Menu
in , , ,

KILICHOWATOA PSG KLABU BINGWA ULAYA

Tanzania Sports

Wanasema mtoto yake nepi na kweli kwa mara nyingine tena Real Madrid wametuonesha hicho tu na kiukweli kabisa PSG bado wanakosa vitu vingi sana kuwaona wakifanya vizuri kwenye michuano hii lakini yafuatayo yamesababisha wao kushindwa kuvuka hatua inayofuata.

UBORA WA REAL MADRID KWENYE MICHUANO HIYO.

Utasema yote lakini ni ukweli usiopingika kuwa Real Madrid inabaki kuwa moja ya timu tishio na zenye kupewa nafasi kubwa zaidi ya kufanya vizuri kwenye michuano hiyo hata wawe na msimu mbaya vipi kwenye ligi ya ndani lakini linapokuja swala la UEFA champions league Real Madrid huwa ni moto wa kuotea mbali. Wametinga hatua ya robo fainali mara ya 8 mfululizo na ni Barcelona pekee ndio wamefanya hivyo zaidi ambayo ni rekodi (10) hivyo ni wazi PSG walikuwa na uwezo mdogo wa kulidhibiti hilo.

UNAI EMERY.

Hii inaweza kuwa ni mara ya pili mfululizo kwa PSG kushindwa kuvuka hatua ya 16 bora lakini kimsingi mwalimu Unai Emery haijui robo fainali ikoje kabisa kwenye maisha yake. Hajawahi kuvuka hatua hii kwenye majaribio yake 5 aliyowahi kufanya mpaka sasa. Amekosa mbinu thabiti za kuweza kuvuka hatua hiyo na kiukweli aliifanya kazi iwe nyepesi kabisa kwa Zinedine Zidane kuweza kumdhibiti hapo.

UZOEFU.

PSG wanaweza kuwa wamewekeza lakini ukweli ni kwamba utu uzima dawa. Real Madrid wana uzoefu mkubwa na michuano hii na ni wazi hichi ni kitu ambacho kimewapa faida mbele ya PSG ambao kimsingi hawana uzoefu mkubwa na mashindano haya. Hivo ni wazi Madrid wana mbinu zote na mikakati bora ya kufanya vizuri kuliko wapinzani. Uzoefu umewabeba Real. Wanaweza kuwa wamekata moto kwenye ligi lakini huku njia zote wanazijua kama Panya.

LIGI YA UFARANSA.

Ligi ya Ufaransa mimi naweza kusema kwamba haiwajengi PSG bali inawaharibu. Kwanini nasema hivi? Ligi yao ya ndani inawadanganya kuwa uwezo ule wanaweza wakauhamishia hata katika usiku wa Ulaya na wakafanya na vizuri jambo ambalo sio la kweli. PSG bado hawana wachezaji wengi wa kiwango cha dunia lakini matokeo mazuri kwenye ligi yanawafanya wasiwekeze zaidi kwa ajili ya klabu bingwa. Mchezaji wa kiwango cha Dunia kwenye kikosi chao kwa sasa ni Neymar tu na hatoshi. Kumtegemea yeye tu ni kumpa mzigo asiouweza. Ili waweze kufanya vizuri wanahitaji wachezaji wenye kaliba ya Neymar kama watano kwenye nafasi nyingine uwanjani ili waweze kuwa washindani halisi na huku Ulaya.

KUKOSA MALENGO.

Unajua mtoto ndio huwa anakosa malengo lakini mtu mzima huwa anafanya vitu kwa malengo. PSG utoto umewatoa mara hii kabla hata mechi ya marudiano. Kwa jinsi walivyocheza kule Santiago Bernabeu ni kama vile hawakuwa wanajua timu ina malengo gani. Walicheza kama watoto ambao kimsingi hawaangalii mbele. Timu ilikuwa na mpasuko mkubwa na hakukuwa na umoja wowote. Kila mtu pale mbele alicheza kivyake na hili kiukweli limewagharimu pakubwa kwenye michuano hii. Dani Alves alikuwa haridhiki mpaka ampe Neymar ambaye ni mbrazili mwenzie hata pale ambapo Cavani angeweza kufunga, Neymar nae akawa anacheza na majukwaa badala ya kuichezea timu yake na huku kwingine kukawa na timu Cavani na timu Mbappe. Yani ilimradi kila mtu alicheza kivyake uwanjani na wakawa kama watoto tu. Wakaifanya kazi iwe nyepesi kwa Real Madrid.

Written by haatimabdul

Exit mobile version