*Ni kwa ubaguzi dhidi ya Anton Ferdinand
*Kocha Fabio Capello ajitokeza kumtetea
John Terry yungali mbele ya jopo huru la Chama cha Soka (FA) cha England linalosikiliza mashitaka kwamba alimtukana kibaguzi mchezaji wa Queen Park Rangers, Anton Ferdinand.
Terry ambaye ni nahodha wa Chelsea, anaingia siku ya nne mfululizo ya usikilizaji huo Alhamisi hii, kwa kutumia maneno ya kibaguzi au yahusuyo asili ya mtu akiwa dimbani.
Jana Jumatano, Terry alitumia saa nane mbele ya jopo hilo, ambapo anakanusha kutenda kosa la aina hiyo Oktoba mwaka jana.
Hatua hizi zinakuja wakati Mahakama ya Hakimu Mkazi Wesminster ilishamsafisha dhidi ya mashitaka ya jinai yaliyokuwa yakimkabili katika suala hilo hilo.
Hata hivyo, hatua ya FA ni tofauti na ya mahakama, kwani korti ililazimika kupata ushahidi usio na chembe ya shaka ili kumtia hatiani, wakati FA inaweza kuangalia tu ujumla wa mambo na kutoa uamuzi.
Terry mwenye umri wa miaka 31 aliandamana na Mwenyekiti wa Klabu ya Chelsea, Bruce Buck kwenye ofisi za Wembley shauri linakosikilizwa. Wote wanaelezwa kuondoka muda mfupi kabla ya saa 10.30 alasiri jana.
Terry aliamua kujiuzulu kuchezea timu ya taifa ya England, kwa maelezo kwamba FA kung’ang’ania mashitaka dhidi yake kulimfanya asiweze kuendelea kuitumikia timu hiyo.
Terry alipata kuwa nahodha wa England, kabla ya kuvuliwa nafasi hiyo, baada ya kuhusishwa na kutembea na mpenzi wa mchezaji mwenzake.
Alirejeshewa tena unahodha kabla ya kadhia ya sasa, na FA ilipompokonya wadhifa huo, kocha aliyekuwapo, Fabio Capello alijiuzulu kuifundisha England. Harry Redknapp anayeifundisha sasa alimteua tena kwenye kikosi chake.
Wakati usikilizaji wa shauri hilo ukiendelea, Capello ameelezwa kwamba yupo tayari kutoa ushahidi wake mbele ya jopo hilo kwa niaba ya Terry.
Aliyekuwa msaidizi wa Capello, Franco Baldini, naye pia yu tayari kwa kazi hiyo na walijiandaa kusafiri hadi jijini London, lakini inadaiwa walifikiria kutuma taarifa za utetezi badala ya kusafiri wenyewe.
FA ilianza uchunguzi wake kabla ya kuusitisha pale polisi wa London walipoingilia na kuchunguza, kwa kuwa kisheria ni kosa la jinai kutukana mtu, na kipengele kingine cha sheria kinagusia kubagua kwa rangi, jinsi au asili.
Taarifa za Capello na Baldini, inadaiwa, zinagusia hali isiyo ya kawaida kwa mchezaji aliyesafishwa na mahakama kuitwa kujibu mashitaka ya chama cha soka katika suala hilo hilo.
Wanasheria wa Terry wanataka mashitaka ya FA dhidi ya Terry yatupiliwe mbali kwa kuzingatia msingi wa hukumu ya mahakama.
Terry alianza kuingia kwenye chumba cha shauri hilo Jumatatu, ambapo Jumanne aliondoka mapema kwenda kuiongoza timu yake kucheza mechi ya Kombe la Ligi dhidi ya Wolves, licha ya kutofanya mazoezi Jumatatu na asubuhi ya Jumanne.
Kocha Msaidizi wa Chelsea, Eddie Newton, anasema Terry alikuwa katika hali nzuri kisaikolojia, akishughulikia suala lake, lakini pia akiisaidia timu yake iliyoichapa Wolves mabao 6-0.
Pamekuwa na taarifa kwamba usikilizaji wa sasa ni wa faragha zaidi, ambapo taarifa kwa umma hazikutolewa juu ya kilichojiri.
Inatarajiwa kwamba suala hili litamalizwa wakati wowote mwishoni mwa wiki, kwa uamuzi kutolewa wa ama kumtia hatiani au la. Akitiwa hatiani anaweza kufungiwa mechi kadhaa na kutozwa faini.
Luis Suarez wa Liverpool alifungiwa mechi nane na kutozwa faini ya Pauni 40,000 kwa kosa la kumtolea maneno ya kibaguzi mchezaji wa Manchester United, Patrice Evra.
Rio Ferdinand (kakaye Anton Ferdinand) aliadhibiwa faini ya Pauni 45,000 hivi karibuni, kwa kutoa maneno ya kibaguzi dhidi ya Ashley Cole aliyemtetea Terry mahakamani kwenye kesi hiyo.
Rio alimfananisha Cole na ‘choc ice’, kwamba rangi iliyo nje si iliyo ndani. Alimaanisha Cole ni mweusi, lakini alikuwa akijidai mweupe, kwa jinsi alivyomtetea Terry ambaye ni mweupe, dhidi ya Anton, mweusi mwenzao.