Arsenal wameshinda rufaa zao kuhusiana na kitendo cha mwamuzi Andre Marriner cha kutoa kadi nyekundu kwa Kieran Gibbs Jumamosi kwenye mechi dhidi ya Chelsea.
Chama cha Soka, FA, kimesema kwamba Arsenal wamewashawishi kwa hoja zao juu ya utoaji kadi kwa mtu ambaye hakuwa amehusika na kosa katika mechi iliyokuja kuisha kwa Chelsea kushinda 6-0.
Baada ya ushindi wa rufaa ya awali, kadi nyekundu ilihamishiwa na FA kwa Alex Oxlade-Chamberlain ambaye ndiye aliunawa mpira huo, lakini Arsenal pia wakapangua hoja wakisema kwamba mpira alionawa haukuwa ukielekea golini.
Arsenal walisema kwamba, sheria ya kadi nyekundu kwa anyeunawa mpira ipo wazi, na ni kwamba ataipewa mchezaji aliyeuzia kwa mkono mpira unaoelekea dhahiri golini. Hata hivyo, mpira aliourukia na kuzuia Oxlade-Chamberlain ulikuwa ukitoka nje, hivyo kadi ilitolewa kimakosa.
Kwa msingi huo, katika mechi ya Jumamosi, hapakuwa na mchezaji yeyote aliyetakiwa kupewa kadi nyekundu, na pengine matokeo yangekuwa tofauti, ikizingatiwa kwamba kutolewa kwa Gibbs ambaye hakuhusika kabisa kulisababisha pengo kubwa kwenye ulinzi.
Kana kwamba hiyo haitoshi, baada ya kipindi cha kwanza, mchezaji wa kimataifa wa Ufaransa na beki wa kati wa Arsenal, alilazimika kubaki nje kutokana na maumivu ya paja, hivyo ukuta wa Arsenal ukazidi kuwa teketeke.
Tayari mwamuzi Marinner ameshaomba radhi kwa kitendo chake, na taasisi inayosimamia marefa imesema ni bahati mbaya sana kumfika jambo hilo, lakini imeamua kumpa nafasi ya kujirekebisha kwa kuchezesha mechi Jumamosi ijayo badala ya kumweka benchi ambapo angeweza kuathirika zaidi.