Menu
in , ,

JURGEN KLOPP HAWEZI TENDA MIUJIZA

 

Ujio wa Jurgen Klopp umepeleka matumaini na matarajio makubwa ndani ya Liverpool. Washabiki wa timu hiyo England na duniani kote wana imani kubwa juu ya uwezo wa kimbinu na kiutawala wa meneja huyo wa zamani wa Borussia Dortmund aliyesaini mkataba wa miaka mitatu wiki iliyopita.

Hata wadau wengine wa soka wasio na mapenzi na Liverpool wameonyesha kumwamini Klopp. Sir Alex Ferguson aliyewahi kudumu na Manchester United kwa miaka 27 pia ameonyesha kuwa na mtazamo kuwa Klopp anakwenda kuipa mafanikio makubwa Liverpool.

Sir Alex aliyeiongoza United kushinda taji la EPL mara 13 amesema kuwa anahofia kuona meneja mahiri na mweledi kama Jurgen Klopp anakwenda kuifundisha klabu hasimu ya Manchester United. Amedai kuwa ni wazi kuwa Liverpool itapata mafanikio chini ya meneja huyo Mjerumani.

Haishangazi hata kidogo kuona Jurgen Klopp akichukuliwa kama mkombozi wa Liverpool yenye historia kubwa England na Ulaya. Mafanikio aliyoyapata akiwa na Borrussia Dortmund yanastahili kumwaminisha karibu kila mshabiki wa soka la Ulaya kuwa meneja huyo hawezi kushindwa kutimiza yale yanayotarajiwa na mashabiki wa Liverpool hata kabla ya mkataba wake wa miaka mitatu kufikia mwishoni.

Klopp alifanikiwa kuzima utawala wa Bayern Munich na klabu nyingine kali za Ujerumani na kuifanya Dortmund kuwa moja kati ya timu tishio Ujerumani na Ulaya nzima. Kumbukumbu ya mambo makubwa aliyoyafanya akiwa na Dortmund ni ishara kubwa ya umahiri alio nao.

Akijadiliana jambo na kocha wa academy ya Liverpool
Akijadiliana jambo na kocha wa academy ya Liverpool

Si jambo dogo kushinda taji la Bundesliga mara mbili mfululizo ukiwa na timu kama Borussia Dortmund ambayo uwezo wake wa kifedha wa kusajili wachezaji hauwezi kulinganishwa na Bayern Munich ambayo imekuwa ikitawala soka la Ujerumani kwa kipindi kirefu kutokana na uwezo wake wa kifedha.

Lakini Jurgen Klopp alifanya hivyo kwenye misimu miwili ya 2010/11 na 2011/12. Hakuhitaji kushindana na uwezo wa kifedha wa Bayern Munich kuyafikia mafanikio hayo. Kwenye maandalizi ya msimu wa 2011/12 alitumia kiasi cha chini ya euro milioni 10 kwa ajili ya usajili wa wachezaji huku Bayern wakitumia takribani euro milioni 45 lakini bado akawapiku na kutwaa taji la Bundesliga kwa msimu wa pili mfululizo.

Kwa kuwa Liverpool pia haina uwezo wa kifedha wa kushindana kusajili wachezaji na timu kama Manchester City, Chelsea na hata Manchester United ndio maana inaonekana Klopp ndiye meneja sahihi zaidi wa kuipa mafanikio Liverpool.

Ndani ya kipindi cha miaka mitano ilyopita Liverpool imetumia takribani paundi milioni 400 pekee kwa ajili ya usajili huku fedha nyingi kati ya hizo zikichangiwa na mauzo ghali ya Fernando Torres, Luis Suarez na Raheem Sterling. Wakati Manchester City imetumia zaidi ya paundi milioni 60o, Chelsea ikitumia zaidi ya paundi milioni 560 kwa kipindi hicho hicho.

Klopp amesema kuwa kinachohitajika kwa sasa ni kukitumia kikosi kilichopo hata kama timu haitampa pesa ya usajili mwezi Januari. Wachezaji kama Philippe Coutinho, Roberto Firmino, Daniel Sturrridge, Christian Benteke na wengine huenda wakafanya makubwa chini ya Klopp.

Hata hivyo Jurgen Klopp si Kristo na hivyo hawezi kutenda miujiza. Anahitaji kupewa muda ili aweze kuirudisha hadhi ya Liverpool iliyopotea kwa zaidi ya miaka 20 nchini England. Hayo si maneno yangu, yamesemwa na Klopp mwenyewe.

Meneja huyo amesema kuwa matarajio ni muhimu kwenye maisha kwa ujumla na kwenye soka pia. Lakini anahitaji muda kuyafikia mafanikio yanayotarajiwa na washabiki kwa kuwa yeye hana uwezo wa kutenda miujiza. Namuunga mkono moja kwa moja.

Advertisement

 

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version