*Vieira, Ancelotti, Benitez wafikiriwa City
*Fununu zaidi za wachezaji kuhama zatoka
Kocha wa Manchester City, Manuel Pellegrini anatarajiwa kufukuzwa kazi iwapo watamaliza ligi nje ya nafasi nne za juu.
Zipo habari pia kwamba wamiliki wa klabu hiyo wanafikiria anaweza kufukuzwa hata kabla ya mwisho wa msimu kutokaa na mwenendo mbaya wa timu hiyo.
City walipoteza mechi muhimu dhidi ya mahasimu wao, Manchester United na kuwafanya wabakie na alama zao 61 katika nafasi ya nne huku vinara Chelsea wakiwa nazo 73 na wana mchezo mmoja mkononi.
City ambao ndio mabingwa watetezi wanadaiwa wanaweza kumpa nafasi hiyo mchezaji wao wa zamani na Arsenal, Patrick Vieira anayeheshimiwa sana klabuni hapo.
Mwingine anayetajwa kuweza kuchukua nafasi hiyo ni Kocha wa Napoli ya Italia aliyepata mafanikio Liverpool miaka iliyopita, Rafa Benitez.
Jina la Kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti nalo linatajwa tajwa, ikizingatiwa kwamba hivi karibuni alisema hana uhakika wa nafasi yake Santiago Bernabeu.
Hata hivyo, kocha wa zamani wa City na Timu ya Taifa ya Vijana ya England, Stuart Pearce anaamini kwamba itakuwa makosa kumfukuza kazi Pellegrini.
City pia wanadaiwa kutaka kuondosha wachezaji sita ili kusajili vijana zaidi kwa ajili ya kuimaisha kikosi hicho. Wanaotajwa kwamba wataingia City ni pamoja na kiungo mshambuliaji wa Kevin De Bruyne (22).
De Briyne anayechezea Wolfsburg ya Ujerumani amepata kukipiga Chelsea. Mwingine wanayemuwinda ni kiungo wa Juventus ya Italia, Paul Pogba.
Kwa upande wa beki, wanataka kumsajili beki wa kushoto wa Tottenham Hotspur, Danny Rose (24) anayefanya vyema msimu huu.
Inaelezwa kwamba beki wao, Aleksandar Kolarov (29) anaweza kuuzwa ama Roma au Inter Milan.
Nao Manchester United wanapewa nafasi kubwa kumsajili mshambuliaji wa Burnley, Danny Ings (22) na tayari mazungumzo na klabu hiyo yameanza.
Lazio ya Italia wanatarajia kuwazidi kete West Ham, Liverpool na Spurs katika kutaka kumsajili mshambuliaji wa Manchester United, Javier Hernandez (26) aliye kwa mkopo Real Madrid.
Hata hivyo, raia huyo wa Mexico anadaiwa kutaka kurudi England kucheza badala ya taifa jingine lolote la Ulaya.
Beki wa kulia wa Southampton, Nathaniel Clyne (24) huenda hatimaye akahama kiangazi hiki kwani amesikika akisema anafurahia kutajwa tajwa kwamba anawaniwa na klabu kubwa kama Manchester United na Chelsea.
Kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti amesema hana mpango wa kumuuza kipa wake namba moja, Iker Casillas hivyo kuwapa United matumaini ya kubaki na kipa wao David de Gea (24) anayesuasua kusaini mkataba mpya.
Barcelona wanataka kumsajili beki wa Torino ya Italia, Matteo Darmian (25) kuchukua nafasi ya Dani Alves (31) anayemaliza mkataba wake na hanuii kuuhuisha tena.
Mshambuliajiw a Chelsea, Didier Drogba (37) amesema anataka kucheza tena mwaka mmoja, licha ya kwamba hajafunga bao hata moja tangu Desemba mwaka jana.
Anatarajiwa kuanza mazungumzo karibuni, ikiwa ni pamoja na dili jipya la kuwa balozi wa klabu hiyo.