo na kwamba Brazil wana jukumu la kutekeleza yote kwa sababu yamo kwenye mkataba wa awali wa makubaliano ya kuwa nchi mwenyeji.

Jukumu jingine ambalo baadhi ya miji inaonekana kupiga chenga ni kuhusu uwekaji taratibu na uandaaji wa matamasha kwa ajili ya washabiki licha ya kuwa imesaini kwenye mkataba wa makubaliano, ambapo wetu wengi zaidi huyahudhuria kuliko washabiki wenyewe katika mechi.

Kwa mfano, mwaka 2006 nchini Ujerumani, watu milioni 3.5 walihudhuria kwenye mechi lakini milioni 18 walikwenda kwenye matamasha hayo ambayo ni muhimu kwa sababu huwakutanisha Fifa na wabia wao wa kibiashara na wadau wa soka kwa ujumla.

Mamlaka za miji husika yenye viwanja kwa ajili ya michuano hiyo inaonekana kuogopa kutoa fedha za walipa kodi kwa ajili ya masuala yanayohusiana na soka, ikiogopa maandamano, lawama za ufujaji fedha hasa kama hazitarudi baada ya mashindano.

Huu ni mtihani wka wanasiasa ambao wanashindwa kuamua ikiwa kuwa wenyeji kunaweza kutumiwa kama kete kisiasa ya kuwapandisha kwenye kilele cha mafanikio au kinaweza kuwa kigezo cha kuwang’oa kwenye nafasi zao kwenye uchaguzi ujao au hata kabla ya hapo.

Hata hivyo, Fifa inaelekea kufarijika na jinsi mauzo ya tiketi yalivyokwenda vizuri, mashirika makubwa yanavyoonesha ushirikiano kwao tofauti na hali ilivyokuwa nchini Afrika Kusini miaka minne iliyopita.

Ni kwa sababu hiyo, uenyeji wa Brazil katika Kombe la Dunia unaonekana kuwa chaguo sahihi japokuwa wakati siku pungufu ya 100 zimebaki, utabiri wa miaka mingi iliyopita unaelekea kutimia, ambapo jamaa mmoja alisema mtu mwenye haraka hatakuwa na furaha nchini Brazil, hali inayodhihirika kwa ajina Valcke na Rais Sepp Blatter wa Fifa.

Licha ya Sao Paulo, viwanja vingine vinavyoonekana kuwa na walakini, japokuwa inasemwa vitatengamaa ndani ya muda kabla ya mashindano ni Curitiba na Manaus huku pakiwa na maswali iwapo miundombinu ya viwanja vya ndege itamudu wasafiri kwa sababu maelfu ya wasafiri wakishaingia nchini watakuwa na mipangilio ya kusafiri kwenye miji tofauti haraka haraka, kwanza kwa ajili ya mechi lakini pia kwa utalii msimu huo wa kiangazi, Brazil ikijulikana kwa wingi wa fukwe nzuri na kwenye starehe kubwa.

Watu wengine pamoja na mamlaka bado wanajiuliza iwapo waandamanaji watatokezea tena wakati wa michuano na jinsi dola itakavyowajibu; utulivu utakuwa wa kutosha na kufaa kwenye fukwe, mitaani na kona za kitalii?

Swali kubwa zaidi na linalowaumiza vichwa watu wa Chama cha Soka Brazil na serikali ya nchi ni jinsi timu yao itakavyofanya kwenye michuano, ambapo ikisonga mbele hadi mwisho ndiyo salama yao, la ikitolewa mapema, hasira za Wabrazili zinaweza kuwakia mitaani kwa maandamano lakini pia hawatahudhuria mechi zilizosalia, kana kwamba kifo kimeifika familia.

Kocha wa Brazil, Luiz Felipe Scolari na benchi lake la ufundi hawana wasiwasi na kwa hakika wana furaha na maendeleo waliyofikia hadi sasa kwa kupata uwiano mzuri kwenye kikosi chenye vijana wanaotisha japokuwa kuna shaka kwenye nafasi mbili muhimu – kipa na mshambuliaji wa kati.

Wanapocheza nchini Afrika Kusini Jumatano hii katika pambano la kirafiki, wadau wengi watapenda kuelekeza macho yao kwenye nafasi hizo muhimu, lakini pia nyingine kwa ujumla wake.

Golikipa wao, Julio Cesar aliyekuwa akicheza ligi daraja la pili nchini England na Queen Park Rangers (QPR) hatimaye amekamilisha uhamisho wake kwenda MLS lakini hajapata mechi kubwa za kiushindani.

Scolari bado anajiuliza iwapo amchezeshe Jefferson aliye kwenye kiwango kizuri katika timu ya Botafogo lakini hajapata kujaribiwa akiwa na timu hii ya taifa.

Kwa upande wa mpachika mabao, kuna wasiwasi kwa sababu shujaa wa Kombe la Mabara, Fred, ndio kwanza ametoka kwenye mapumziko ya majeraha ya muda mrefu. Papili wake ni Jo ambaye hajaonesha kiwango cha juu hivi karibuni.
 

51.556588-0.117546

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version