KWA miongo kadhaa Timu za Jeshi la Kujenga Taifa na Jeshi la Wananchi zimekuwa maarufu kwa mchezo wa mpira wa pete (Netball).
Timu hizo zimekuwa zikitamba na kuwa mabingwa wa Tanzania bara mara zote wakati mara kadhaa kwa upande wa Afrika Mashariki.
Miongoni mwa timu hizo za netiboli ni Jeshi Stars na Mbweni JKT ambazo kwa kipindi kirefu zimekuwa zikichuana vikali katika kubadilishana ubingwa.
Lakini wakati mambo yakienda vizuri kwa upande wa timu za netiboli, majeshi hayo yalikuwa kimya bila ya kuwa na timu yoyote ya maana katika masuala ya mpira wa miguu.
Katika kipindi hicho ni Idara ya Magereza iliyofanikiwa kuwa na Timu ya Prisons iliyokuwa na makao makuu jijini Mbeya ambayo sasa imeporomoka na kuwa katika ligi ya daraja la kwanza.
Nalo polisi, miaka mitano iliyopita liliandaa mkakati wa kuwasaka vijana wanaojua kucheza soka na kufanikiwa kuwa na Timu ya Polisi Dodoma ambayo mpaka sasa ndiyo inayocheza Ligi kuu ya Tanzania.
Wakati polisi wakifikiria hilo, nalo Jeshi la Kujenga Taifa bila shaka kwa kushirikiana na Jeshi la Wananchi liliweka mkakati wa kuandaa timu za soka ambapo tatu zilifanikiwa kuingia kwenye ligi kuu.
Mpaka sasa Jeshi la Kujenga Taifa lina timu tatu za soka ambazo zimeonyesha kuwa moto katika michuano inayoendelea.
Mkuu wa Kikosi cha Ruvu JKT, Kanali Mbelle ambaye kikosi chake kina timu za Ruvu JKT na Ruvu Shooting anasema Jeshi limejipanga kuinua kiwango cha soka Tanzania.
Anasema lilianza kuipandisha Ruvu JKT , halafu ikafuata Ruvu Shooting na bahati nzuri mwaka huu Oljoro JKT ya Arusha imeingia na mwakani wamejipanga kuzipokea Mlale JKT ya Ruvuma na Mgambo JKT ya Tanga.
Taarifa zaidi zinasema uongozi wa Jeshi umeshatoa maelekezo kuhakikisha Jeshi linakuwa na timu imara ambayo itakuwa Bingwa wa Tanzania na hatimaye kushiriki michezo ya kimataifa na kuondoa aibu ya kutolewa mapema katika mashindano ya kimataifa.
Kwa kipindi kirefu timu za Yanga na simba zimekuwa zikitolewa katika mechi za awali katika kuwania Klabu Bingwa Afrika .
Mkakati huo unaonekana kuandaliwa vema mwaka huu kwani tayari timu za JKT zimekuwa miongoni mwa timu ngumu zikiwa na malengo kamili.
Timu ya Ruvu JK, ilianza kwa mbwembwe kwa kuitandika Yanga Sports goli 1-0 ambayo ni kongwe na yenye mashabiki wengi Tanzania. Hadi Jumapili ya Oktoba 2, timu hiyo ilikuwa imecheza mechi nane ambapo imeshinda mbili kutoka sare sita na haijapoteza mechi yoyote kama ilivyo Simba Sports Club.
Lakini pia OljoroJKT ilikuwa imecheza mechi tisa na kupata ushindi wa mechi nne , sare mechi nne na kupoteza mechi moja tu, huku Ruvu Shooting ikiwa na sare tano kufunga mara mbili na kufungwa mechi moja.
Kufuatia mwenendo huo, kiongozi wa timu ya Azam ambayo ni moja ya timu kali mwaka huu, amekiri wazi kwamba timu za Simba na Yanga siyo tishio kwake kuliko timu za JKT zilivyo.
Ameesema kwamba timu hizo zinacheza mchezo wa ushindani na siyo rahisi kuzifunga.