Menu
in , ,

Kenya kidedea

 

*Wametwaa medali 16 riadha jijini Beijing

 

*Jamaica, Marekani, Uingereza wafuata

 

*Tanzania hawapo popote, Uganda moja

 

Kenya imesafisha jina lake kimataifa katika riadha, baada ya kuibuka kidedea kwenye michuano ya Ubingwa wa Dunia 2015 jijini Beijing, China yaliyomalizika Jumapili hii.

 

Wanariadha wa Kenya walijikusanyia jumla ya medali 16, kati ya hizo saba za dhahabu, sita za fedha na tatu za shaba. Kilikuwa kishindo kikubwa kwenye michuano hiyo, kwa Kenya kuifunika dunia ya riadha.

 

Alikuwa ni Asbel Kiprop aliyehitimisha karamu ya medali alipopata ushindi wa tatu mfululizo, huu wa mwisho ukiwa ni kwenye mbio za mita 1,500 kwa wanaume, akiacha watu 80,000 waliokuwa kwenye Bird’s Nest Stadium kutoa heshima kwao.

 

Alikuwa mwisho kabisa wakati kengele ikilia, na taratibu alipanguwa washindani wake hadi kumshinda aliyekuwa mbele wakiwa umbali wa mita 20 tu kumaliza mbio hizo alizokamilisha kwa dakika 3:34.40.

Jedwari linaloonyesha idadi ya medali, hongera sana Kenya...
Jedwari linaloonyesha idadi ya medali, hongera sana Kenya…

 

Waliopata dhahabu na umbali wa mita walizokimbia kwenye mabano ni; kwa upande wa wanaume  – David Rudisha (800); Asbel Kiprop (1,500m); Nicholas Bett (400 kuruka vihunzi); Ezekiel Kemboi (3,000 kuruka vihunzi juu) na Julius Yego kurusha mkuki).

 

Kwa upande wa wanawake waliopata dhahabu ni Vivian Cheruiyot kwa mbio za mita 10,000 na Hyvin Kiyeng mbio za mita 3,000 kuruka vihunzi. Medali za fedha zilikwenda kwa Elijah Manangoi (1,500); Caleb Mwangangi (5,000), Geoffrey Kamworor (10,000) na Conseslus Kipruto (3,000).

 

Wanawake waliopata fedha ni Faith Chepng’etich (1,500) na Helah Kiprop wa marathoni. Paul Tanui aliyekimbia mbio za mita 10,000m alipata shaba, sambamba na Brimin Kipruto wa kuruka vihundi mita 3,000. Kwa wanawake, Eunice Sum aliyekimbia mita 800 ndiye alipata shaba.

 

Jamaica wameshika nafasi ya pili kwa kutwaa jumla ya medali 12, saba zikiwa za dhahabu, mbili za fedha na tatu za shaba.

 

Nafasi ya tatu imekwenda kwa Marekani, ambayo wanariadha wake waliikusanyia jumla ya medali 18, lakini wakikasoro moja katika dhahabu kuwapita washindi wa kwanza na wa pili, kwani walitwaa dhahabu sita, fedha sita na shaba sita kadhalika.

 

Uingereza walioingia kwa tambo wameishia nafasi ya nne kwa medali nne za dhahabu, moja ya fedha na mbili za shaba. Ethiopia walikuwa wa tano kwa medali tatu za dhahabu, sawa na Poland lakini waliwazidi wenzao kwa kuwa na medali tatu za fedha na mbili za shaba wakati Poland walikuwa na moja ya fedha na nne za shaba.

 

Nchi nyingine zilizofuatia kwenye orodha ya 10 bora ni Canada, Ujerumani Urusi na Cuba.

 

Miongoni mwa nchi za Afrika, nyingine zilizochomoza walau kidogo ni Afrika Kusini medali tatu katika nafasi ya 13, Eritrea wakawa wa 15 ka medali yao moja tu, nayo ni ya dhahabu, Misri wakapata moja ya fedha katika nafasi ya 23 sawa na Tunisia.

 

Tanzania haitokei popote katika orodha hiyo wakati Uganda wameshika mkia kwa waliotwaa medali, kwani walipata moja tu ya shaba, sawa na mataifa mengine 12 yaliyopata medali hiyo ya chini kwa ubora. Hayo ni Bosnia Herzegovina, Bahrain, Finland, Ugiriki, Grenada, Japan, Kazakhstan, Latvia, Morocco, Ureno na Serbia.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version