Kamati itakayoratibu mfumo mpya wa wa uendeshwaji wa Ligi Kuu Tanzania bara inategemewa kutembelea nchi zinazoendesha ligi zao kwa mfumo wa kampuni ili kujifunza mafanikio ya nchi hizo katika uendeshaji wa ligi kwa mfumo huo kampuni.
Akizungumza na NIPASHE jana, mmoja wa wajumbe wa kamati ya vilabu inayoratibu kuanzishwa kwa kampuni, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ alisema kuwa baada ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) kukubaliana na vilabu kutafuta njia bora ya kuendesha ligi, mpango uliokuwa ukiendelea wa vilabu kutishia kususia ligi umesimamishwa.
Kaburu alisema kuwa haitakuwa vizuri kwa vilabu kuendelea kushikilia msimamo wao wa kuanzishwa kwa kampuni wakati tayari TFF imekubali kukaa nao meza moja na kuangalia mfumo bora wa kuendesha ligi.
“Ukiangalia tayari wajumbe watatu waliokuwepo kwenye kamati ya vilabu ya kuanzisha kampuni wapo kwenye kamati ya TFF, sisi kama vilabu matakwa yetu ni kutaka ligi iendeshwe na kampuni, lakini baada ya TFF kukubaliana na sisi kutafuta mfumo bora wa uendeshwaji wa ligi yetu hatuna sababu ya kushikilia kususia ligi,” alisema Kaburu.
Aidha, alisema kuwa ili kujiridhisha wataenda kutembelea nchi za jirani zinazoendesha ligi kwa mfumo wa kampuni ili kujua faida na hasara yake na mafanikio waliyoyapata nchi hizo kwa ligi kuendeshwa na kampuni.
“Tumeona kuna njia nzuri na fupi ya kufikia maafikiano na TFF, vilabu hatutaki kufika mbali..TFF wamekuwa wazi sana kwa suala hili na ligi ya mwakani itakuwa na tofauti kubwa wa ki-mfumo,” aliongeza Kaburu.
Kaburu alisema kuwa hata kanuni za Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA) zinakataza ligi kuendeshwa na chombo kingine nje ya chama cha soka cha nchi husika ambacho ni mwanachama wa FIFA.
“Ni lazima tumalizane kwanza na TFF tukubaliane nao kwa sababu wao ndio wenye mpira wa hapa nchini…. vilabu sio mwanachama wa FIFA, hivyo ni lazima tufuate kanununi zilizopo,” alisema Kaburu.
Awali uongozi wa vilabu ulitishia kutoshiriki Ligi Kuu msimu ujao endapo kampuni haitoruhusiwa kuendesha ligi, hata hivyo baada ya TFF kupitia kwa Rais wake Leodgar Tenga, kukubaliana na vilabu juu ya mabadiliko ya uendeshwaji wa Ligi Kuu, uongozi wa vilabu umesitisha azma yao na kukaa na TFF kujadili mfumo bora wa kuendesha ligi msimu hujao.