Shirikisho la mpira wa kikapu nchini, TBF, limeuangukia uongozi wa klabu ya mchezo huo ya Pazi kwa kuiandikia barua ya kuomba radhi kwa kushindwa kuwapa taarifa mapema juu ya ushiriki wao wa michuano ya Ligi ya Taifa iliyoendelea jijini Dar es Salaam, jambo lililoifanya timu hiyo iwe nje ya michuano hiyo.
Aidha, TBF imesisitiza kuwa klabu ya Pazi haijajitoa kwenye michuano hiyo kama ilivyokuwa ikiripotiwa, bali imeshindwa kushiriki kwa kucheleweshewa taarifa juu ya michuano hiyo.
Katibu Msaidizi wa TBF na Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano hayo, Michael Maluwe, aliiambia Nipashe jana kuwa, shirikisho lao limeamua kuiandikia barua ya kuiomba radhi klabu ya Pazi kutokana kushindwa kuwapa taarifa mapema juu ya michuano hiyo ya Taifa.
Maluwe alisema kutokana na kucheleweshewa taarifa, Pazi wameshindwa kushiriki ligi hiyo na hivyo wameona vyema kuwataka radhi.
Katibu huyo alisema kuwa awali, TBF walidhani kwamba kila mkoa ungewakilishwa na timu moja na pale walipobaini zinahitajiwa timu mbili-mbili, walilazimika kuwataarifu Pazi licha ya kusaliwa na saa chache kabla ya kuanza kwa ligi na ndipo, klabu hiyo iliposema hawakuwa na barua.
“Tulichelewa kuwataarifu na hivyo kuwafanya washindwe kushiriki kama washindi wa pili wa ligi ya mkoa wa Dar es Salaam na kwa kubaini uzembe huo tumelazimika kuwaandikia barua ya kuwaomba radhi, pia ifahamike wazi timu hiyo haijajitoa,” alisema Maluwe.
Alisema barua yao ya kuiomba radhi Pazi imeandikwa Aprili 10 kwa kumb. namba TBF/LTR/NBL 03, kuthibitisha kukiri kosa lililojitokeza na kukanusha kwamba wameifanyia makusudi klabu hiyo, ili isishiriki kuipa nafasi Oilers.
“Sio kweli kama tumeinyima fursa Pazi ili kuibeba Oilers, bali baada ya kuambiwa na Pazi kwamba wasingeweza kushiriki kwa kuchelewa kupata taarifa, tuliwasiliana na washindi hao watatu ambao walikubali kushiriki ligi hiyo, tunapenda tueleweke hivyo,” alisema Maluwe.
Maluwe aliamua kutoa ufafanuzi huo baada ya kuwepo kwa malalamiko toka klabu ya Pazi kwamba, TBF, iliwafanyia makusudi kutowapa taarifa mapema ili kuipa nafasi Oilers ambayo imeungana na Savio kuiwakilisha Dar es Salaam kwenye ligi hiyo.
Naye kocha mkuu wa Pazi, Ramadhani Kalema, alisema jana kuwa wamepanga kukutana na viongozi wote wa klabu hiyo kwa ajili ya kutoa msimamo wao kuhusu kunyimwa nafasi ya kucheza michuano hiyo.
Awali ilidaiwa kuwa TBF ilichelewesha kuwataarifu Pazi, kwa kuwapigia simu saa 2:00 ya kuwataarifu kuwa michuano inaanza kesho yake.