Menu
in , ,

John Terry hatiani kwa ubaguzi

Hatimaye John Terry ametiwa hatiani kwa ubaguzi na amepatiwa adhabu kali.

Kwa makosa hayo, Terry ameadhibiwa kutocheza mechi nne na kulipa faini ya £220,000.
Kamati Maalum ya Chama cha Soka (FA) cha England imejidhirisha kwamba nahodha huyo wa Chelsea alimtukana kibaguzi Anton Ferdinand ambaye ni beki wa Queen Park Rangers (QPR).
Uamuzi huo umetolewa na FA baada ya siku tatu mfululizo za kusikiliza kesi yake kwenye ofisi zilizo Uwanja wa Wembley, ambapo Terry alikuwa akihudhuria.
Terry ameng’aka kwa uamuzi huo, akisema amesikitishwa kwamba FA inaweza kufikia uamuzi tofauti kabisa na wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Westminster iliyomwona hana hatia, tena katika mashitaka yale yale.
Hata hivyo, uzito wa matakwa ya kisheria kuthibitisha tuhuma katika jinai ni mkubwa kuliko kwenye madai, hivyo ilikuwa rahisi kwa FA kumtia hatiani na kumpa adhabu hiyo.
Msemaji wa kampuni inayosimamia masuala ya Terry, alisema kwamba nahodha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya England anatafakari cha kufanya.
Kwamba ameomba apate nakala ya mwenendo wa shauri zima na hukumu, ili achambue na kuona kama kuna haja ya kukata rufaa au la.
Ikiwa atakata rufaa au kueleza nia ya kupinga uamuzi huo, adhabu yake haitaaanza, lakini asipokata ataanza kukosa mechi wikiendi hii, ambapo Chelsea wanacheza na Arsenal Jumamosi.
Ni lazima atafakari na kushauriwa vyema na wanasheria wake, kwa sababu anaweza kukata rufaa na kujikuta hatia ikiidhinishwa na adhabu kali zaidi kutolewa dhidi yake.
Sakata la kumtolea Anton lugha chafu ni la tangu Oktoba mwaka jana, lilivuta hisia za wengi, ikiwa ni pamoja na kwenye mitandao ya jamii, na kujenga uhasama miongoni mwa baadhi ya wacheaji weusi na weupe.
Adhabu hii inavunja rekodi ya faini wanasoka walizopata kutozwa kwa kutoa lugha za kashfa za kibaguzi, na huenda ikawa fundisho kwa wengine.
Terry alitangaza Jumapili ijayo kuachia ngazi katika timu ya taifa, akisema amesukumwa kuchukua hatua hiyo baada ya FA kung’ang’ania kuendelea na mashitaka dhidi yake, hata baada ya Mahakama kumsafisha.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version