*Kilimanjaro Stars, Chipolopolo wapigwa
Nusu fainali ya Kombe la Chalenji kwa Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) imekuwa ya mvutano mkubwa.
Wakati awali Sudan na Zambia walikwenda suluhu hadi dakika 90 za kawaida, walitoshana nguvu pia katika dakika 15 za ziada.
Hata hivyo, Zambia walivunja kigingi baada ya kupata bao dakika ya 19 ya muda wa nyongeza kupitia kwa Ronald Kampamba aliyewahadaa mabeki na kumchambua kipa Abdulrahman Ali.
Wazambia ambao ni washiriki waalikwa, waliona kana kwamba walishavuka kwa bao hilo, wakamtoa mfungaji huyo dakika chache baadaye.
Hata hivyo, Sudan walisawazisha katika dakika ya 24 kupitia kwa Niez Abraham na dakika mbili kabla ya kipenga cha mwisho Sallah Ibrahim aliandika bao la pili na la ushindi.
Mechi ilipomalizika, wachezaji wa Zambia hawakuwa na la kufanya zaidi ya kulia, huku wa Sudan wakijipongeza. Kwa ujumla ilikuwa mechi iliyokuwa na kosakosa nyingi katika muda wa kawaida na haikutarajiwa kabisa kwamba mabao yangepatikana kwenye muda wa ziada.
Katika nusu fainali ya pili ambayo awali ilikuwa ichezwe Machakos ambako uwanja ulijaa maji, Kilimanjaro Stars walilala, baada ya mechi kuahirishwa mara kadhaa na kwenda kuchezwa Uwanja wa Nyayo, Nairobi.
Bado mechi hiyo ilichezwa kukiwa na hali ya mvua na bao la mapema la Harambee Stars lilitosha kuwasukuma kando Stars ambao watatafuta mshindi wa tatu kwa kucheza na Zambia.
Hiyo imekuwa faraja kubwa kwa Wakenya, kwa sababu fainali inafanyika katika maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru wao Alhamisi, na ingekuwa pigo kubwa kutokuwapo kwenye fainali.
Bao la Kenya lilifungwa na Clifton Miheso wa klabu ya Thika United baada ya kupata pasi ya Alan Wanga, ambapo kipa wa Stars anayecheza Gor Mahia, Ivo Mapunda hakuwa na uwezo wa kuizuia.