*Chelsea na Higuain Bilic kocha mpya West Ham
*Alves abaki Barcelona, Carver ‘out’ Newcastle
Mabingwa wa Italia, Juventus wamemsajili kiungo mahiri wa Real Madrid na Ujerumani, Sami Khedira ambaye ni mchezaji huru.
Khedira (28) alipata kuhusishwa na Arsenal na Chelsea misimu miwili iliyopita, lakini imeelekea kwamba klabu hizo za London hazikumhitaji tena. Manchester United nao walihusishwa naye.
Yawezekana pia kwamba zimezidiwa kete na Wataliano waliofika fainali ya Klabu Bingwa Ulaya msimu huu na kufungwa na Barcelona wikiendi iliyopita.
Kiungo huyo amesaini mkataba wa miaka minne na Bibi Kizee wa Torino, kama wanavyojulikana Juventus.
Khedira alicheza mechi 54 kwa klabu ya Real Madrid na alikuwa katika kikosi cha Ujerumani kilichotwaa ubingwa wa dunia kwa kuwafunga Argentina kwenye fainali mwaka huu nchini Brazil.
West Ham wamemtangaza mlinzi wao wa zamani, Slaven Bilic kuwa kocha wao mpya kuchukua nafasi ya Sam Allardyce.
Bilic (46) amesaini mkataba wa miaka mitatu, akisema kwamba amerejea nyumbani alikojihisi vyema kucheza na anaamini atapata ushirikiano mzuri.
Alicheza mechi 54 kwa timu hiyo ya Upton Park kati ya 1996 na 1997 na amekuwa kocha wa Timu ya Taifa ya Croatia kwa muda wa miaka sita, ambapo amefanikiwa kuwafunga England mara mbili kwenye mechi za kufuzu kwa Euro 2008.
Ni kocha mkubwa aliyepata pia kuwafundisha Lokomotiv Moscow na Besiktas alikotangaza kuondoka Mei mwaka huu, na tetesi zikawa kwamba angerejea West Ham.
Kocha wa zamani wa Tottenham Hotspur na Queen Park Rangers (QPR), Harry Redknapp alikuwa akitajwa tajwa angeteuliwa kushika hatamu hapo na msaidizi wake angekuwa Rio Ferdinand aliyecheza QPR msimu uliopita.
Kocha wa muda wa Newcastle, John Carver amefukuzwa kazi sambamba na mkufunzi wa kikosi cha kwanza, Steve Stone.
Carver (50) aliwaongoza Newcastle kwenye mechi 20 za mwisho wa msimu huu baada ya kocha wa zamani, Alan Pardew kuondoka na kujiunga na Crystal Palace lakini walishinda mechi tatu tu.
Kocha wa zamani wa England na Derby County, Steve McClaren anatajwa tajwa kwamba atateuliwa kuchukua nafasi hiyo baadaye wiki hii.
Beki mkongwe wa kulia wa Barcelona, Dani Alves (32) ameghairi kuondoka klabuni hapa na kusaini mkataba mpya wa miaka miwili Camp Nou.
Raia huyo wa Brazil alikuwa anatarajiwa ajiunge na ama Roma au Manchester United lakini hatimaye akasema kwamba ameamua kufanya kile moyo unachomtuma na kile wanaompenda wanachotaka.
Alves amekaa Barca kwa miaka saba na wikiendi iliyopita alikuwa mmoja wa wachezaji walioshinda ubingwa wa Ulaya dhidi ya Juve.
Wakati hayo yakijiri, Juventus wanaandaa pauni milioni 10 kwa ajili ya kumnasa mshambuliaji wa kati wa Man United, Robin van Persie (31).
Van Persie anasema kwamba anachotaka ni kucheza mpira na si kukaa benchi, baada ya kuwa na msimu mbaya kabisa Old Trafford kwa maana ya kiwango na majeraha.
Chelsea wanaandaa pauni milioni 30 ili kumsajili mpachika mabao wa Napoli, Gonzalo Higuain (27).
Wanamchukua kwa hadhari maana mfungaji wao mkubwa, Diego Costa hukabiliwa na majeraha na pia majuzi amekaririwa akisema ana hamu ya kurudi kwao. Didier Drogba ameondoa na Loic Remy anapenda kupata muda zaidi wa kucheza, hivyo anaweza kuondoka.
Arsenal wanapanga kumsajili mshambuliaji wa Porto, Jackson Martinez (28) ikiwa watafanikiwa kumuuza au kumtoa kwa mkopo Mjerumani Lukas Podolski.
Kocha Arsene Wenger pia anaelezwa kuwa na nia ya kumsajili kiungo wa Sevilla na raia wa Poland, Grzegorz Krychowiak (25) ambaye mkataba wake unaweka kiwango cha pauni milioni 21 ili kumwachia.
Kipa wa Chelsea, Petr Cech (33) amewapa matumaini mapya Arsenal baada ya kusema kwamba angependa kubaki jijini London iwapo ataondoka Stamford Bridge kiangazi hiki.
Newcastle wanataka kumsajili kiungo wa Chelsea, Marco van Ginkel (22) kwa mkopo na pia wanataka kumsajili mshambuliaji wa The Blues hao, Patrick Bamford (21). Chelsea wanataka pauni milioni 10 ili wamuuze Bamfordambaye msimu uliopita alicheza kwa mkopo klabuni Middlesbrough.
Mlinzi wa zamani wa Liverpool, Sami Hyypia (41) anasema kwamba angependa kujiunga na benchi la ufundi Anfield chini ya kocha Brendan Rodgers.
Hata hivyo, zipo habari kwamba kocha msaidizi wa zamani wa Manchester United na Fulham, Rene Meulensteen (51) anapewa nafasi kubwa zaidi hapo Anfield.