Menu
in , , , ,

KARIBU KARIAKOO PRINCE MPUMELELO DUBE

Mtoto wa Mfalme Prince Mpumelelo Dube ametibuana na mabosi zake wa Azam FC. Ameomba kuondoka katika timu, kuhamia katika timu nyingine ya kishindani zaidi. 

Haujakosea kusoma. Ni kweli Dube ameomba mkataba wake unaokata roho baada ya miaka miwili na nusu uvunjwe awe huru kutafuta timu mpya anayoitaka. 

Umewaza maisha ya Dube nje ya Tanzania? Umekosea! Dube atabakia nchini na moja ya kituo chake kipya cha kazi kitakuwa Kariakoo. Ni Simba SC au Yanga SC. Ishi humo. 

Dube, karibu Dar es salaam kwa Mheshimiwa Albert Chalamila, karibu katika jiji la maajabu. Hii ni ardhi aliyofia na kuzikwa Steven Kanumba na filamu zake.

Ni Dar es Salaam hii hii anapoteketea Chid Benz na umwamba wake wote, nini zaidi unahitaji kujuzwa kuhusu Dar es salaam? Hapa kila mtu ana sura yake na moyo wake, usidanganyike na vicheko. Watu wabaya na wazuri wanaishi katika jiji hili. 

Unataka starehe? Zipo, mpaka zile zisizompendeza shetani. Hii ndio Dar es salaam tamu iliyomkimbiza Mr Nice na kumfedhehesha 20 Percent akiwa katikati ya utamu wake.

Hili ndilo jiji pekee duniani wanakopatikana watu aina ya Shilole, Snura, Amber Lulu na Giggy Money kwa wakati mmoja. Wako wazuri hapa wa kila rangi na utakutana nao kama alivyokutana nao mahotelini Andrey Coutinho kipindi kile, uamuzi ni wako kijana mwenzangu Dube.

Karibu Dube. Kama umekuja na akili zako kama alivyokuja nazo Mzamiru Yassin kipindi kile anatoka Mtibwa Sugar, bila shaka una pepo yako ndogo ya kuishi Kariakoo. Ila kama umekuja na mabegi tu kama alivyokuja nayo Said Bahanuzi jiandae kuishangaa Kariakoo kama anavyoishangaa Ibrahim Ajib hivi sasa. Jiji limekosa adabu hili.

Nilivyokutazama na niliyoyasikia kuhusu wewe bila shaka una sifa zote za kuwa mchezaji wa kucheza hatua za Makundi ya klabu Bingwa Afrika katika kila msimu. 

Jiji la maajabu sasa linakaribia kupata mtu wake wa maajabu! Wakati huu huruma yangu iko mastaa wengi wanaocheza katika nafasi ya Dube ndani ya timu hizo vigogo. Kivyovyote vile hawapendi kuona, kusikia taarifa za Dube. Hofu imewapanda. 

Uwezo wa Dube unampa nafasi ya kuanza moja kwa moja katika vikosi vyote vya timu za Kariakoo. Bahati nzuri kwake Dube ataenda kukutana na makocha mahiri kimbinu.

Simba SC na Yanga SC zina aina ya makocha wanaoamini katika uwezo. Dube una yote mawili. Una uwezo, lakini pia una jina. Hii hawi nayo kila mchezaji. Iko kwa wachezaji wachache. 

Dube haendi moja ya timu ya Kariakoo kwa nguvu ya viongozi, wanachama au mashabiki kama wanavyosajiliwa mastaa wengine. Amefanya kazi. Haitaji kujielezea kwa kinywa

Mara ngapi unaona hili likitokea kwenye usajili wa Bongo uliotawaliwa na tabia za watu wa ‘ Bongo Movie’? Mara nyingi tu. Watu wa nje ndiyo huwa wanapambana kuliko mapambano ya mchezaji mwenyewe kiwanjani. Kwa Dube iko tofauti. 

Dube ana muda mwingi wa kucheza nchini. Ana muda mwingi wa kulikuza jina lake tofauti na alivyokuwa na Azam FC. 

Yanga SC na Simba SC ni mahala sahihi kwake kwa wakati huu, kwanini? Sababu ni mbili tu. Moja, Atacheza mechi nyingi kubwa, hivyo atapata uzoefu na mbili, yuko kwenye barabara ya kwenda Ughaibuni.

Ndiyo, Michuano ya Ligi ya Mabingwa ni ndoto za wachezaji wengi wa Kiafrika, hii ni fursa kwake kuonesha thamani yake.

Akijiunga na moja ya mkubwa wa Kariakoo akili yake inatakiwa kupoa mara mbili zaidi ilivyopoa nyakati zile anatoka kwao kuja kujiunga na Azam FC miaka minne iliyopita.

Anataka sifa na makelele ya Kariakoo? Vipo viti vya Meddie Kagere na Fiston Mayele ambavyo havijapata mtu wa kuvikalia mpaka leo hii.

Ziko laki na viroba vya mchele vinavyomsubiri kama akiamua kuwa ‘mfalme wa Kariakoo’ katika moja ya timu. Mashabiki hawana hiyana ukiwafanyia vile wanavyotaka. 

Na kama nafsi yake ina wivu wa kufika alipofika Mbwana Samatta au anapokwenda Patson Daka yule Mzambia pale Leicester City wakati ni huu.

Magazeti hayataacha kuandika habari zake, akifanya vyema yatasifia, akiboronga atashughulikiwa vilevile, japo asiyaweke akilini. Hii ni changamoto anayotakiwa kuizoea siku ya utambulisho wake tu. Iwe Jangwani, iwe Msimbazi. 

Binafsi nimeona nuru kubwa ikiangaza ndani yake, nimemuona staa mpya mjini nje ya mipaka ya Tanzania.

Kitu pekee anachotakiwa kukumbuka Dube kwa sasa, anakaribia kuingia Kariakoo iliyo ndani ya Jiji la Dar es salaam, mengi yasiowezekana kwingine, hufanyika kirahisi hapa. Karibu mtoto wa mfalme.

SIMBA SC NA CHAMA KILA MMOJA ATAMVUTA KATI MWENZAKE

Mkataba wa Simba SC na Clatous Chama unakwenda kukata roho mwishoni mwa msimu huu. Nasikia baada ya hapo kila mmoja atashika njia yake.

Inatajwa hivi na watu wa  karibu wa Simba SC na watu wa karibu na Chama. Kuna mengi yanayoendelea nyuma ya pazia kuhusu Chama na Simba SC.

Kıbaya zaidi ni manazi wachache wa Simba SC wanaoelewa kinachoendelea. Wengi bado wako kizani. Hawajui kinachoendelea.

Mwisho wa siku Chama amewagawa kati manazi wa wa timu. Kuna kundi linalotamani apewe mkataba mpya haraka iwezekanavyo. Lakini liko kundi linalotaka aondoke hata hivi sasa.

Kiwango chake katika michezo ya hivi karibuni kimewafanya wanaotaka apewe mkataba mpya wawe na kitu cha utetezi katika mikono yao.

Kiwango chake katika michezo ya mechi za mtani ni sehemu nyingine inayomuhukumu kwa watu wanaotaka aondoke hata muda huu. Mchuano ni mkali.

Imewahi kumtokea kiungo wa zamani wa Yanga SC na Simba SC, Haruna Niyonzima alivyokuwa na Yanga SC kabla ya baadae kwenda kujiunga na Simba SC. Haruna alikuwa na maisha ya namna hii ambayo Chama anaishi na manazi wa Simba SC.

Wanayanga waliishi katika mtindo huu na Haruna. Hadi Haruna anajiunga na Simba SC wale manazi wasiompenda walijisemea moyoni HAYA KIKO WAPI?

Manazi wale wakaenda mbali. Wakazichoma moto jezi zake hadharani. Mpira ni mchezo ajabu. Lilikuwa suala la muda tu. Haruna baadae alirejea Yanga SC kwa shangwe kubwa.

Wale waliomkataa na kuchoma moto jezi zake ndiyo walikuwa vinara wa mapokezi yake kwa nderemo na vifijo kuanzia pale Airport Jijini Dar es Salaam hadi Jangwani. Kila kitu wakasahau. Huu ndiyo mpira.

Tanzania Sports

Sijui hatima ya Chama na Simba SC itakavyokuwa. Lakini ninachokiona sasa kila mmoja anajaribu kumvuta kati mwenzake kuhusu mkataba mpya.

Kiwango anachokionesha sasa kinatosha kumfanya apewe mkataba mpya, tena mnono, lakini nani ana uhakika na kiwango chake katika pambano la mtani? Hili linabaki kuwa swali gumu zaidi katika nyakati hızı.

Hatujui baada ya msimu kumalizika Chama na Simba SC wataamua kitu gani juu yao. Huku nje Kila mmoja anasubiri kuona ndoa yao iliyoko mashakani hivi sasa kama itaendelea au kila mmoja atashika njia yake.

Lakini kuna mahala Chama amewageuza mateka wake Simba SC. Wako kiganjani mwake kwa muda mrefu sasa. Ndiyo mfalme wa timu katika nyakati hizi baada ya ufalme wa Emmanuel Anord Okwi kuondoka Msimbazi

Chama katika ubora wake anabakia kuwa mchezaji hatari zaidi katika lango la adui. Inawezekana Simba SC wanatamani kuachana nae, lakini swali wanalojiuliza sasa sokoni kuna mchezaji wa daraja lake?

Kila wakilifikiria jibu la swali hilo, hawajui nini waamue juu yake. Katika muda huu ambao Chama anakwenda ukingoni mwa mkataba wake, kisha Simba SC wanataka kujenga timu yao mpya viongozi watakuwa wamegawanyika kati. Hawajui waamue nini.

Ilitokea miaka kadhaa nyuma Chama alivyoondoka Simba SC na kwenda kusajiliwa RS Berkane. Ndani ya Berkane Chama alikuwa na maisha magumu. Akarudi zake Tanzania uliko ufalme wake.

Hadi sasa mkataba wake unapokwenda kumalizika Chama ndiyo staa wa timu. Chama anajua atavutana vutana na mabosi wa Simba SC, mwisho wa siku atakakutana nao kati.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version