Wakati kocha wa Ivory Coast Vahid Halihodzic ameshangazwa na kiwango kikubwa kilichoonyeshwa na wachezaji wa Taifa Stars katika mechi yao ya kimataifa ya kirafiki kwenye Uwanja wa Taifa juzi, beki Kolo Toure amesema kiungo wa Stars Abdulhalim Humoud anastahili kucheza Ulaya.
Halihodzic, Mfaransa mwenye asili ya Bosnia, amesema kuwa Stars imecheza katika kiwango cha juu na kwamba wachezaji wanaelewana sana licha ya wageni kushinda 1-0 kupitia goli la mshambuliaji Didier Drogba anayechezea klabu ya ligi kuu ya England ya Chelsea.
“Wanacheza kwa ufundi mkubwa,” alisema kocha huyo kuzungumzia mechi hiyo ambayo aliwatumia wachezaji wake 22 baada ya kubadili wachezaji 10 wakati wa mapumziko.
Halihodzic alisema kuwa Stars ilikuwa inacheza kwa kuelewana, kiufundi na kwa kasi jambo ambalo limesaidia kuipa timu yake maandalizi mazuri ya kuelekea Angola.
“Nilibadilisha timu kwa sababu hapa tumekuja katika maandalizi na wachezaji wote walitakiwa kupata nafasi hiyo ya kuonyesha uwezo wao,” alisema kocha huyo.
Naye beki wa kati wa Ivory Coast Kolo Toure, alimsifu kiungo wa Stars, Abdulhalim Homoud anayefahamika kama ‘Gaucho wa Mtibwa’ akisema ameonyesha kwamba ana kipaji kizuri na endapo atapata nafasi zaidi anaweza kuisaidia timu yake.
“Nimefurahishwa na kiwango cha timu ya Tanzania na hasa yule kiungo, (mweupe na amesuka nywele zake), anaweza kufika mbali,” alisema Kolo ambaye anaichezea Manchester City ya Uingereza.
Kolo aliiambia Nipashe baada ya mechi hiyo kuwa amefurahishwa na kiwango cha wachezaji wa Taifa Stars na hakudhani kwamba wangeweza kutoa ushindani kwa timu yake.
Nahodha wa Ivory Coast, Didier Drogba, alisema pia ameshangazwa na kiwango cha Stars katika mechi hiyo ya kirafiki na kutabiri kwamba wachezaji wakiendelezwa, taifa litashiriki katika fainali za mashindano mbalimbali yanayofuata.
“Wanaelewana na wanaweza kujituma, kuna vitu vidogo vidogo ndio wanatakiwa kujirekebisha,” alisema nyota huyo wa Chelsea.
Naye kocha wa Taifa Stars, Marcio Maximo, amesema kwamba wachezaji wake wameonyesha kwamba wanaweza baada ya kuonyesha uwezo wa juu katika mechi hiyo licha ya kufungwa.
Maximo alisema pia kwa mara ya kwanza ameshangazwa kuona mashabiki wa timu hiyo wakitoa pongezi licha ya kuwa wamefungwa na anaamini kwamba hilo limetokana na kiwango walichokionyesha katika kuwakabili nyota hao wa klabu za Ulaya.
Mbrazili huyo pia aliwasifu wachezaji Abdulhalim Homoud, Stephano Mwasika na Kelvin Yondani kutokana na jinsi walivyokuwa wanajituma katika mchezo huo.
“Mechi ilikuwa ngumu, lakini mashambulizi yalikuwa sawa kwa sawa, nashukuru imesaidia kuiweka Tanzania katika ramani nyingine ya soka duniani, wachezaji wangu walicheza vizuri,” alisema kocha huyo na kuongeza kwamba anaamini kuja kwa Ivory Coast na ushindani walioupata hapa vinaweza kuishawishi Brazili ifikirie kuja kuweka kambi hapa nchini kabla ya kuelekea Afrika Kusini kwenye fainali za Kombe la dunia baadaye Juni.
Aliongeza kwamba ushindani ambao Stars umeonyesha katika mechi hiyo umedhihirisha kwamba sasa hawaihofii timu yoyoye watakayokutana nayo.
“Natarajia kwenda Brazili kwa mapumziko… mechi hii ya Ivory Coast itanisaidia kuwaeleza Brazili jinsi Tanzania ilivyoimarika, wachezaji wangu hawakati tamaa na wanajituma muda wote, ni hatua nzuri,” aliongeza.
Aliwapongeza pia Ivory Coast kwa kuonyesha uzoefu wao na kuishukuru serikali ya Tanzania na wadhamini kwa kufanikisha ziara hiyo ya Ivory Coast.
Ivory Coast imekuja nchini kwa mwaliko wa shirikisho la soka Tanzania (TFF) na kesho wanatarajiwa kucheza mechi nyingine dhidi ya timu ya taifa ya Rwanda kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.