*Ni kwa uungwana katika matumizi ya fedha
SOKA kweli inalipa, hasa England, maana klabu za soka za hapa katika Ligi Kuu zimejikusanyia faida ya pamoja kwa mara ya kwanza katika miaka 16.
Wakati kivuno kinaongezeka kwa kiasi kikubwa sana, kutoka kwenye hasara hadi faida ya pauni milioni 198, takwimu zinaonesha kwamba kasma ya mishahara ya wachezaji inaongezeka kidogo tu.
Mapato haya makubwa yamerekodiwa baada ya mwaka uliotangulia kuelezwa kwamba klabu hizo zilipata hasara ya jumla ya pauni milioni 291.
Hii ni mara ya kwanza kwa klabu za Ligi Kuu England kutengeneza faida hiyo ya pamoja katika kipindi cha miaka 16, na hii inatokana na kanuni za uungwana katika matumizi ya fedha, hasa vigingi kwenye usajili.
Kanuni hizo ziliwekwa kuanzia 2013 zinadhibiti klabu kwenye matumizi ikiwa hazina mapato makubwa, na sasa mishahara ya wachezaji imeongezwa kwa wastani wa 5.5% wakati mapato yamepanda kwa 22%.
Hesabu za klabu husika zinazorejewa hapa ni za klabu 20 za Ligi Kuu England kwa 2013/14, kwani ndizo zimeshachapishwa hadi sasa, kuendana na kanuni za uhasibu na ukaguzi wa hesabu.
Ukienda kwenye klabu moja moja, kwa msimu husika, klabu 15 kati ya 20 zimetengeneza faida, ambapo hata wastani wa zote unazifanya ziwe na faida ya jumla.
Mwaka wa fedha uliotangulia hali ilikuwa tofauti, ambapo klabu 12 kati ya hizo 20 zilitengeneza hasara.
Wakati huo, klabu tano kwa pamoja zilipata hasara ya pauni milioni 50 au zaidi huku ligi hii tajiri zaidi ilishuhudia jumla ya hasara ikifika pauni milioni 291.
Klabu zinaingia kwenye dili kubwa la vituo vya televisheni ambapo pauni bilioni 5.5 zinamwagwa kwa Bodi ya Ligi Kuu kwa miaka mitatu.
Klabu zimejizuia kuongeza mishahara, isipokuwa kwa klabu zilizopanda daraja ambazo ziliruhusiwa ili wachezaji wawe na hadhi ya Ligi Kuu, nazo ni Cardiff City, Crystal Palace na Hull City.
Manchester United waliongeza mishahara kwa pauni milioni 34 au zaidi mwaka huo uliokuwa na misukosuko baada ya kung’atuka kwa kocha wao, Sir Alex Ferguson.
Mapato ya United yalikuwa yamepanda kwa £70m hadi £433m, hivyo kasma yao ya mishahara ikawa £215m, kubwa zaidi katika ligi, lakini bado ilikuwa pungufu ya 50% ya mapato yao.
Mapato ya Manchester City yaliongezeka kwa kiasi kikubwa, kwa sababu ya udhamini kutoka kwa kampuni kadhaa za Abu Dhabi waliko wamiliki wao.
Hata hivyo, bado mapato yao yalikuwa pungufu ya yale ya United kwa pauni milioni 86, kutokana na jinsi United walivyojijenga kwa miaka mingi.
Klabu kadhaa ziliongeza kasma ya mishahara kwa pauni milioni sita tu au hata pungufu.
Mojawapo ni Aston Villa kwa £3m kutoka £72m wakati mmiliki wao Mmarekani Randy Lerner akijitahidi kuweka sawa hesabu ili auze klabu hiyo.
Mmiliki wa Stoke, Peter Coates anafurahia kanuni za uungwana katika matumizi ya fedha, maana wanyonge walikuwa wakinyongwa na wakubwa wakifaidi kusajili watakavyo na kutoa mishahara mikubwa.
Kanuni hizo zinaweka kima cha chini kwa klabu kupata hasara kutokana na matumizi makubwa mno na hii imesaidia klabu kuimarika kifedha.
Wakati klabu nyingine zikichuma fedha na kutumia kununua wachezaji au kuongeza mishahara, klabu kama Arsenal, Everton, Newcastle United, Tottenham Hotspur na Crystal Palace walifanikiwa kuweka benki kiasi kikubwa cha fedha.
Spurs waliopata faida ya pauni milioni 80, ilikuwa ya kwanza katika Ligi Kuu kupata kiasi kikubwa kama hicho.
Wakati Bodi ya Ligi Kuu ikifurahia mabadiliko hayo chanya, wahasibu na wakaguzi wa hesabu Deloitte wanasema ni faida ya kwanza tangu 1997-98.
Kwa ujumla, klabu za Ligi Kuu zilitumia 57.5% ya mapato yao kulipa mishahara likiwa ni punguzo la karibu 10% ikilinganishwa na ilivyokuwa 2012-13.