DAKIKA 15 za kwanza za mchezo kati ya wenyeji Manchester City dhidi ya bingwa mtetezi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Real Madrid zilikuwa nzuri na majukwaa yote yalionesha furaha kwa mashabiki wake. mashabiki waliimba nyimbo zao, waliwatania Real Madrid na kuwakebehi huku wakitambia tuzo ya mchezaji bora Rodri ambaye alikuwa benchi kwa majeruhi aliyopata Septemba mwaka 2024.
Ujumbe wa mashabiki ulikuwa unakwenda kwa Real Madrid ambao waligomea kuhudhuria hafla ya utoaji wa tuzo za Ballon D’or jijini Paris. Lakini filimbi ya mwisho ya refa Clement Turpin ilipopulizwa kuashiria kukamilika dakika 90 za mchezo huo matokeo ya yalikuwa 3-2. Manchester City walikula kipigo wakiwa kwenye dimba lao la nyumbani la Etihad. Man City waliumizwa zaidi pale walipomuona mchezaji wao waliyempika Brahim Diaz akisawazisha bao la Erlin Haaland na ubao kusomeka 2-2 katika dakika 86. Katika dakika za nyongeza ndipo Jude Bellingham alipokimbia kwa kasi kuwahi mpira uliopanguliwa na golikipa wa Man City, Ederson na kusukumia wavuni. Lilikuwa bao lenye kila aina ya maumivu kwa Mna City katika msimu ambao wamekumbana na matokeo mabaya zaidi.
Magoli mawili ya Erlin Haaland yalionekana kama vile Man City wangekuwa na mchezo mzuri na kuwa na akiba mkononi kuelekea mchezo wa marudiano nchini Hispania. TANZANIASPORTS inachambua kwa kina juu ya Man City kuharibu mechi yao wenyewe katika usiku wa jumanne kwenye Uefa.
Majeruhi wengi Etihad
Man City iliingia kipindi cha pili bila beki wake Manuel Akanji aliyeumia. Akanji alikuwa mchezaji mwingine aliyeingia kwenye orodha ya majeruhi wa Man City. Kama kuna kitu kimewagharimu Man City msimu huu basi ni majeruhi wengi katika kikosi chao. Hata upande wa Real Madrid nao wanakabiliwa na tatizo hili ambalo linaharibu mechi zao nyingi. Mabeki wake wa kati hawapo, Eder Militao, Antonio Rudiger, David Alaba, Lucas Vazquez na Dani Carvajal. Katika hoja hii Man City wanaweza kujitetea na kwa hakika imewaumiza kuwakosa wachezaji wake muhimu. Kwa mfano wakati mchezo ukiendelea winga Jack Grealish alitolewa uwanjani baada ya kuumia, na nafasi yake ilichukuliwa na Phil Foden. Hii ni dhahiri kuwa timu hiyo ilikuwa inayumba, ukizingatia Grealish ndiye aliyepika bao la kwanza la Man City. Kumpoteza winga kama huyu tayari ilikuwa inapata pengo ambalo kuliziba inabidi mkakati maalumu wa kocha na wachezaji wake.
Kuyumba kwa beki wa kulia
Kyle Walker amehamia AC Milan ya Italia kwa mkopo hadi mwishoni mwa msimu. NI Walker ndiye alikuwa anamudu mpambano na winga hatari wa Real Madrid, Vinicius Junior. Walker na Vini walikuwa washindani wakubwa kila timu hizo zinapopambana, lakini kwenye mchezo huu Walker hakuwepo. Badala yake Man City walijikuta wakikosa mtu sahihi wa kumdhibiti Vinicius hasa baada ya Manuel Akanji kuumia. Ni Akanji ndiye alikabidhiwa jukumu la kupambana na Vini kwenye mchezo huo, lakini akawafanya mashabiki wa Man City waumie zaidi kwa ushindi wa timu yake. Rico Lewis hakuweza kumdhibiti Vini, kwa sababu alikuwa akicheza nafasi mbili kwa wakati mmoja. Vinicius Junior alikuwa kama mshambuliaji aliyekuwa akibadilishana nafasi na Kylian Mbappe.
Hivyo upande wa kushoto wa Real Madrid ulikuwa na wachezaji wawili wenye jukumu la kuisukuma nyuma Man City, huku Jude Bellingham akiwa nyuma yao. ndani ya dakika 10 tangu kuanza kwa mchezo huo, Man City walishuhudia umahiri wa Real Madrid kupitia Jude, Mbappe, Vini na Rodrygo. Mara kadhaa Vini aliwacheza shere Ruben Dias ikiwemo kucheza kwa kasi na mbio nyingi hali ambayo mabeki wa Man City wakafanya makosa mengi, eneo la beki wa kulia wa Man City halikuwa imara katika mchezo huo.
Mgongano wa majukumu
Nathan Ake, Manuel Akanji, Ruben Dias na John Stones ni mabeki wa kati kwa asili. John Stones anaweza kucheza kiungo mkabaji, lakini hawezi kumpa kila kitu kocha wake kinachotolewa na mchezaji wa eneo hilo. Bao la kwanza la Real Madrid ililitokana na kukosekana mawasiliano kati ya mabeki wa kati na pembeni kulia. Akanji aliingia eneo la 18 huku John Stones akiwa hana mwendo wowote wa kueleka langoni kwa sababu alitegemea Ake na Dias wafanye kazi ambayo alitakiwa kushirikiana nao. Mabeki wa Man City ni wazuri na hodari kwa muda mrefu, lakini msimu huu kila wanahcokifanya dhidi ya timu zenye maarifa makubwa ni makosa mengi yanayowafanya wapoteze mchezo.
Nathan Ake alikuwa analinda lango kuelekea kushoto kwake, Ruben Dias alitakiwa kuongoza safu ya ulinzi kwa kucheza karibu na kiungo mkabaji (John Stones), huku Manuel Akanji akikaba kueleka kulia. Mgongano wa mabeki hawa ulisababisha mara nyingi wajikute wote watatu wakiwa kwenye eneo la 18 bila kuchukua jukumu la kukabana na wapinzani wao kueleka upande upi.
Kilichotokea si ile Man City ambayo ingeweza kuondosha hatari kwa kupigiana pasi nzuri na umiliki bora wa mpira, lakini walikuwa wanabutua ili kuondoa hali ya hatari. Kazi nyingine iliyokuwa ngumu kwao ni kujaribu kukabana na mtu na mtu badala ya kukaba nafasi. Bao la pili la Real Madrid, mpira ulimkuta Brahim Diaz akiwa peke yake bila walinzi, na hivyo akapiga mpira kwa mguu wa kulia na kutinga kimyani. Eneo alilokuwepo Brahim Diaz ndilo lilitakiwa kuwepo kwa mabeki wawili wa kuziba nafasi ile huku mmoja akiwa na jukumu la kumkaba Diaz.
Lakini yote mawili hayakufanyika, kuziba nafasi na kumkaba Diaz hivyo basi wakajikuta wanaruhusu bao la kusawazisha. Kwenye bao la tatu Man City angalau walikuwa wameweka ulinzi mzuri, kwani wakati Jude Bellingham anaenda kutumbukiza mpira ule wavuni alikuwa amepambana na changamoto ya beki wa Man City, hivyo ndivyo wanavyopaswa kuwa kuliko makosa waliyofanya.
Mawasiliano katika vipande vitatu vya Man City
Ile hali ya umwamba, kupiga pasi maridadi, kumfikia mlengwa, kupanga mashambulizi kwa mtindo mtamu na wa kuvutia unaonekana kuondoka kwa Man City. Pep Guardiola ana kazi moja nzito sana, kuhakikisha Man City inacheza kama timu yenye mawasiliano kuelekea lango mwa adui au kiungo na ulinzi. Ukitazama mechi hii, Man City walikuwa mbali katika utawala wa pasi nyingi, ingawaje menchi tangu mwanzo ilionesha kuwa ni mali yao. kutoka safu ya ulinzi hadi viungo kuna mapengo ambayo yanavunja mawasiliano. Wachezaji wanaonekana wanataka kufanya kitu, lakini kila wanapopata mpira na kujaribu kuunganisha, timu yao inavunjika kipande cha ulinzi ambacho hakiwezi kupandisha mashambulizi, kisha kipande cha viungo kinaonekana kukosa ubunifu, huku washambuliaji wanataka kupachika mabao tu bila mpango.
Kuna wakati Erlin Haaland anapigiwa pasi ndefu ili apambane na mabeki bila kujali mpango wao wa kusaka bao utakuwaje. Unabaki unashangaa, Man City ile yenye nakshi nakshi za kutosha imemenda wapi? Ule umwamba wa kupiga pasi, kuandaa mashambulizi na namna mabao yanavyopikwa unaona wazi Man City walikuwa watawala kwenye mchezo. Lakini Man City iliyocheza na Real Madrid inaendelea kuvunjika vipande na mawasiliano hakuna.