Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA) kimetangaza mchakato wa uchaguzi wa chama hicho ambao unaanza kesho (Septemba 23 mwaka huu).
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Ombeni Zavala, mchakato utaanza kesho ambapo fomu zitatolewa ofisi ya TWFA ambayo iko Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 10 jioni.
Mwisho wa kuchukua na kurudisha fomu ni Septemba 27 mwaka huu. Nafasi zinazogombewa ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu, Mhazini, Mjumbe wa Mkutano wa TFF, na wajumbe watatu wa Kamati ya Utendaji.
Ada ya fomu kwa nafasi za Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Katibu ni sh. 200,000 wakati nafasi zilizobaki ni sh. 100,000. Uchaguzi wa chama hicho kwa mujibu wa Kalenda ya Uchaguzi ya Wanachama wa TFF iliyotolewa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF utafanyika Novemba 4 mwaka huu.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)