Menu
in , , ,

Klabu EPL hali mbaya

Tanzania Sports

Klabu EPL hali mbaya

Klabu za Ligi Kuu ya England (EPL) zipo katika hali mbaya kiuchumi, imebainika.

Mwekezaji maarufu, Warren Buffet alipata kusema kwamba baada ya maji kupwa ndipo itajulikana nani alikuwa anaoga akiwa uchi.

Na sasa ukubwa wa janga la virusi vya corona vinavyosababisha homa kali ya mapafu vimesababisha kupwa kwa yaliyokuwa yakivifunika klabu za EPL na sasa aibu imeanikwa wazi.

Tangu kuahirishwa kwa mechi za ligi kuu hiyo, pameibuka mijadala mingi ya wazi, lakini ndani kwa ndani klabu zimekuwa zikihangaika kujinasua na hali hiyo mbaya, kwa sababu hakuna mapato tena, huku matumizi yakibaki kuwa makubwa na msimu wa usajili ukikaribia.

Sasa watu wanakumbuka maneno ya Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, David Cameron aliyezoea kuwa na msemo wa maulizo; “je, ulikumbuka kukarabati paa lako wakati mvua ikinyesha?”.

John Purcell – mwasisi mwenza wa kampuni ya uchambuzi wa masuala ya fedha – Vysble, anasema kwamba akaunti za fedha za klabu zipo katika hali mbaya sana. Dk Dan Plumley, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya fedha katika Chuo Kikuu cha Sheffield Hallam, anasema mshituko wa kifedha uliotokana na Covid-19 umeonesha sekta ilivyotandawaa na ni klabu zipi zinaishi kijungujiko.

Crystal Palace na Newcastle United wamechukua unafuu kupitia serikali inayotoa ruhusa ya kuwa na miezi mitatu ya ziada bila kuchapisha taarifa za biashara zao za mwisho wa mwaka, lakini kuna kila dalili kwamba hali yao ni mbaya sana.

Hesabu za msimu wa 2017/18 zinaonesha kwamba mapato ya jumla ya ligi yalikuwa pauni bilioni 4.8, klabu nyingi zikiripoti maongezeko ya mapato, japo kwa viwango vidogo. Mmiliki mwenza wa zamani wa Tottenham Hotspur alisema ni kiasi kidogo mno kilikuwa kinaingia kwenye klabu.

Ni Watford pekee waliokuwa wakipunguza ankara ya mishahara mwaka hata mwaka. Na kwa ujumla inaonekana kwmaba klabu zimekuwa zikitumia zaidi ya asilimia 64 ya mapato yao kwenye mishahara kwa wafanyakazi, zikibaki na faida kidogo sana, lakini zikawa zinaficha.

Kwa wastani Bournemouth, Everton na Leicester zimekuwa zikitumia zaidi ya asilimia 80 ya mapato yao kwa wafanyakazi. Ukweli ni kwamba, zaidi ya nusu ya klabu za EPL zimekuwa zikitumia zaidi ya asilimia 70 ya mapato kwenye mishahara, hali inayoashiria kunyooshwa bendera nyekundu ikimaanisha hali ni mbaya England.

Kwa klabu tatu za Aston Villa, Norwich City na Sheffield United, zimekuwa katika hali mbaya lakini zinajitahidi tu, ikielezwa kwamba hali ni mbaya zaidi kwenye Ligi Daraja la Kwanza – Championship.

Klabu zipo katika sintofahamu kutokana na mengi, huku virusi vya corona vikizuia mapato. Gharama za usafiri, ankara za umeme, gesi, maji, bima, makaratasi na kadhalika zikiwaacha patupu na nyingine zikisonga mbele na kukopa. Kwa sasa nyingi za klabu zipo katika madeni.

Klabu sita tajiri zaidi zinachukua pauni bilioni tatu ambayo ni asilimia 61 hivi ya mapato yote ya ligi. Arsenal walioshuka kidogo wamekuwa wakipata £367.5m kwa msimu wa 2017/18, ikiwa ni £176.8m zaidi ya zile za West Ham. Bournemouth na Aston Villa wanaonesha kuwa na nakisi.

Manchester United, wanalamba kiasi kikubwa zaidi kwenye ligi wakifuatiwa na Manchester City na Liverpool lakini hata sasa wanajiuliza janga hili likiendelea watakuwa katika wakati gani. Klabu nyingi zimeingia katika madeni makubwa na sasa zinaomba tu janga limalizike ili mechi ziendelee, wapate mapato ya mlangoni, mauzo ya bidhaa zao na ya haki za televisheni.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version