Wakati jina la Zlatiko Krmpotic likitangazwa na mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Yanga, Injia Hersi nilipata wasaa mzuri wa kupita vyanzo mbalimbali kujua kwa undani kuhusu Zlatiko Krmpotic.
Moja ya kitu kikubwa ambacho nilikigundua wakati napitia mengi kuhusu Zlatiko Krmpotic ni kuwa kocha huyu ni mkubwa sana na ana wasifu mkubwa sana.
Wasifu ambao ameutengeneza huko alipotoka. Ameweka alama nyingi na kubwa kila sehemu ambayo alifanikiwa kupita kwenye uchezaji wake na ufundishaji wake wa mpira wa miguu.
Tukumbuke huyu kocha Zlatiko Krmpotic wakati akiwa mchezaji alikuwa anacheza katika eneo la beki wa kati. Eneo ambalo alikuwa analimudu sana.
Kumudu kwake katika eneo hilo kulimfanya awe beki wa timu ya taifa ya Serbia iliyoshiriki michuano ya kombe la dunia. Kwa hiyo Zlatiko Krmpotic ashawahi kucheza kombe la dunia.
Kombe ambalo ni kubwa lenye heshima na hadhi kubwa duniani. Michuano ya kombe la dunia ni michuano ya ndoto kwa wachezaji wengi kutamani kuwa sehemu ya michuano hiyo.
Kocha huyu aliwahi kuwafundisha wachezaji wakubwa. Beki wa zamani wa Manchester City , Alexander Kolarov aliwahi kufundishwa na kocha huyu mpya wa Yanga.
Kocha aliwahi kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya vijana ya Serbia yenye wachezaji waliochini ya umri wa miaka 21. Timu ambayo aliipeleka michuano ya Euro ya vijana.
Zlatiko Krmpotic amepita TP Mazembe akiwa kama kocha msaidizi mwaka 2015 na ndiyo muda ambao yeye alifanikiwa kuwa sehemu ya makocha walioipa kombe la klabu bingwa Afrika.
Kocha huyu kapita vilabu vingi kama Zesco , Polokwane City FC na vingine vingi ambavyo vinabeba wasifu wake mkubwa katika ufundishaji wa mpira wa miguu.
Kocha huyu ashawahi kuwa kocha bora katika ligi mbalimbali kama ligi ya Congo mwaka 2016, aliwahi kuwa kocha bora wa ligi kuu ya Zambia mwaka 2017-2018 na kocha bora wa Botswana mwaka 2018.
Achana na wasifu huu mkubwa wa Zlatiko Krmpotic. Kocha huyu anatakiwa atumike vyema kulingana na wasifu wake mkubwa alionao.
Kocha huyu anatakiwa atengeneze kitu ambacho kinaweza kikawa na msaada kwa Yanga. Yanga inapambana sana kuingia kwenye mabadiliko.
Mabadiliko haya yasiwe kwenye uongozi tu ila yawe mpaka kwenye suala la kujenga falsafa ya mpira kwenye mpira wa miguu Yanga. Huyu kapita sehemu ambazo ni kubwa.
Aliiwezesha timu ya taifa ya vijana ya Serbia kufuzu michuano ya Euro. Angepewa nafasi na Yanga kuchora mchoro mzuri wa kuzalisha wachezaji vijana kwa manufaa ya Yanga. Mashaka yangu ni kuwa kaletwa kwa ajili ya kuifunga Simba.