Msimu jana ulikuwa msimu wa kwanza kwa kocha Antonio Conte akiwa
Chelsea. Pamoja na kwamba ulikuwa msimu wake wa kwanza akiwa kama
kocha wa Chelsea, na msimu wa kwanza kwake akiwa kwenye nchi ya
England lakini alifanikiwa kuchukua ubingwa wa ligi kuu ya England.
Antonio Conte aliikuta Chelsea ikiwa imefanya vibaya msimu mmoja kabla
ya kuja yeye.
Lakini alifanikiwa kufanya vizuri, na timu yake kuchukua ubingwa wa ligi kuu.
Lakini msimu huu imekuwa tofauti na msimu jana, mpaka sasa iko nafasi
ya tatu kwenye msimu wa ligi kuu ya England.
Na jana tumeshuhudia ikitolewa katika michuano ya kombe la ligi ( EFL)
Katika hatua ya nusu fainali na Arsenal.
Kipi kinafanya Chelsea iwe na mwenendo wa kusuasua msimu huu tofauti
na msimu jana ??
Chelsea ni timu ya mtu mmoja, mtu huyu akiwa hayupo Chelsea huyumba na
wakati mwingine hata akiwepo na asipocheza vizuri timu nayo hucheza
vibaya na kuhangaika kupata matokeo.
Pamoja na kwamba Hazard amekuwa tegemeo kubwa kwa misimu mingi pale
Chelsea ila msimu huu amekuwa tegemeo kubwa sana kutokana na wenzake
wanaomzunguka kuwa katika viwango visivyo bora.
Willian na Pedro wamekuwa wakitumika kama suluhisho kipindi ambacho
Hazard akiwa hayuko katika kiwango kizuri.
Msimu huu imekuwa tofauti, Willian na Pedro wameshuka kiwango na hii
inakuwa inaipa shida Chelsea inapokuwa haina Hazard au Hazard akiwa
hayuko vizuri anakosekana mtu wa kuyaziba madhaifu yake.
Vipi usajili wa Antonio Conte katika dirisha la majira ya joto
lililopita ulikuwa na faida kwenye timu ?
Mpaka sasa hakuna kitu kikubwa alichonufaika nacho kutoka kwa
wachezaji aliowaleta msimu huu.
Wachezaji wote waliokuja msimu huu katika timu ya Chelsea hawajazoea
ligi hali ambayo inawafanya wasitoe mchango mkubwa wa moja kwa moja
kwenye timu.
Pamoja na kwamba Morata mpaka sasa ameshafanikiwa kufikisha magoli 12
lakini anakosa hali ya kuibeba timu wakati mgumu.
Na hii inachangia kwa kiasi kikubwa na ugeni wa ligi, kama ilivyo kwa
wenzake kina Zappacosta na Rudiger.
Kama Alvaro Morata anakosa uwezo mkubwa wa kuibeba timu nyakati ngumu
na alisajiliwa kwa ajili ya kuziba pengo la Diego Costa , ndiyo ina
maanisha hakuwa mtu sahihi wa kuziba pengo la Diego Costa?
Kuna ukweli kwenye hili swali, kwa sababu Diego Costa ni mpambanaji
zaidi ya Alvaro Morata, alikuwa anapambana hata wakati ambao Chelsea
ilikuwa inaonekana imeshikwa lakini alikuwa na uwezo wa kuiokoa
Chelsea katika nyakati ngumu hii ni tofauti na kwa Alvaro Morata.
Msimu jana tulimuona Antonio Conte akija na mfumo wa 3-4-3 na
kufanikiwa kuchukua ubingwa , vipi msimu huu kwanini imekuwa ngumu
kwake kutumia mfumo huu na kuendelea kuwa tishio kwa wapinzani wake?
Baada ya kufungwa goli 3-0 na Arsenal msimu jana Antonio Conte aliamua
kubadili mfumo kutoka mfumo wa kutumia mabeki wanne mpaka mfumo wa
kutumia mabeki watatu
Timu iliimarika mpaka timu ikashinda michezo 12 mfululizo ikawa rekodi ya klabu.
Msimu huu imekuwa tofauti na msimu jana, msimu huu amebadilika kutoka
katika mfumo wa 3-4-3 mpaka katika mfumo wa 3-5-2 ili aweze
kuwachezesha kwa pamoja Kante, Bakayoko na Fabregas katika eneo la
katikati mwa uwanja.
Mfumo wake huu umekuwa na changamoto tatu.
Changamoto ya kwanza , ni aina ya wachezaji ambao alikuwa nao msimu
jana na msimu huu ni tofauti.
Kwa sababu msimu jana eneo la katikati walikuwa na Kante pamoja na Matic.
Matic alicheza kama box to box middfielder, ambapo alijitahidi kuleta
uwiano mzuri wa kushambulia na kuzuia , alimaliza msimu akiwa na pasi
saba (7) za mwisho za magoli.
Msimu huu imekuwa tofauti Bakayoko pamoja na kwamba amekuwa akifanya
vizuri timu inapokuwa inazuia lakini timu ikiwa inashambulia amekuwa
akifanya vibaya kwa kukosa nafasi nyingi za wazi pia siyo mbunifu wa
kutoa pasi za mwisho za magoli.
Tatizo la pili ni wachezaji wa mbele kushuka viwango tofauti na msimu
jana. Pedro na Willian msimu jana walikuwa msaada mkubwa sana katika
mfumo huu lakini msimu huu imekuwa tofauti.
Tatizo la tatu, makocha wengi wameshajua mbinu za kupambana na mfumo
wa kutumia mabeki watatu, ndiyo maana hata wenyewe wameanza kuutumia
mfumo huu.
Antonio Conte amekuwa akilalamika kuwa kikosi chake kinakumbwa na
uchovu , hii inaweza ikawa na ukweli ndani yake ?
Ndiyo, msimu jana Chelsea alikuwa na michuano michache, alitoka mapema
EFL, akabaki na FA Cup pamoja na Ligi kuu ambapo FA Cup nayo hakufika
mbali.
Hivo EPL lilikuwa kombe pekee alilowekeza nguvu kubwa.
Msimu huu ana michuano mingi ambayo amewekeza nguvu kubwa kwa kikosi
hicho hicho, kikosi anachokitumia ligi kuu ya England ndicho hicho
hicho anachokitumia EFL, FA Cups na ligi ya mabingwa barani ulaya.
Hivo kwa ufinyu huu wa kikosi unawafanya wachezaji wapate uchovu,
mchezaji akipata uchovu kasi yake ya kupigana hupungua kwa kiasi
kikubwa.