Menu
in

Kina Ajib hawaoni wivu kwa kina Chama ?

Tanzania Sports

Simba SC iliwahi kufika robo fainali ya ligi ya mabingwa barani Afrika mwaka 2003. Kipindi hicho waliingia robo fainali kiume kweli kweli tena kiume haswaa.

Kitendo cha kuifunga Zamaleki tena kwenye ardhi ya Misri, ardhi ambayo siyo nyepesi hasa kwa timu ambazo zinatoka kwenye ukanda wetu.

Ukanda wetu haujaendelea sana kisoka ukilinganisha na ukanda ambao Zamaleki ipo. Pia timu za kiarabu zinasifika sana kwa mbinu chafu za nje ya uwanja.

Mara nyingi mbinu chafu huwa zinawadhoofisha wageni wanaotembelea nchi za kiarabu na kujikuta wanapoteza mchezo kirahisi tu. Lakini hii ilikuwa tofauti na Simba SC ya mwaka 2003.

Kwenye ile ile ardhi ya vipaji vikubwa tena mbele ya timu kubwa barani Afrika, timu yenye wachezaji bora. Kwenye ardhi ile ile ya figisu nje ya uwanja lakini Simba SC waliwatoa Zamaleki kwenye mashindano ya ligi ya mabingwa barani Afrika.

Ndiyo maana narudia kusema kuwa Simba SC waliingia robo fainali ya ligi ya mabingwa barani Afrika kiume tena kiume haswaa. Walipigana ndani na nje ya uwanja kuhakikisha wanafanikiwa kuingia robo fainali ya ligi ya mabingwa barani Afrika.

Ukitazama kikosi ambacho kilifanikiwa kufika robo fainali ya ligi ya mabingwa barani mwaka huo wa 2003 asilimia kubwa ya wachezaji walikuwa wachezaji wa kitanzania. Mchezaji pekee ambaye alikuwa wa kigeni ni Ramadhani Wasso kutoka Burundi.

Beki huyu wa kushoto ndiye alikuwa beki pekee ambaye alikuwa mchezaji wa kigeni ndani ya kikosi cha Simba SC kilichoiua miamba ya soka barani Afrika, Zamaleki na kufanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya ligi ya mabingwa barani Afrika.

Juma Kaseja ndiye alikuwa golikipa ambaye alikuwa anailinda milingoti mitatu na anakumbukwa kwa uhodari wake wa kuchomoa michomo ya penalti hasa kwenye mechi dhidi ya Zamaleki.

Beki namba mbili alikuwa ni Said Sued, huyu alikuwa Mtanzania. Beki namba tatu alikuwa Ramadhani Wasso kutoka Burundi wakati mabeki wa kati walikuwa Watanzania Boniface Pawasa na Victor Costa “Nyumba”.

Hawa ndiyo walikuwa mabeki katili ambao walikuwa imara muda mwingi mwa mchezo kuhakikisha Simba SC wanafika katika hatua ngumu ya robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika mwaka 2003.

Mabeki hawa walikuwa wanalindwa na kiungo wa ukabaji ambaye kwa sasa ni kocha msaidizi wa Simba SC, Suleiman Matola , tukumbuke bandage Suleiman Matola alienda Afrika Kusini kucheza soka la kulipwa chini ya timu ya Super Sport.

Suleiman Matola alikuwa anacheza na Christopher Alex kwenye eneo la kati la Simba SC. Upande wa mshambuliaji aliyekuwa anatokea pembeni kulia aliyekuwa anacheza ni Yusuph Macho.

Wakati Yusuph Macho akicheza upande wa kulia, upande wa kushoto mtu aliyekuwa anacheza ni Ulimboka Mwakingwe na yeye pia alikuwa mchezaji kutoka Tanzania.

Simba SC walikuwa wanaongozwa na washambuliaji wawili, Athuman Machupa na Emmanuel Gabriel. Hawa ndiyo walikuwa wamebeba dhamana ya kuchana nyavu za wapinzani.

Ukitazama asilimia kubwa ya wachezaji waliocheza kikosi cha kwanza walikuwa Watanzania. Tangu mwaka 2003 mpaka leo mwaka 2021, miaka 18 imepita Simba SC inazidi kufanya vyema kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika.

Lakini pamoja na kufanya vyema asilimia kubwa ya wachezaji wanaopata nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Simba SC ni wachezaji wa kigeni na siyo wachezaji kutoka Tanzania.

Hili jambo ni la kufikirisha sana. Je Simba SC wameacha kutafuta wachezaji wenye vipaji vikubwa ndani ya nchi? Au tatizo lipo kwa wachezaji wa Tanzania ?

Inawezekana kina Ibrahim Ajib hawaoni wivu kwa kina Claoutus Chota Chama? Hawapigani vya kutosha ili waweze kupata nafasi ndani ya kikosi cha kwanza cha Simba SC?

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya martinkiyumbi@gmail.com

Leave a Reply

Exit mobile version