*Arsenal, Chelsea, Man City nje…..
*Liverpool walioanza msimu huu vibaya kwenye ligi ya nyumbani, walishindwa pia kuhimili mikiki ya Ulaya na walifungasha virago mapema bila chuki.
Ni mwaka wa njaa kwa klabu za England kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL), kwani zote zimetolewa.
Waliofuzu kwa kuwa ngazi za juu kwenye Ligi Kuu ya England (EPL) msimu uliopita walikuwa Manchester City, Liverpool, Chelsea na Arsenal, lakini sasa wametindikiwa.
Man City wamekuwa wa mwisho kutoka, si kwamba wamevuka saa bali kwa sababu ya ratiba yao tu, ambapo wamechapwa na Barcelona 1-0 baada ya kuwa nyuma kwa 2-1 kwenye mechi ya awali.
Hii imekuja siku moja tu baada ya Arsenal kutolewa na Monaco wa Ufaransa. Arsenal walishinda 2-0 Jumanne hii lakini kwa makosa ya mechi ya awali Emirates walikoruhusu kufungwa 3-1 wameng’oka.
Kocha wa Arsenal, Arsene Wenger amesema kwamba haikuwa sahihi kwa Monaco, timu aliyopata kuinoa, kuwatoa huku nahodha Per Metersacker akisema kwamba timu bora imepenya.
Chelsea wenyewe walitolewa na Paris Saint-Germain (PSG) wa Ufaransa kwa faida ya bao la ugenini, kwenye mechi ambayo vijana wa Jose Mourinho walicheza mmoja zaidi baada ya Zlatan Ibrahimovic kutolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kumchezea vibaya Oscar.
Liverpool walioanza msimu huu vibaya kwenye ligi ya nyumbani, walishindwa pia kuhimili mikiki ya Ulaya na walifungasha virago mapema bila chuki.
Katika mechi iliyochezwa Jumatano hii, Barcelona waliwalamba Man City 1-0, kwa bao la Ivan Ractic aliyetiliwa vyema na nyota wa Barca, Lionel Messi na kumhadaa kipa Joe Hart.
City hawakuwa na bahati kwa sababu walikosa penati dakika za mwisho, mpigaji akiwa ni Sergio Aguero. Penati ilitolewa baada ya mshambuliaji huyo matata wa kati kuangushwa na Javier Macherano.
Barca walitawala kwa muda mrefu, ambapo walijaribu mipira 23 ya kugunga langoni mwa Man City lakini kipa Hart alikuwa vyema na wakati mwingine mipira ilikuwa mingi.
Hii ni mara ya nne City wanashindwa kuvuka hatua kama hii, wakiwa ni timu inayoelezwa kuwa na wachezaji wanaolipwa vizuri zaidi duniani, achilia mbali fedha zilizotumika kununua wachezaji husika.
Katika mechi nyingine, Juventus wamewatandika Borussia Dortmund mabao 3-0.