Kocha wa zamani wa Borussia Dortmund, Jurgen Klopp amesaini mkataba wa miaka mitatu kuwanoa Liverpool.
Mjerumani huyu anachukua nafasi ya Brendan Rodgers aliyefukuzwa Jumapili iliyopita.
Wamiliki Wamarekani wa Liverpool waliwasiliana na Klopp wakimtaka hadi leo awe amethibitisha kuwafanyia kazi na hatimaye wamekubaliana.
Kulikuwapo habari pia kwamba kocha wa zamani wa Real Madrid na Chelsea, Carlo Ancelotti alikuwa kwenye orodha.
Klopp aling’atuka Dortmund akisema alitaka kupumzika kwa mwaka mmoja, lakini akabainisha alikuwa huru kuingia Anfield, kwa sharti kwamba awe na kauli ya mwisho kwenye usajili.
Klopp atapata pauni milioni tano kwa mwaka, na mshahara huo utaongezeka hadi pauni milioni saba pamoja na bonasi mbalimbali ikiwa watatwaa ubingwa wa England au kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Anatarajiwa kuwasili Anfield pamoja na wasaidizi wapya, Zeljko Buvac na Peter Krawietz – aliokuwa akifanya nao kazi Bundesliga.
Kocha huyu mpya atatakiwa kuwaandaa Liverpool kukabiliana na Tottenham Hotspur Oktoba 17.
Taarifa iliyotolewa na Chama cha Makocha wa Ligi kwa niaba ya Rodgers, 42, ilieleza kwamba kocha huyo amesikitishwa kukatishwa muda wake Anfield, baada ya miaka mitatu unusu tu.
Rodgers ameeleza kufurahishwa kufanya kazi kwenye klabu kubwa, hana haraka ya kutafuta kazi nyingine, na sasa majadiliano yatafanyika juu ya fidia, ambapo huenda Liverpool wakalipa pauni zaidi ya milioni tano.
Makocha wasaidizi, Sean O’Driscoll, Gary McAllister na, Pep Lijnders ndio waliongoza mazoezi uwanjani Melwood Jumanne.
Liverpool walitangza Jumapili iliyopita kumfukuza Rodgers, raia wa Ireland Kaskazini baada ya mwenendo wa timu kuwa si mzuri.
Kuondoka kwa Rodgers kumemfanya kocha wa Arsenal, Arsene Wenger awe mwalimu aliyefanya kazi kwa muda mrefu zaidi katika klabu kuliko makocha wengine wa Ligi Kuu England wakiwekwa kwa pamoja. Rodgers ndiye alikuwa akimfuatia baada ya kuwa Anfield kwa karibu miaka mitatu.