Mwalimu wake alikuwa akifundisha soka la kitabuni. Ni ule mpira ambao timu inatandaza kwa pasi nyingi, weka mpira chini na mfanye adui autafute kwa ‘tochi’. Kipindi hicho Arsene Wenger alikuwa na wachezaji wazuri wenye vipaji lakini hawakuwa na majina makubwa.
Tangu alipokiondoa kizazi cha ‘Invicible’ cha akina Thiery Henry, Patrick Vieira,Lauren Etame Mayer, Nwankwo Kanu na wengineo alikuja na kizazi cha akina Abou Diaby,Kierab Gibbs,Denilson, Mikel Arteta, Emmanuel Eboue, Fabregas na wengineo. Kipindi hicho cha mwisho Arsene Wenger alikuwa akiwafanya wapinzani wao wautafute mpira kila wakati. Kwa sababu mara zote timu yake ilikuwa inaumiliki.
Katika kikosi chake hakukuwa na mastaa wakubwa na walikimbiwa na wengi lakini hakutetereka na kila msimu alifuzu Ligi ya Mabingwa. Kati ya vijana waliorithi mikoba ya Arsene Wenger ni Mikel Arteta. Kocha huyu wa Arsenal yuko sambamba na mchezaji mwenzake wa zamani Edu Gaspar. Kwa wanaomfahamu Edu wanakumbuka jinsi alivyotumia vyema guu lake la kushoto akiwa pale katikati ya dimba.
Edu alikuwa miongoni mwa wahimili wa kiungo cha Arsenal enzi za Wenger na miongoni mwa vipaji vilivyotambulishwa na kocha huyo kwenye Ligi Kuu ya England. Sasa Edu Gaspar ndiye Mkurugenzi wa Arsenal ikiwa na maana wanafahamu utamu wa timu kutandaza kandanda maridhawa. Edu baadaye alihamia Valencia ya La Liga. Lakini ni kati ya wachezaji waliopendwa na Wenger.
Nyakati za mwisho za Wenger hakuchukua ubingwa lakini timu yake ilifurahisha mashabiki wengi. Katika kipindi cha uongozi wa Edu na Mikel Arteta imeshuhudiwa Arsenal ikicheza soka safi na kuvutia wengi. Ni jambo la kawaida kwa mashabiki na wachambuzi wa mpira wa miguu kueleza kuwa Mikel Arteta anafundisha soka kama la Pep Guardiola na Arsene Wenger.
Baadhi ya wachambuzi wanasema Mikel anafundisha kile alichokuwa akikifanya Manchester City. Kwamba mchezo wao unakuwa na pasi nyingi, kutawala mchezo na kuhakikisha mpinzani hana muda wa kumiliki mpira kama wao. Ni mchezo ambao umezoeleka kwa kocha wa Man City Pep Guardiola tangu akiwa Barcelona B na baadaye kikosi cha wakubwa amekuwa akifundisha mchezo huo.
Mikel Arteta katengeneza kapu moja
Kama kuna makocha ambao wanafanana na mbinu za Mikel ni Arsene Wenger na Pep Guardiola. Aina yao ya ufundishaji zinafanana kwa maana ya kucheza mpira mwingi, pasi nyingi na kuwatawala kwa wingi wapinzani wao. Mbinu hii hufanya kazi kwa maana ya kuwashambulia wapinzani wao muda mwingi wa mchezo. Akili ya kwanza ya timu kila inapoingia uwanjani ni kuhakikisha inashambulia kuanzia mwanzo wa mchezo hadi mwisho.
Timu inayofanya hivi mara nyingi inakuwa na wachezaji wenye vipaji vikubwa na wale wanaoitwa kisoka ‘viungo visheti’. Hawa ni viungo wanaong’arisha timu kwa ubunifu na uwezo wa kupangua ngome za adui. Mabao yao yanapatikana kwa kupigiana pasi nyingi. Maandalizi yao ya kutafuta bao (build up) yanaonekana wazi na mpangilio wake unawavutia wengi.
Hayo ni matokeo ya ufundi ambao Arteta ameuchota kwa Pep Guardiola na mwalimu wake Wenger. Ingawaje Ppep Guardiola anayo mataji mengi kutokana na mtindo wake wa kucheza lakini amejikuta akipoteza mechi muhimu ikiwemo fainali ya Ligi ya Mabingwa mbele ya Chelsea ya Thomas Tuchel.
Pep alipoteza mechi hiyo kizembe kwa sababu alikadiria vibaya na kumweka pembeni mchezaji wa kiungo mkabaji. Katika kapu hili Wenger na Pep wana mchango mkubwa katika ufundishaji wa Arsenal ya Mikel Arteta na uongozi wa Edu. Lakini wawili hawa wamegundua kitu kimoja muhimu. Kisome hapa chini.
Jose Mourinho amemshtua Mikel Arteta?
Ni dhahiri Mikel Arteta anautaka ubingwa kwa mbinu zozote zile. Miongoni mwa mambo ambayo Mikel ameyaongeza katika kikosi chake ni kuhakikisha anaifanya timu yake icheze hata kwa mbinu nyeusi. Mbinu hizi ni zile ambazo zinamfanya mpinzani anayetandaza soka kwa wingi, yaani anapiga pasi nyingi na kutengeneza mabao kwa wingi aendelee na uhuru huo lakini Arenal yake yote inakuwa kwenye eneo lake la kujihami.
Ingekuwa katika soka la Tanzania, mashabiki wangemkumbuka kocha wa zamani wa Taifa Stars, Marcio Maximo. Kocha huyo alipendelea mfumo wa 4-5-1 kwa kuifanya timu yake ijihami zaidi na kushambulia kwa kushtukiza. Kocha anaifanya timu icheze kwenbye mstari aliopanga na kushambulia mara chache, huku muda mwingi inazuia na kuwazibia wapinzani mianya yote ya kutaka kufunga bao katika lango lao.
Katika ligi ya EPL Jose Mourinho alikuwa maarufu kwa mbinu hizi mara alipochukua jukumu la kuinoa Chelsea mwaka 2004 ilipokuwa ikilimiwa na tajiri wa Urusi, Roman Abramovich. Mourinho alisifika kwa soka la shoka tena lile la kujihami. Timu yake ilikuwa inacheza mchezo wa kujilinda zaidi lakini ilikuwa ikipata matokeo mazuri.
Chelsea walifanikiwa kunyakua mataji mbalimbali walipokuwa na Mourinho. Licha ya kulalamikiwa mbinu zake za kihuni na kujihami, lakini Mourinho aliwajibu alikuja England kutwaa ubingwa. Hicho ndicho alichokifanya alipokuwa Chelsea, Inter Milan, Real Madrid, Tottenham Hotspurs,Man United na AS Roma.
Kwa maana hiyo Mikel Arteta na Edu bila shaka waliketi mezani kujadiliana na benchi zima la ufundi kuhusiana na mbinu za kutafuta ubingwa hadi kwa mbinu nyeusi au chafu za kijilinda. Arteta amekuja msimu huu akiwa mwingine kwenye mechi kubwa dhidi ya Man City ambapo walitoka suluhu 2-2. Ni moja ya mechi zilizoonesha dhahiri Arteta amejifunza kitu kutoka kwa Jose Mourinho.
Arteta aliwaona Real Madrid
Carlo Ancelotti alisafiri hadi jijini Manchester kwa ajili ya kukabiliana na Manchester City kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa msimu uliopita. Mchezo wa kwanza Ancelotti aliambulia sare 1-1 na aliahidi kuwa Real Madrid haitolewi na timu moja mara mbili.
Katika mchezo wa kwanza Ancelotti aliwapa jukumu mawinga wake wawili Rodrygo na Vinicius Junior kucheza upande wa kushoto kwa wakati mmoja hali iliyowachanganya Man City kujua nani hasa alipangwa upande huo.
Man City walivurugwa kwa mbinu hiyo. Hata hivyo mchezo ambao Mikel Arteta alinufaika nao ni ule wa marudiano pale Etihad Stadium. Pep Guardiola alitupwa nje ya mashindano baada ya kufungwa kwa njia ya matuta. Real Madrid wlaiingia na mbinu zao nyeusi na walihakikisha wanajihami muda wote wa mchezo na kushambulia pale walipotaka.
Man City walihangaika kupenya ngome ya Real Madrid ili kuibuka na ushindi lakini walishindwa. Kama kuna mchezo na mbinu zilizompa akili Mikel Arteta basi ni mechi hiyo. Hapo ndipo tumeshuhudia Mikel Arteta akipambana na Man City kwa mbinu zilezile za Real Madrid. Ameifanya Arsenal kuwa na mabeki wenye roho ngumu na wakatili kiwanjani. Na kwa hakika alimvuruga Pep Guardiola. Hii ina maana Mikel Arteta anautaka ubingwa liwake jua au lisiwake, iwe kwa mbinu chafu na nyeusi au halali. Huyu Mikel Arteta wa sasa ni balaa na nusu.