*Wapangwa kufanyika Mei 18, wadau wataka uahirishwe
*Kamati ya muda iingie na wapatikane wawaniaji wengi
Chama cha Mpira wa Wavu Tanznaia TAVA kipo katika maandalizi ya mwisho ya mkutano mkuu wa uchaguzi mwishoni mwa wiki hii.
Uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Mkonge mjini Tanga unatarajia kujumuisha wajumbe 60 kutoka mikoa wanachama Tanzania Bara.
Mwenyekiti anayemaliza muda wake, Augustino Israel Agapa amesema wajumbe wanatarajiwa kuanza kuwasili Tanga tangu Alhamisi wiki hii. Uchaguzi utasimamiwa na Baraza la Taifa la Michezo (BMT).
Nafasi zinazogombewa ni pamoja na mwenyekiti , makamu wenyeviti wawili , katibu mkuu na msaidizi wake pamoja na wajumbe wanane wa kuongoza vitengo mbalimbali kama Beach Volleyball, Ufundi, Coaches, Wanawake, School Programs na Vijana.
Hata hivyo, habari zisizothibitika zinasema kuna wadau wanataka mkutano huo usifanye uchaguzi na badala yake kamati ya muda iundwe. Wadau hao wanadai kuwa uongozi wa kamati iliyopo madarakani umeshamaliza muda wake, hivyo basi haistahili kuongoza kwa sasa.
Katiba ya TAVA haioneshi uwezo wa wadau, kwani wanachama wake ni vyama vya mikoa, na haya ndiyo mapungufu ya katiba nyingi za vyama vya michezo Tanzania.
Kwa uzoefu nilio nao katika uongozi wa TAVA (niliwahi kuwa katibu mkuu msaidizi na mwenyekiti wa kamati ya ufundi) naamini uamuzi wa kusimamisha mkutano mkuu wa TAVA utakuwa na maslahi kwa mchezo huo kuliko kuufanya, huku idadi ya waombaji uongozi ikiwa ndogo. Kadhalika, uongozi wa sasa umeshapitisha kipindi chake.
Lakini uamuzi wa mwisho ni wa BMT, kwani ndio wasimamizi wa mkutano wa uchaguzi kama katiba yao inavyosema. Jana nilizungumza kwa simu na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Leonard Thadeo, ambaye alikiri kwamba BMT inaangalia kwa makini mchakato huo, ili kuchukua uamuzi kwa maslahi ya taifa, hususan wadau wa mchezo huu mzuri nchini Tanzania.