*Jamal Emil Malinzi aliyeenguliwa kugombea urais wa TFF na Hamad Yahya aliyeondolewa kwenye kinyang’anyiro cha kuwania uenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu (TPL Board).
KAMATI ya Rufani ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inayoongozwa na Idd Mtiginjola imetupa maombi ya kufanyia marejeo (review) uamuzi wake kama yalivyowasilishwa mbele yake na waombaji watano.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za TFF, Dar es Salaam leo mchana (Februari 18 mwaka huu), Mtiginjola ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo amesema wamepitia Katiba ya TFF na Kanuni za Uchaguzi za TFF na kubaini kuwa hakuna Ibara yoyote inayotoa fursa ya review kwa uamuzi ambao wameshaufanya.
Amesema Kanuni za Mwenendo wa Madai (CPC) katika mahakama za kawaida zinaruhusu Hakimu aliyefanya uamuzi katika kesi kufanya marejeo, lakini katika masuala ya mpira wa miguu hakuna fursa hiyo, hivyo hawawezi kujitungia kitu kipya kwani kazi yao ni kufanya uamuzi kwa kutafsiri Katiba na kanuni walizopewa na mamlaka ya uteuzi (TFF).
Waombaji watano waliokuwa wakitaka Kamati hiyo ifanyie marejeo uamuzi wake kutupa rufani zao ni Jamal Emil Malinzi aliyeenguliwa kugombea urais wa TFF na Hamad Yahya aliyeondolewa kwenye kinyang’anyiro cha kuwania uenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu (TPL Board).
Wengine ambao waliomba kuwania ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF na Kanda zao kwenye mabano ni Eliud Peter Mvella (Iringa na Mbeya), Farid Salim Nahdi (Morogoro na Pwani) na Mbasha Matutu (Shinyanga na Simiyu).
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)