*Imo mechi Ligi ya Mabingwa iliyochezwa England
*FA yasema haijui, UEFA yaahidi kuchukua hatua
Mtikisiko umeikumba soka ya Ulaya, baada ya kuwapo tetesi za kashfa kubwa ya upangaji matokeo ya mechi.
Europol, chombo cha polisi cha Ulaya kimebainisha kwamba upelelezi wake wa kina umebaini kuwapo mchezo mchafu katika mechi zaidi ya 380.
Mechi hizo zinajumuisha zile za Kombe la Dunia, mechi za kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya na mechi mbili za Ubingwa wa UEFA, moja ilifanyika England.
Mkuu wa Europol, Rob Wainwright anasema kwamba upelelezi umegundua kiwango cha upangaji mechi ambacho hakikupata kuwapo kabla.
Wainwright anasema uchunguzi wao uligundua kadiri ya pauni milioni kadhaa zilizopatikana katika faida za kamari na pauni milioni 1.27 kama hongo kwa wachezaji na waamuzi, ambapo tayari kuna mashitaka kadhaa yamefunguliwa.
Uchunguzi huo umegundua waamuzi, waamuzi wasaidizi, wachezaji na wahalifu sugu 425 kwenye eneo la rushwa katika nchi 15, ambapo hadi sasa watu 50 wametiwa nguvuni.
Wainwright pia alisema kwamba kuwapo ulaji njama miongoni mwa wadau mbalimbali kunaonesha jinsi tatizo lilivyo kubw akatika soka ya Ulaya, huku magenge ya walanguzi wa kamari ya Asia yakitambuliwa kama wahusika wakubwa kwenye mchakato wa kupanga mechi.
Mkuu huyo wa polisi wa Ulaya hakuwa tayari kutaja kwa majina wahusika wala mechi ya Kombe la Mabingwa Ulaya iliyochezwa England, kwa sababu bado shughuli za uchunguzi wa kimahakama unaendelea.
Hata hivyo, Wainwright anathibitisha kwamba kashfa hiyo nchini England ilitokea kati ya miaka mitatu na minne iliyopita, lakini England si moja ya nchi zinazomulikwa kwa uozo huo.
“Mkazo umekuwa kwenye nchi nyingine, si Uingereza. Hata hivyo, tulishangazwa na kiwango cha ujumla cha shughuli za kijinai zinazoendelea na jinsi zilivyotanuka.
“Itakuwa ni ukosefu wa busara na kubweteka kwa hali ya juu nchini Uingereza kudhani kwamba ulaji njama za jinai hauhusu mchezo nchini na soka yote ya Ulaya,” akasema Wainwright.
Europol pia imeweza kunasa mechi nyingine 300 zilizojaa maswali nje ya Ulaya, hasa Afrika, Asia, Amerika Kusini na Kati.
Hata hivyo, inaelekea kuna mazingira ya kukosekana uwazi, kwani Chama cha Soka (FA) cha England kinakana kujua kuwapo kwa uchunguzi wa kashfa hiyo.
Msemaji wa FA alikuwa na haya ya kusema: “FA haijui lolote juu ya uhakika wa taarifa kuhusu madai ya upangaji mechi ya Ligi ya Mabingwa nchini England, wala haijashirikishwa taarifa yoyote itokanayo.
“Wakati Ligi ya Mabingwa huwa chini ya mamlaka ya UEFA, FA pamoja na Ligi Kuu, Ligi ya Soka na Conference, huwa waangalizi wa masoko kwa ligi saba kubwa na mashindano matatu makubwa ya vikombe nchini England na kuchukulia masuala ya uadilifu kwenye soka kwa umakini mkubwa.”
UEFA imesisitiza kwamba haina uvumilivu hata kidogo pale inapotokezea mazingira ya kashfa ya upangaji matokeo.
“UEFA inatambua kwamba Europol imetoa taarifa kuhusu tuhuma za upangaji mechi katika mashindano tofauti na inatarajia kupokea taarifa zaidi katika siku zijazo.
“Kama sehemu ya mapambano dhidi ya mchezo mchafu wa upangaji matokeo ya mechi, tayari UEFA inashirikiana na mamlaka husika kwneye masuala haya makubwa, kwani hakuna uvumilivu hata kidogo katika upangaji matokeo kwenye mchezo wetu.
“UEFA ikipata tu taarifa za kina juu ya uchunguzi huu, zitapitiwa na vyombo husika vya kinidhamu ili hatua zinazotakiwa zichukuliwe,” ikasema taarifa ya UEFA.
Tayari taarifa hiyo ya kuwapo mechi zilizopangwa matokeo kwa kuhonga ama wachezaji au waamuzi zimeanza kuwa mjadala mzito kwenye maeneo mbalimbali miongoni mwa wadau.