Kocha aliyewapatia Bayern Munich ubingwa wa Ujerumani na Ulaya, Jupp Heynckes anataka kuchukua nafasi ya Jose Mourinho Real Madrid.
Uamuzi wake wa kuachia ngazi Bayern mwishoni mwa msimu huu haumaanishi kwamba anastaafu kazi yake, bali anataka kuachana na Ligi Kuu ya Ujerumani – Bundesliga, na ameonesha nia ya kurejea Real Madrid alikokuwa mwaka 1998.
Heynckes alitangaza kitambo uamuzi wake wa kuachia ngazi Bayern, hivyo wenye klabu wakatafuta mapema mrithi wake, ambaye ni kocha wa zamani wa Barcelona, Pep Guardiola. Mourinho anaondoka Real baada ya msimu usiokuwa na mafanikio, mwenyewe akisema ndio mbaya zaidi maishani mwake.
Kocha Heynckes aliwaongoza Bayern Jumamosi hii kutwaa ubingwa wa Ulaya dimbani Wembley, London, katika mchezo mkali dhidi ya Wajerumani wenzao, Borussia Dortmund, ambapo Bayern waliibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Wakala wa kocha Heynckes, Enrique Reyes amesema kwamba mteja wake angefurahi kurudi Real, lakini akaongeza kwamba suala si la yeye kuamua, bali Rais wa Real, Florentino Perez ambaye pia ndiye alitangaza kuondoka kwa Mourinho.
Heynckes anayefikisha umri wa miaka 68 anazungumza Kihispaniola kizuri, ambapo katika rekodi zake, aliipatia Real ubingwa 1998 na pia amefundisha timu nyingine za La Liga, ambazo ni Athletic Bilbao na Tenerife.
Reyes anasema ni juu ya Rais Perez kutumia njia ya mkato kumchukua mtu wake asiyekuwa na kazi lakini mwenye mafanikio makubwa, badala ya kuendelea kuhangaika kumpata kocha Mtaliano anayewanoa Paris Saint-Germain, Carlo Ancelotti.
Iwapo Heynckes atakwenda Real, utakuwa mzunguko wa aina yake wa makocha, kwani Guardiola anatoka Hispania kwenda Ujerumani, wakati Mourinho akitajwa tajwa kuchukua nafasi ya Rafa Benitez inayobaki tupu Chelsea hivi karibuni, wakati Manuel Pellegrini wa Malaga ameshatangaza kuondoka, akidhaniwa ataziba nafasi ya Mtaliano Roberto Mancini klabuni Manchester City.