Moja ya habari kubwa wiki hii ni kuachwa kwa Nahodha wa Simba na Taifa Stars, Juma Kaseja kwenye usajili wa 2013/14.
Zilikuwa tetesi kwenye vijiwe vingi mitaani, huku yeye mwenyewe akisema hajui lolote, kwa vile mkataba wake ulikuwa unakaribia kumalizika.
Hata hivyo, Jumatano ilithibitika kwamba Kaseja hataidakia tena Simba msimu ujao, isipokuwa kama wana Msimbazi watabadili mawazo yao na kumrejesha kundini.
Kinachodaiwa dhidi yake ni kwamba kiwango kimeshuka, lakini inadaiwa hivyo wakati akiwa ndiye chaguo namba moja klabuni kwake, lakini pia katika Taifa Stars.
Je, kiwango kimeshuka kiasi hicho nab ado akapangwa kwenye mechi nyingi kiasi hicho, ambapo kwa wastani alionesha umahiri katika dakika nyingi alizocheza?
Kocha wa Simba, Abdallah Kibaden anadhaniwa kutopendekeza kusajiliwa kwake, maana alisikika akisema kwamba anaona Kaseja atafute timu nyingine.
Mwenyekiti wa Simba, Ismael Aden Rage alikata mzizi wa fitna kwa kueleza wazi kwamba Kaseja ameachwa, na hapo watu wamekuwa na maswali mbalimbali kuhusu kipa huyo, sababu za kuachwa na hali ya Msimbazi kwa ujumla.
Kwa siku kadhaa zilizopita, tumekuwa tukishuhudia Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zakaria Hanspoppe alidaiwa kutaka Kaseja aendelee kucheza klabuni hapo, lakini yaelekea wenzake walimzidi nguvu.
Hata hivyo, upande wa pili wa shilingi unaonyesha kwamba Kaseja amekuwa na masharti ya kuendelea kuwachezea Simba, na mojawapo ni kutaka mkataba wa Sh milioni 50 ili aanguke saini kwa usajili.
Ni kutokana na hali hiyo, wadau wa soka, wakiwamo wa Simba, wamekuwa wakijiuliza iwapo kiwango chake kimeshuka kweli au ni Simba wamekosa hizo Sh milioni 50 za usajili wake.
Kaseja alipata kutoka Simba na kucheza Yanga msimu mmoja na kurudi tena Simba, alikoanza kucheza tangu mwaka 2002, na wadau wanadhani kwamba hata kama Simba hawakumhitaji tena, walitakiwa kuachana naye kwa heshima na kwa kukaa naye, kwa sababu ameisaidia mengi, ikiwa ni pamoja na kuleta makombe na kuwaongoza kama nahodha.
Wachezai wengine hivi karibuni waliopata kuwa wakichezea Simba au kukaribia kusajiliwa kisha kuhamia kwa mahasimu wao Yanga ni pamoja na Kelvin Yondani, Mbuyu Twite aliyewapelekesha sana Msimbazi na Mrisho Ngasa aliyekuwa Yanga akaenda Azam kisha Simba na sasa amerudi Yanga.
Usajili bado unaendelea, ambapo kila timu inajiwinda kwa ajili ya kupata kikosi bora cha ligi msimu ujao, ambapo Simba hawatashiriki mashindano ya kimataifa kwani walishika nafasi ya tatu na Yanga watashiriki Klabu Bingwa Afrika, wakiwa ndio mabingwa.
Uongozi wa Simba umekuwa na migawanyiko katika siku za karibuni, ambapo Hanspope aliwahi kujiuzulu kabla ya Rage kumwangukia ili arudi lakini Makamu Mwenyekiti aliyekuwa pia na nguvu kwenye usajili, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ alijiuzulu na kukataa kabisa kurudi.