SAFU ya ushambuliaji ya Liverpool ni miongoni mwa maeneo yanayotazamwa kwa jicho la tatu. Ni safu ambayo inaundwa na washambuliaji waliocheza pamoja kwa muda mrefu. Washambuliaji watatu wamekaa pamoja zaidi ya miaka minne sasa.
Mohammed Salah, Roberto Firmino na Sadio Mane, wamedumu kikosini Liverpool na kutwaa mataji mbalimbali. mabao ya washambuliaji hao yamelata Ligi ya Mabingwa Ulaya, Supercup na Ligi Kuu EPL.
Ushindani,ubora na uwezo wao umeipa mabao mengi klabu hiyo. Kwa pamoja wamechangia mabao mengi, na hivyo wameipa nafasi Libverpool kurudisha makali ambayo yalitoeka kabla ya ujio wa Jurgen Klopp. Katika safu hiyo ilikuwa inasaidiwa na Divock Origi na Shaqiri wamekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha viwango vya washambuliaji wenzao.
Hata hivyo kocha Liverpool aliona inafaa kuongeza changamoto kwa wshambuliaji hao ili pawe na ushindani. Uamuzi wa kumnunua mshambulia raia wa Ureno, Diogo Jota ulikuwa sahihi na umelata mafanikio makubwa.
Katika kipindi ambacho Firmino aliporomoka kiwango, majukumu yake kwa kiasi kikubwa yalichukuliwa na Diogo Jota. Mreno huyo hakumwangusha kocha wake kwani alionesha ubora ulioibua mjadala ni nani apangwe kikosi cha kwanza kati ya Firmino na Jota?
Mwishoni mwa wiki iliyopita Liverpool walianza kampeni ya kuwania ubingwa wa EPL kwa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Norwich. Na jambo zuri zaidi walicheza na nyota wao Virgil van Dijk ambaye hakuonekana uwnajani tangu mwezi Oktoba mwaka 2020 kutokana na kuumia katika mchezo wao na wapinzani wa jadi Everton baada ya kugongana na mlinda mlango Jordan Pickford.
Kwenye mchezo huo Virgil alicheza kwa dakika zote 90 ikiwa ni ishara nzuri kwa vigogo hao. lakini mjadala wa Firmino na Jota bado umetawala, si huko jijini Liverpool bali kwa mashabiki wa EPL na wadau mbalimbali.
Mjadala huo unajikita ni nani atamudu kufunga mabao 20 kwa msimu kwa washambuliaji waliopo au atafutwe mwingine ambaye atawahakikishia upatikanaji wa mabao hayo.
Klopp anaonekana kuwataka washambuliaji wake wote wanne, Sadio Mane,Diogo Jota, Salah na Firmino. Katika mchezo wa ufunguzi wa EPL dhidi ya Norwich washambuliaji wake Diogo Jota, Roberto Firimino na Mohammed Salah walifunga mabao ya timu hiyo.
Mane pekee hakupachika bao. Kwa upande wa Salah amepachika mabao 100 EPL na kumfanya mchezaji wa kwanza wa Misri kufikisha idadi na kuwaacha mbali nyota kama Emr Zaki na Mohamed Mido waliowahi kucheza ligi hiyo.
Kibarua kigumu kwa Klopp ni kuamua nani awekwe benchi kati ya Mane,Firmino na Salah ili nafasi yake katika baadhi ya mechi acheze Diogo Jota. Kama hiyohaitoshi, Salah anaonekana kuwa mchezaji muhimu katika safu ya ushambuliaji kwahiyo anabaki kikosi cha kwanza.
Mane na Firmino wanakuwa washambuliaji ambao wanasimama katikati ya mjadala huo, nani kati yao ampishe Diogo Jota katika kikosi cha kwanza. Katika mchezo wa Norwich, Diogo Jota alikuwa mchezaji hatari langoni mwa wenyeji wao kiasi kwamba kocha msaidizi wa Liverpool Pep Lijnders anasema Jota ni dubwasha lisilozuilika linapoingia eneo la hatari sababu ya kasi na uwezo wa kupita mashuti.
Hilo linathibitisha uamuzi wa kumsajili kutoka Wolves msimu uliopita wa ada ya piuani milioni 45 ulikuwa bora na wenye manufaa zaidi kwa maendeleo ya Liverpool.
Klopp anawea kujisifu sasa amesajili mshambuliaji mwenye uwezo mzuri wa kutoa ushindani kwa washambuliaji wake watatu Firmino,Mane na Salah. Firmino hakuwa na msimu mzuri 2020/2021 ambako alipachika mabao 9 tu.
Lakini ameonesha mabadiliko katika mchezo wa kwanza wa msimu mpya 2021/2022 na kuwafanya washabiki wa Liverpool waanze kuona tabasamu lake. Sadio Mane alipachika mabao 16 msimu uliopita, na la kukumbukwa zaidi ni lile lililoipatia nafasi Liverpool kufuzu hatua ya Ligi ya Mabingwa.
Hata hivyo kibarua cha Klopp kipo palepale. Baadhi wanashauri washambuliaji hao wapangwe wote katika mchezo mmoja; Jota,Mane,Salah na Firmino kama walivyocheza dhidi ya Manchester City msimu uliopita.
Ikiwa wote watapangwa katika mchezo ina maana Klopp atalazimika kutumia mfumo wa 4-2-3-1. Kukosa kikosi kipana kunaipa Liverpool shida kubwa. Labda Takumi Minamino aliyeonesha kiwango kuzuri katika mechi za maandalizi ya msimu huenda akawa mbadala mzuri kikosini.
Pia kutakuwa na ingizo jipya la Harvey Elliot na Kaide Gordon ambao wameonesha maendeleo mazuri na huenda wakachukua nafasi za watu kwenye kikosi cha kwanza. Hata kama makinda hao hawatafurukuta bado atakuwa na hazina ya washambuliaji wanne katika kikosi chake hivyo kuwa na uamuzi nani aanze na nani akae benchi.
Kwa ukubwa wa majina na uwezo wao, Klopp atakuwa na mtihani mkubwa kuamua wa kumwanzisha mechi na kumridhisha yule atakayeanzia benchi.