Menu
in , ,

JOSE MOURINHO ALIVAA AKILI ZA SIR ALEX FERGUSON PALE ETIHAD

Baridi limevaa ngozi yangu hii imekuwa kawaida sana siku hizi asubuhi
kuwa na baridi kutokana na mvua, mvua ambayo imetusahaurisha kuhusu
joto la Dar es Salaam

Joto ambalo limekuwa likitutesa kwa muda mrefu sana, mateso haya huwa
ya nyakati fulani yenye majira ya joto.

Ndipo hapa huwa napenda kusema kila nyakati zina majira yake, nyakati
zote hazina majira yanayofanana hata siku moja

Ndiyo maana pale Manchester United kulikuwa na nyakati za Sir. Alex
Ferguson. Nyakati ambazo zilikuwa na majira ya mvua kwa kipindi
kirefu.

Mvua ambazo zilileta neema kwenye mavuno ya Manchester United, tangu
mwaka 1986-2013 ghala la Manchester United lilikuwa limejaa mazao
mengi sana waliyovuna viziri.

Vikombe 38 chini ya Sir Alex Ferguson, kitu ambacho kiliifanya
Manchester United ilijivunia nacho, kila shabiki wa Manchester United
akawa amezoea raha.

Paul Pogba

Paul Pogba

Hakutaka kabisa shida ipite katika maisha yake kwa sababu furaha ndiyo
nguzo ambayo ilijengwa na Sir Alex Ferguson

Nguzo hii ilisambaa mpaka kwa wachezaji wa Manchester United, kwao wao
walijiona ni wachezaji ambao wamezaliwa kushinda.

Neno kushindwa lilikuwa mbali sana kwenye ubongo wao, kila mboni zao
za macho zilipokuwa zinatizama mbele ziliona mafanikio makubwa ndani
yao.

Walitaka vikombe, walikuwa na njaa ya mafanikio kiasi kwamba neno
kukata tamaa halikuwepo ndani yao hata kidogo.

Ndiyo maana wengi wetu tulijua pale Camp Nou mwaka 1999 Bayern Munich
anabeba kombe la ligi ya mabingwa barani ulaya.

Tuliona dakika zinaelekea ukingoni na Bayern Munich alikuwa anakaribia
kwenda kulibeba kombe hili, lakini Sir. Alex Ferguson alituonesha
namna ya kutumia kwa usahihi kila sekunde unayoipata kwenye maisha
yako.

Dakika tatu (3) za nyongeza zilitosha kabisa kumhakikishia ubingwa
tena akiwa na timu yenye morali kubwa ya ushindi kwenye mishipa ya
damu yao.

Hawakukata tamaa, mechi kwao ilikuwa haijaisha na walikuwa wanasubiri
dakika ya mwisho ili kuhakikisha mechi imeisha, kuwa kwao nyuma ya
goli 1 mpaka dakika za nyongeza hakukuwavunja moyo kupigania ushindi,
mwisho wa siku ikashinda kwa magoli 2-1 magoli mawili ambayo
yalipatika dakika tatu za nyongeza.

Dakika chache sana kwenye macho ya nyama lakini ni dakika nyingi sana
kwenye mpira ndiyo maana jumamosi iliyopita Jose Mourinho alihitaji
dakika tatu za magoli mawili ya Paul Pogba ili kuirudisha timu yake
mchezoni.

Mashabiki wa Manchester City walikuwa wameshavua jezi zao na kubaki
kifua wazi ili wazipeperushe kwa furaha ya kutwaa ubingwa.

Unatwaa ubingwa mbele ya mpinzani wako mkubwa? Hapana shaka ilikuwa
furaha ya ajabu sana lakini ilikuja kuwa furaha ya muda.

Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilitawaliwa na furaha kubwa ndani yao
lakini dakika 45 za kipindi cha pili zilitawaliwa na huzuni kubwa sana.

Manchester United waliwaonesha mechi haiwezi kuisha kabla haijaisha,
walicheza kwa kujiamini na kupigana ndani yao. Hawakuhofia tena kuwa
mbele yao walikuwa wanacheza na timu bora.

Ushindi ndicho kitu ambacho kilikuwa kinazunguka kwenye fikra zao,
hatimaye roho ya Manchester United ya kipindi cha Sir Alex Ferguson
ilirudi kwao na kufanikiwa kuzuia ndoto za wapinzani wao Manchester
City.

Hawakutaka kupata aibu ambayo ingedumu kwenye vizazi vingi , ndiyo
maana kila walipokuwa wanamwangalia Sir Alex Ferguson jukwaani roho ya
kupigana ilizidi kuwa kubwa ndani yao.

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya martinkiyumbi@gmail.com

Exit mobile version