Menu
in

Kikwete ataka TFF kuweka fedha za kuwalipa makocha

RAIS Jakaya Kikwete amewapasha viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania, TFF kuwa wasikae na kujisahau na waanze mikakati ya kutafuta fedha kwa ajili ya kulipa makocha watakaokuwa wakitumika kuzinoa timu za taifa.

Akihutubia Wabunge mjini Dodoma, Kikwete amesema yeye kama Rais alikubali kumlipa kocha ikiwa ni mwanzo wa kuendeleza soka lakini kwa fedha wanazopata TFF, waanze kuweka kwa ajili ya makocha.

Kikwete amesema serikali imekuwa ikipanga mishahara ya watumishi wake lakini katika mishahara ya watumishi hao wa umma, mshahara wa kocha haupo.

“TFF wasigeuze ufadhili wangu kuwa wa milele, suala la kuajiri kocha si kazi ya serikali. Hii ni taasisi huru inaweza kufanya mambo yake kwa kujitegemea bila kuingiliwa na mtu.

“Fedha wanazopata, waanze kutengeneza fungu la makocha, wasile zote,” amesema Kikwete na kusisitiza: “Katika mpango wa ajira za serikali, mshahara wa kocha wala kocha hayumo.”

Inawezekana hatua ya Kikwete imekuja baada ya TFF kuwa katika udhamini mzito wa Kampuni ya Serengeti Breweries, SBL ambao wameingia mkataba wa Sh2.1bil. kwa miaka mitatu pamoja na udhamini wa Benki ya NMB ambao hudhamini Taifa Stars, TFF na timu za vijana.

Kikwete amesema kuwa azma yake na serikali kwa ujumla ni kuona michezo inapiga hatua na hasa soka na ndiyo maana akachukua jukumu la kuajiri na kumlipa kocha kwa ajili ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.

Amesema kuwa kutokana na hali hiyo, aliamua kumleta kocha, Marcio Maximo kwa ajili ya soka Tanzania na sasa Tanzania imepiga hatua katika mchezo huo. “Nimeleta kocha na nikakubali kumlipa, nai sasa Tanzania inafanya vizuri katika medani ya soka.

“Tanzania si kichwa cha mwendawazimu tena, sasa hivi Tanzania ni kinyozi…nina hakika katika mashindano mengine yajayo, Cameroon watajiuliza wakipangwa na Tanzania na naamini wataomba wasipangwe na Tanzania.

Rais Kikwete pia alitolea mfano wa mechi ya Tanzania na Ghana. “Hata katika mchezo wa Ghana, tumeona mambo yalikuwa magumu kwa Ghana na hadi kipa kaenda kusawazisha bao,” alisema.

Katika kuenda sanjari na kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa, FIFA, Taifa Stars ilicheza na Ghana mchezo wa Kirafiki kwenye Uwanja Mkuu wa Taifa na kutoka sare ya 1-1.

Bao la Taifa Stars lilifungwa na Henry Joseph kwa kichwa wakati bao la Ghana lilipatikana dakika sita kabla ya mchezo kumalizika likifungwa na Richard Kingston.

Rais Kikwete pia alisema baada ya kumaliza ya soka, atageukia kwenye riadha.

“Nataka tukae na viongozi wa riadha, tuzungumze nini matatizo katika mchezo huu. Mimi niko tayari kusaidia kuendeleza maeneo ya kiufundi katika michezo suala la malumbano mimi halinihusu, hilo ni juu yao wenyewe,” alisema.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version