KAMATI ya Utendaji ya TFF ya imefanya jambo jema kulimaliza kwa busara kubwa suala la adhabu waliyoitoa kwa Yanga ya kutoshiriki mechi za kimataifa baada ya Shirikisho la vyama vya Soka vya Afrika Mashariki na ya Kati(CECAFA) kuiadhibu.
Yanga iliadhibiwa kwa kutoingiza timu uwanjani kwenye mechi ya kutafuta mshindi wa tatu wa mashindano ya Kombe la Kagame Dar es Salaam mwaka huu.
Kamati hiyo inastahili pongezi kwa sababu uamuzi wake umekuwa wa busara na umezingatia maslahi ya Taifa, maslahi ya familia ya soka na maslahi ya mchezo wenyewe kwa ujumla wake.
Mjadala wa suala la adhabu ya TFF kwa Yanga ufungwe ili upande unaotetea ubingwa wa Tanzania Bara mwaka huu na utakaotuwakilisha mwakani kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika uelekeze nguvu zake zote kwenye kufanikisha hayo.
Upande unaopigana kuziba pengo la pointi ulizopoteza kwa vipigo na sare, ujielekeze zaidi katika kuhakikisha pengo hilo linazibwa na upande unaoiandaa timu yetu ya Taifa kwa mechi ya muhimu dhidi ya Sudan pamoja na Mkutano wake Mkuu nao ujiweke sawa kwa hayo badala ya kuendeleza vijembe kwa jambo lililokwisha kufa.
Athari ya vijembe hivyo ni kujengeana chuki za ndani kwa ndani na mawazo ya “we waache tu, si wanajifanya watemi, tutaonana wakijikwaa tena” kama atakayepigwa kijembe na Yanga ni TFF, endapo Shirikisho hilo la soka lina angalau jeuri ya kufikiri hivyo dhidi ya Yanga kulingana na nitakayoyaeleza baadaye kwenye makala hii.
Nimeona nitoe tahadhari hiyo kutokana na ukweli kwamba viongozi wetu kadhaa wa soka hupenda kutumia matukio mazito yanayozikuta klabu zao kujenga umaarufu kwa maujiko hewa kwa wadau mbalimbali hasa wafuasi wa klabu zao wenye upeo mdogo.
Si jambo lisilowezekana kumsikia kiongozi wa Yanga leo akisema “tumewabwaga TFF” au “tulijua lazima tungeshinda kesi hii kwa sababu tuliadhibiwa bila kanuni kufuatwa”.
Nadhani sasa mtu yeyote hapaswi kumkejeli mwingine katika suala lililomalizika. Limalizike kwa sababu yoyote ile si jambo la msingi na si jambo la kujadilika, la msingi ni kwamba, suala limemalizika na lililobaki ni la adhabu ya CECAFA tu, ambalo,ili Yanga walimalize, wanahitaji msaada mkubwa wa TFF katika kuwashawishi CECAFA washushe hasira kama TFF hiyo ilivyowasaidia kupata Katiba ya CECAFA kwa kukatia rufani kwenda kwenye Mahakama ya Usuluhishi wa Migogoro ya Michezo(CAS).
Katika hali hiyo, nitawashangaa Yanga wakiendeleza vijembe kwa TFF hata baada ya TFF hiyo kuwachukulia viongozi wake hatua sahihi ya kutowafungia tofauti na ilivyowafanyia wenzao wa Simba waliofungiwa.
Pamoja na kuomba kufungwa kwa mjadala wa adhabu ya Yanga ya TFF, naomba niishauri tena TFF kuacha kuwa na uvumilivu kwa Yanga pekee na kuwa wakali sana kwa wengine, hasa Simba.
Nilishawahi kubainisha kwamba siku zote Yanga ikiteleza, viongozi wa TFF hushughulikia suala hilo kwa ubaridi na katika hali inayoonyesha kwamba suala hilo linashughulikiwa kiofisi.
Lakini Simba inapoteleza,kauli za watendaji wa TFF, hasa katibu Mkuu wake Frederick Mwakalebela, huwa kali dhidi ya wakosaji wa klabu hiyo na maneno mengi ya kibabe hutolewa.
Kauli kama “lazima sheria ifuate mkondo wake” na “tutachukua hatua kali ili liwe fundisho” huwa za kusikika hapa na pale kutoka kwa watendaji hao kama vile hatua za kuchukuliwa ni za ugomvi binafsi na si za kiofisi!
Kibaya ni kwamba aghalabu kauli hizo hutolewa hata kabla ya vyombo vya maamuzi vya TFF havijaanza au kumaliza kusikiliza kesi hizo za Simba! hali hiyo inaonekana kama ushawishi kwa vyombo hivyo viamuaje kesi hizo!
Na ndiyo maana naamini kabisa kama ingekuwa Simba ndiyo haikupeleka timu uwanjani dhidi ya Yanga, moto ambao ungewashwa na TFF ungekuwa wa ukubwa wa kutisha!
Naamini hivyo kwa kumtazama Katibu Mkuu wa TFF alivyokuwa akitema moto kila kwenye kipindi cha michezo redioni katika suala la Kaduguda na Rubeya ambapo kwenye suala la Yanga alikuwa baridi kama barafu hata aliposhambuliwa kwa kumuandikia barua Mwenyekiti wa Yanga, Iman Madega,ya kumtaka ajieleze.
Alishambuliwa na mwenyekiti huyo kwa swali la yeye mwajiriwa wa TFF alipata wapi mamlaka ya kumwandikia barua ya kujieleza mjumbe wa Kamati ya Utendaji ambaye ndiye mwajiri wake?
Katibu Mkuu wa TFF alishindwa hata kufunua mdomo na kujibu kuwa aliyemwandikia barua hiyo alikuwa kiongozi wa klabu kwa tuhuma za aliyotenda akiwa kwenye wadhifa huo wa kuongoza klabu.
Alishindwa kabisa kumwambia kwamba alimuandikia barua hiyo kama ambavyo angemuandikia barua kiongozi wa klabu yoyote ile asiye mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF kwa kosa ambalo angelitenda kama kiongozi wa klabu hiyo.
Hali hii ya uvumilivu kwa Yanga tu na ukali kwa wengine ndiyo iliyoamsha hoja inayotokana na maneno yanayosemwa sana chini chini kwamba Yanga inaogopwa kwa sababu ni timu ya serikali!
Ingawa siioni mantiki ya madai hayo kutokana na ukweli kwamba kura zilizoiweka madarakani serikali hii ni za mashabiki wa klabu tofauti na si wa Yanga tu, lakini nailaumu TFF kwa kupalilia utolewaji wa madai hayo kwa kuwa wavumilivu kwa klabu moja tu ambapo ilipaswa iwe na uvumilivu huo kwa klabu zote.
Ushindi wa kishindo ulioiweka madarakani serikali hii wa asilimia zaidi ya 80 haukutokana na kura za wanachama na mashabiki wa Yanga peke yao.
Licha ya ukweli kwamba Yanga ina mashabiki wengi kuliko Simba popote Tanzania,isipokuwa Shinyanga, lakini tofauti ya idadi ya mashabiki hao haiko kwa uwiano wa asilimia 80 kwa 20! inaweza ikawa ni aslimia 50 kwa 45 na tano ni kwa wasio na ushabiki kwa yoyote kati ya timu hizo.
0713 297085
Barua pepe: ibramka2002@yahoo.com