Menu
in

Kaeni chonjo, CAF yawataja

Azamfc

Shirikisho la soka barani Afrika CAF limezitaja klabu ambazo zitachuana kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho msimu huu 2021/2022.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na CAF inaonesha timu pinzani zitakazochuanana vilabu vya Tanzania katika mashindano ya kimataifa msimu huu. Tanzania inawakilishwa na timu nne za Simba,Yanga na Azam za jijini Dar es salaam na Biashara United ya mkoani Mara.

Biashara United imepata nafasi hiyo baada ya kumaliza ligi ikishika nafasi ya nne, huku wawakilishi wa msimu uliopita Namungo ya mkoani Lindi ikikosa nafasi kabisa.

SIMBA vs JWANENG/DFC Beme

Mabingwa wa soka nchini Tanzania, Simba wamepangwa kukutana na timu mbili za Jwaneng na DFC Beme. Lakini timu hizo zinatakiwa kupepetana kwanza zenyewe ili kupata mshindi wa kuifuata Simba katika raundi ya pili. 

Simba hawajapangwa kuanza Ligi ya Mabingwa hatua za awali badala yake watakutana na timu mojawapo katika raundi ya pili. Msindi wa raundi ya pili ndiye ataingia Ligi ya Mabingwa Afrika. Jwaneng ni timu ya Botswana, wakati wapinzaniwao DFC Beme inatoka nchini Afrika ya kati.

YANGA vs RIVERS UNITED

Vijana wa mitaa ya Jangwani na Twiga nchini Tanzania, Yanga wamepangwa kupepetana na Rivers United ya nchini Nigeria katika raundi ya awali. Kwa mujibu wa CAF, Yanga wataanza nyumbani kisha wataelekea Nigeria kucheza mchezo wa marudiano ambao utatoa mwelekeo wao kati ya Septemba 10 na 12 mwaka huu.

Tanzania Sports
CAF

Mshindi atakayepatikana katika pambano la Yanga na Rivers United atapambana na mshindi wa mechi nyingi ya Fasil Kenema ya Ethiopia dhidi ya Al Hilal ya Sudan.

Historia ya klabu ya Rivers United inaonesha kuwa ilianzishwa mnamo mwaka 2016 kutokana na muungano wa timu mbili za nchini humo, Dolphins na nyingine Sharks ambapo inatumia uwanja wa Yakubu Gowon uliopo jijini Port Harcourt.

Jina la Yakubu Gowon ni kubwa katika historia ya siasa za Nigeria. Ni miongoni mwa wanajeshi waliopata kuingia kwenye mfumo wa utawala mwishoni mwa karne ya 20 kufuatia mapinduzi ya kijeshi ya mara kwa mara yaliyotokea huko.

Rivers United, wao wanashiriki Ligi ya Mabingwa kwa mara ya pili baada ya kufanya hivyo mwaka 2017 na kutupwa mashindano na Al Merreikh ya Sudan.

AZAM FC vs HORSEED

Mabwanyenye wa Chamazi jijini Dar es salaam, Azam wamepelekwa nchini Somalia kupepetana na klabu ya Horseed ya jijini Mogadishu. Klabu hiyo inayotumia dimba la Banadir wameingia amshindano baadani kushika nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu ya Somalia. Kwa Somalia klabu hiyo ni  wababe baada ya kunyakua taji la Ligi Kuu mara 12 katika historia yao.

BIASHARA UNITED vs FC DIKHIL

Wageni wa mashindano ya Kombe la Shirikisho, Biashara United wamepwangwa kuchuana na FC Dikhil ya Djibout. Mshindi wa mchezo huo atakwenda kupambana na mshindi kati ya Hay Al Wadi ya Sudan na Ahli Tripoli ya Libya.

Hii ni mara ya kwanza Biashara United kushiriki mashindano ya Kimataifa. Kwa msimu wa pili mfululizo Tanzania inatoa mwakilishi mpya kwenye mashindano ya kimataifa baada ya Namungo kushiriki hatua ya makundi kwenye mashindano ya Shirikisho CAF.

Ni dhahiri kibarua kilichopo sasa ni sawa na kuwaambia viongozi,wachezaji na mashabiki wao wakae chonjo kwa sababu CAF imeshataja njia ya kupita ili kusonga mbele mashindanoni.

Swali moja linalotakiwa kusubiriwa majibu ni je timu zetu hizi nne zitafaulu kutikisa mashindano ya Afrika msimu huu? Je kuna timu inaweza kufikia rekodi ya Simba kucheza fainali ya Kombe la Caf? Je timu gani ataweza kuapata mafanikio angalau kufika robo fainali ya michuano yao kama Simba ilivyofanya msimu uliopita?

Vilevile ni changamoto kwa Simba wenyewe ambao wanatakiwa kuvunja rekodi yao ya kufika robo fainali ili wapige hatua mbele. Je wataweza muziki wa Jwaneng au DFC Beme? Hakika hilo linasubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka nchini.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version